Sehemu ya mzigo wa almasi uliokamatwa ambao thamani yake ni zaidi ya Shilingi bilioni 64.
****
ALMASI zenye uzito wa kilogramu 29.5 za
thamani ya zaidi ya Sh bilioni 64, ambazo zilibakiza dakika tano tu
kutoroshwa kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam
(JNIA) kwenda ughaibuni, zimetaifi shwa na serikali.
Aidha, watumishi wa serikali na maofisa
wa Mgodi wa Almasi wa Williamson wa Mwadui Shinyanga, waliohusika na
uthaminishaji wa awali wa almasi hizo na kudanganya kuwa zilikuwa na
uzito wa kilogramu 14 tu, watachunguzwa na kuchukuliwa hatua kali za
kisheria.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akipokea ripoti
ya timu ya wataalamu, iliyoundwa kuchunguza upya uzito na thamani halisi
ya almasi hizo baada ya kuzikamata katika uwanja huo wa JNIA Agosti 31,
mwaka huu.
Uthamini uliofanywa awali kwa almasi
hiyo, iliyokuwa mbioni kupakiwa ndani ya ndege kutoroshewa nchini
Ubelgiji, ulieleza kuwa ilikuwa na thamani ya chini ya Sh bilioni 32,
huku ikielezwa pia kuwa na kilogramu 14, taarifa zilizogundulika kuwa
zilikuwa ni za uongo.
Jana Waziri Mpango alipokea maelezo ya
almasi hiyo kutoka kwa Kiongozi wa Jopo la Wataalamu waliofanya uthamini
mpya, Profesa Abdulkarim Mruma na wasaidizi wake. Baada ya kuridhika na
maelezo, yaliyodhihirisha kuwepo kwa kiwango cha juu cha udanganyifu
kuhusu uzito na gharama za almasi hiyo, kwa lengo la kuliibia taifa,
Waziri Mpango aliagiza almasi hiyo yote kutaifishwa, kupigwa mnada na
fedha zitakazopatikana kuingia serikalini.
Aliagiza pia kuwajibishwa kwa maofisa wa
serikali waliohusika katika udanganyifu huo kwa wahusika hao kukamatwa,
kuchunguzwa mali zao ikiwemo majumba, mashamba, magari kuona kama
vinaendana na mishahara yao na baadaye kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria.
Alisema, Watanzania wamechoshwa kuona
mali zao zikiibiwa kila kukicha huku serikali ikikosa mapato makubwa
kutokea katika rasilimali hizo. Pia, aliagiza kuandaliwa kwa wataalamu
wa madini na wapelekwe kwenye migodi haraka, kukabiliana na wizi wa aina
hiyo, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na wizi
wa aina hiyo.
Waziri Mpango aliagiza pia upimaji wa
madini kufanyikia kwenye eneo la migodi, na pia kununuliwa kwa mashine
za kupimia madini kwenye maeneo ya migodi, baada ya kuelezwa na Profesa
Mruma kuwa ukosefu wa vifaa vya kupimia ni chanzo cha udanganyifu huo.
“Kazi nzuri sana umefanya Professa Mruma
na wenzako na kwa sasa ninaagiza haya madini tuliyokamata hapa,
kulindwa kuanzia hapa hadi pale yatakapoingizwa sokoni, pia ninamtaka
Gavana wa Benki Kuu (Profesa Benno Ndulu) kuanza kuhifadhi madini ya
vito na si fedha peke yake.
“Inashangaza kuona maofisa wa juu wa
Wizara ya Nishati na Madini waliokuwa na jukumu la kuthaminisha madini
haya wamedanganya huku wale walio chini yao wametoa tathmini ya kweli,
sasa huu ndiyo uzalendo unaotakiwa,” aliongeza Dk Mpango.
Kwa upande wa Mgodi wa Williamson
Diamond LTD, Waziri Mpango alisema kutokana na kubainika kujihusisha na
udanganyifu, huku kampuni hiyo ikieleza kupata hasara kila mwaka,
kuanzia mwaka huu itawajibika kutoa gawio serikalini na alimuagiza
Profesa Mruma kuijulisha Bodi ya Kampuni hiyo agizo hilo la serikali
mara moja.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salam, Lazaro Mambosasa akizungumzia agizo hilo,
alisema kuwa hakuna mtuhumiwa ambaye hatoshughulikiwa katika kosa hilo.
