Mwanzilishi wa kampeni ya
“Tanzania ya Viwanda Inawezekana” Bw. Emijidius Cornel (katikati) toka
Chuo cha DUCE akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) baadhi
ya michoro iliyochorwa na wanafunzi wanaowafundisha kwa kujitolea,
kulia ni Ngenda Nkwabi mjumbe wa zoezi hilo na kushoto ni Mwanafunzi wa
Uandishi wa Habari ,ambaye yuko kwenye mafunzo kwa vitendo Idara ya
Habari (MAELEZO) Neema Mathias.
Mjumbe wa kampeni ya “Tanzania ya
Viwanda Inawezekana”, Bw. Ngenda Nkwabi (kulia) akieleza kampeni hiyo
kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es
Salaam katikati ni mwanzilishi wa kampeni hiyo Bw. Emijidius Cornel na
kushoto ni Mwanafunzi wa Uandishi wa Habari, ambaye yuko kwenye mafunzo
kwa vitendo Idara ya Habari (MAELEZO) Neema Mathias.
Picha na Paschal Dotto -MAELEZO
…………………………..
Na Neema Mathias- MAELEZO
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki
cha Elimu Tanzania (DUCE) Wameiunga mkono kauli ya Rais John Pombe
Magufuli ya Tanzania ya Viwanda kwa kujitolea kufundisha masomo ya
Sayansi kwa baadhi ya shule za Sekondari Wilayani Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo Jijini Dar es Salaam. , Mwenyekiti wa kampeni ya “Tanzania ya
Viwanda Inawezekana”, Emijidius Cornel amesema wanachuo wa DUCE wameamua
kutumia muda wao wa ziada kufundisha masomo ya sayansi kwa shule za
sekondari.
“Waalimu wa masomo ya sayansi
tumeamua kujitolea kufundisha bila malipo masomo hayo katika baadhi ya
shule za sekondari ambazo zina upungufu wa waalimu wa sayansi, kwani
maendeleo ya viwanda yanahitaji wataalamu,” alisema Cornel.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa,
walianza kujitolea rasmi Februari 16, 2017 kwa lengo la kumuunga mkono
Rais Magufuli kwa kuhamasisha wanafunzi kuyapenda na kuyapa kipaumbele
masomo ya Sayansi shuleni ili kuongeza ufaulu wa masomo hayo.
Aidha, Cornel alieleza kuwa
wameanzisha matamasha kwa shule za sekondari Temeke yatakayo fanyika
Oktoba 6 na Novemba 18 mwaka huu, kwa lengo la kuendelea kuwapa moyo
wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo
ameiomba Serikali na wadau wengine wenye uzalendo na nchi yao
kuchangia na kuunga mkono kampeni hiyo, kwani muda mwingine wanakumbana
na changamoto mbalimbali ikiwemo nauli za kuwafikia wanafunzi
walioko kwenye shule za mbali na maeneo ya chuo .
“Tunaiomba Serikali pamoja na
wadau mbalilmbali watuunge mkono katika suala hili kwani tumeanza kwa
moyo mkunjufu na tunaomba tusikwamishwe na mtu yeyote yule, kwa wanotaka
kutuunga mkono wanaweza kuwasilisha michango yao kupitia akaunti namba
20701100005 NMB yenye jina la Kibasila Sekondari, tawi la Temeke au
kupitia namba 0718883718”, alieleza Cornel.
Pia ameiomba Serikali kutoa hamasa
kwa vyuo vingine vya Ualimu nchini kufanya kazi ya kujitolea kufundisha
wanafunzi shuleni katika manispaa mbalimbali ili kukabiliana na
changamoto ya waalimu wa masomo ya Sayansi kote nchini.
Kwa upande wake, Mjumbe wa kampeni
hiyo, Ngenda Nkwabi amewataka vijana kuwa wazalendo na kuacha kutumia
muda mwingi kuchati kwenye mitandao ya kijamii na kufanya mambo yasiyo
ya msingi, badala yake kutumia muda huo kutoa elimu kwa wanafunzi
walioko shuleni katika ngazi za elimu ya sekondari.
Aidha, Nkwabi alisema kuwa
anaamini wanafunzi wengi wanapenda masomo ya Sayansi lakini kutokana na
kukosekana kwa waalimu wa kutosha katika shule nyingi wanafunzi hao
huishia kuona ugumu na kuyachukia masomo hayo, hivyo anaiomba Serikali
kuwapa ushirikino katika kampeni hiyo ili kumaliza kabisa tatizo hilo.
SHARE
No comments:
Post a Comment