Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza na washiriki wa kongamano la
Shirikisho la Vyuo na Vyuo vya Elimu ya juu CCM Zanzibar huko katika
hoteli ya Bravo Kiwengwa Mkoa kaskazini Unguja.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Dk. Mohamed Seif Khatib akizungumza katika kongamano hilo.
Baadhi ya vijana wa Shirikisho la Vyuo na vyuo vya elimu ya juu CCM Zanzibar wakishangilia katika shirikisho hilo.
…………………………
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dk. Abdulla Juma Mabodi amewataka vijana wa chama hicho kuchangamkia
fursa za kielimu zinazotolewana serikali ili kupata wasomi
watakaoendeleza misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo.
Rai hiyo ameitoa wakati
akizungumza na vijana wa chama hicho katika kongamano la kuwajengea
uwezo vijana lililoandaliwa na Shirikisho la Vyuo na Vyuo vya Elimu ya
juu CCM Zanzibar, lililofanyika katika hoteli ya Bravo Kiwengwa Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Alisema Chama cha Mapinduzi
kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kimeweka mikakati endelevu
ya kuhakikisha serikali inatoa kipaumbele kwa sekta ya elimu kwa lengo
la kuhakikisha vijana wanasoma na kupatikana kwa viongozi na wataalamu
waliobobea katika fani mbali mbali.
Dk.Mabodi alieleza kwamba mara
baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 waasisi wa CCM walitoa fursa ya elimu
kwa kuanzisha mfumo wa elimu bure kwa nia ya kuhakikisha watoto wa
wanyonge wanapata elimu ili baadae waweze kujitawala.
“Vijana wa CCM tumieni fursa ya
elimu vizuri kwani serikali imeimarisha mfumo wa elimu kuanzia ngazi za
maandalizi mpaka vyuo vikuu hivyo hakuna sababu ya kushindwa kusoma.
Maendeleo ndani ya chama chetu
yataimarika endapo kutakuwa na vijana makada waliosoma fani mbali mbali
za kiuchumi, kijamii na kisiasa ambao watakuwa na uwezo wa kujenga hoja
zenye nguvu zitakazolinda heshima ya chama chetu”, alisema Dk.Mabodi.
Akifungua kongamano hilo Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Dk. Mohamed Seif Khatib aliwataka vijana
waliopata fursa ya elimu ya juu kuwa wabunifu wa masuala mbali mbali
yatakayoweza kuisaidia nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni.
Alisema matarajio ya Chama cha
Mapinduzi na serikali ni kuona vyuo vikuu vinazalisha vijana wenye
weledi na uwezo wa hali ya juu katika kuchanganua na kushauri mambo
yenye tija na manufaa kwa wananchi wote.
“ Rika la vijana ndio nguvu kazi
ya taifa lolote duniani na Chama cha Mapinduzi tunajivunia kuwa tunao
vijana waliobobea katika fani mbali mbali hivyo tunaamini kupitia wingi
wenu mtaendelea kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo yatakayoweza kuleta
manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”, alieleza Dk. Seif.
Dk. Seif aliwataka vijana
kuendelea kuwa wazalendo ili chama cha mapinduzi kiweze kushinda na
kusimamisha serikali kwa kila uchaguzi mkuu wa Dola.
Naye Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya
Mjini, Baraka Shamte ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho,
akitoa mada ya Zanzibar ilipotoka, ilipo hivi sasa na inapoelekea
alisema historia ya Zanzibar ndio somo pekee litakalowajengea uwelewa
mzuri vijana wa sasa.
Alisema kuwa kabla ya Mapinduzi ya
Zanzibar mwaka 1964 nchi ilikuwa katika dhiki na mateso makubwa
yaliyotekelezwa na watawala wa wakati huo dhidi ya wananchi.
Alisema maendeleo yaliyopo nchini
yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa CCM wanaosimamia kwa
nguvu zote sera za maendeleo na kukuza uchumi kama walivyoaidi kupitia
Ilani ya uchaguzi ya chama ya mwaka 2015/2020.
SHARE
No comments:
Post a Comment