Mabalozi wa nchi za Ulaya na Marekani wameitaka Tume
Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) kuhakikisha kuwa uchaguzi
mkuu wa Agosti 8, unafanywa kwa njia huru na ya haki.
Katika misa maalum iliyoandaliwa na Kanisa la Kianglikana la All
Saints na kuhudhuriwa na mamia ya Wakenya kutoka matabaka mbalimbali,
mabalozi kutoka nchi za bara la Ulaya – Uingereza, Uholanzi, Uswisi na
Denmark – pamoja na Marekani wamelaani vikali mauaji ya kinyama ya
mwishoni mwa wiki dhidi ya afisa mmoja wa tume ya uchaguzi na mipaka
IEBC na wakaishinikiza serikali na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa
haraka."Ningependa kusema tu kwamba tunalaani mauaji hayo… Kuhusu uchunguzi huo tunaweza kuwa tayari kutoa msaada lakini kimsingi ni jukumu la serikali ya Kenya kuamua jinsi inavyotaka kuendesha [uchunguzi huo]," amesema Robert Godec, balozi wa Marekani nchini Kenya.
Godec amesema uchaguzi wa mwaka huu ni fursa yenye umuhimu mkubwa kwa Wakenya, kuudhihirishia ulimwengu kwamba wangependelea uthabiti wa kisiasa, demokrasia na maendeleo katika taifa lao.
"Wiki ijayo Wakenya watawachagua viongozi wao.. Ni fursa muhimu kuthibitisha kimsingi maamuzi yao ya katiba ya mwaka wa 2010 na kutuma ujumbe muhimu kwamba wangependa kuwa na demokrasia, usalama na maendeleo katika nchi yao.
Nafikiri huu ni wakati muhimu kwa Wakenya wote kutoka jamii zote kushikamana na kufanikisha shughuli hii. Kuufanya kuwa uchaguzi huru, wa haki na wenye amani," ameongeza Godec.

"Wafanyakazi wa Tume ya IEBC ni sharti wapewe ulinzi wakati huu wanapotimiza jukumu hili muhimu.. Inatupasa kuepukana na machafuko na kukataa kata kata maneno yanayochochea mapigano," amesema Nic Hailey.
Marekani na Uingereza ni miongini mwa wafadhili kutoka jumuiya ya kimataifa ambao wanatoa misaada ya aina mbali mbali kwa taifa hili, ikiwemo miradi yenye lengo la kuimarisha demokrasia na utawala bora.
Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wakazi wa jiji la Nairobi wanaendelea kukimbilia sehemu za mashambani kutokana na hofu ya uwezekano wa kutokea ghasia.
Kenya ipo katika kampeni za mwisho kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Agosti tarehe 8.
Uchaguzi mkuu wa mwaka huu unatazamiwa kuwa na ushindani mkali baina ya mgombewa wa chama cha Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta anayegombea muhula wa pili dhidi ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga, mgombea wa muungano wa upinzani, NASA.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment