Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya kupokea
Taarifa ya Kamati Maalumu ya Bunge ya Kuchunguza Madini ya Almasi na
Tanzanite Ikulu jijini Dar es Salaam.
Na: Mwandishi Wetu, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amepokea ripoti mbili za Kamati
Maalum za Bunge za Uchunguzi wa madini ya Tanzanite na Almasi na
kusisitiza kuwa yeye yupo Ikulu kufanya kazi wala si kutafuta mchumba.
“Watanzania tumechezewa kwa miaka
50, sasa ni wakati wa kufanya kazi; lazima tuamke tukatae kuibiwa huku
tunakoimbiwa sasa kama kwamba tumerogwa” alisema Dkt. Magufuli mara
baada ya kukabidhiwa ripoti hizo.
Aliwaambia viongozi na wananchi
waliokuwa wakifuatilia tukio hilo kupitia vituo vya televisheni, redio
na mitandao ya kijamii kuwa Ikulu ni sehemu ya kupita na yuko radhi
aonekane mwanasiasa mkorofi asiyependwa lakini lazima atatekeleza jukumu
lake la kutetea na kulinda rasilimali za taifa kwa manufaa watanzania
wote wa leo, kesho na mtondogoo.
Alibanisha kuwa fedha zinazoibiwa
kwa matrilioni zingetosha kubadili maisha ya watanzania wengi kwa
kuwapatia huduma za jamii na hata kulipana mishahara mikubwa hivyo akiwa
Rais hawezi kukubali hilo liendelee.
“Tuangalie maisha yetu yalivyo
kila mmoja amuangalie jirani yake anavyoishi maisha ya shida huku
rasilimali zote zikiibiwa na watu wakituacha katika umasikini”alieleza
Rais Magufuli na kuongeza kuwa wanyonyaji hao hawana huruma kabisa na
watanzania.
Akionesha kuchukizwa na matokeo ya
ripoti hizo, Rais Mafuguli alisema kama baadhi iliyoelezwa kuwa udhaifu
huo unatokana na mfumo basi huo mfumo lazima ufumuliwe.
“Unaposaini mikataba ya aina hii
na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inahusika basi kama ni mfumo tuufue ili
tufikie mahala maslahi yetu ya nchi yapewe kipaumbele” alisisistiza Rais
Magufuli na kuongeza kuwa “Tukienda kwa utaratibu huu, tutakuwa watumwa
milele”
Katika hotuba yake hiyo, Rais
alisema mambo mengine ni aibu kuyasema na kusisitiza kuwa yeye hataki
baada ya kumaliza muda wake kuwa miongoni mwa wale wanaotajwa kuwa “Nae
alikuwepo hapa“
Alisema yeye binafsi angependa
kuona watanzania wanakuwa matajiri kutokana na rasilimali zao si
kuwanufaisha watu wa nje na makuwadi wao wa ndani ambao aliwaeleza kuwa
watu waliokosa uzalendo.
Alizipongeza ripoti hizo kuwa
zimekidhi matarajio yake na kwamba zimempunguzia kazi ya kutafuta
wataalamu wengine kuchunguza jambo hilo na kulipongeza Bunge kwa
kutimiza wajibu wake huo vyema.
Katika mnasaba huo alimuagiza
Waziri Mkuu kuwaita wataalamu wa sheria washirikiane na Bunge kukaa
pamoja na kufanya marekebisho ya sheria.
“Tusiulizwe kwa nini tunabadili
sheria hivi sasa kwani jibu ni wazi kuwa huu ndio wakati unaofaa kufanya
hivyo” alisisitiza Rais Magufuli.
Katika mkutano huo alivipongeza
vyombo vya habari kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhabarisha wananchi na
akatoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea kuelimisha wananchi wajitambue na
kuwa wazalendo.
SHARE
No comments:
Post a Comment