Alisema sheria itafuata mkondo na kuwa
kila mtu ambaye ameshiriki kwa namna moja au nyingine, atakamatwa
kuanzia wale waliopo mgodini hadi wale walioshiriki katika kutaka
kutorosha madini hayo.
Ulinzi mkali kisanduku cha almasi Katika
tukio hilo, lililorushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha TBC
1, kwa lengo la kuwaonesha wananchi namna madini yao yanavyohujumiwa,
kilioneshwa kisanduku kidogo kilichohifadhia madini hayo ya mabilioni ya
shilingi, kikiwa katika chumba chenye ulinzi mkali.
Kabla ya lango la chumba hicho
kufunguliwa, alionekana mlinzi akiwasiliana na watu mbalimbali ili
kupata ruhusa ya kufungua lango hilo licha ya kuwa mbele yake alikuwepo
Waziri wa Fedha na maofisa wa juu wa serikali na vyombo vya dola, hatua
inayodhihirisha kuwepo kwa mfumo thabiti wa kulinda almasi hizo.
Baada ya takribani kama dakika 30 za
kuwasiliana na watu wasiojulikana, hatimaye mlinzi huyo alisomewa
tarakimu, ambazo alianza kuziingiza katika kufuli la mlango huo na
hatimaye ulifunguka na kuwawezesha viongozi hao wa serikali kuingia
ndani.
Mlinzi huyo alitajiwa namba kwa awamu
mbili, ambapo awamu ya kwanza alitajiwa namba tisa tofauti na kisha kuja
kutajiwa namba tano tofauti na alipoingiza sefu hiyo ilifunguka, na
bado mlinzi huyo akafungua tena kufuli kadhaa, kabla ya kutoa kisanduku
hicho cha mbao kilichokuwa na madini hayo ya almasi.
Hata baada ya kukifikia, bado haikuwa
kazi rahisi kukifungua kisanduku hicho kwani kilikuwa kimefungwa na
makufuli mawili yenye lakiri; na iliwachukua Profesa Mruma na wenzake
zaidi ya dakika 15 kuvunja makufuli na lakiri hizo na baadaye kufungua
skurubu nne kwa kutumia bisibisi, hatimaye kutoa madini hayo.
Ingawa zilikuwa ndani ya vifuko vya
plastiki vyeupe, lakini kwa mara ya kwanza Watanzania wengi waliokuwa
wakifuatilia matangazo ya televisheni waliweza kujionea utajiri wa
rasilimali zao, na katika tukio la kushangaza zipo almasi ambazo
zilikuwa zikitoa nuru, iliyokuwa ikinakisi kioo cha miwani ya Waziri
Mpango na kutoa mwangaza wa kupendeza.
Baadaye Profesa Mruma na jopo lake,
walianza kutoa maelezo ya kitaalamu ya almasi hiyo, wakisema zipo za
aina tatu; za daraja la kwanza ambazo ni kubwa zikiwa zimechimbwa moja
kwa moja mgodini, za daraja la pili zenye ukubwa wa kati na za daraja la
tatu ambazo ni ndogo ndogo kama punje za sukari ambazo zinapatikana kwa
njia ya kuchekecha masalia ya almasi (Makinikia).
Walimuonesha Waziri pia kifuko chenye
almasi za rangi ya pinki, zinazopatikana Tanzania peke yake kwenye mgodi
huo wa Williamson Diamond wa Mwadui, Shinyanga, ambazo ndizo zilizokuwa
zinatoa mwangaza uliokuwa unaakisi katika miwani ya waziri na kutoa
mwangaza ambao zinaweza kuonekana hata kama kuna giza.
Viongozi wengine walioandamana na Dk
Mpango jana ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Charles
Kichere, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Biswalo Mganga, Naibu Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Brigedia Jenerali John
Mbungo, Kamishina wa Madini Benjamin Mchwampaka na Kamanda Mambosasa.
Ukaguzi huo ni mwendelezo wa harakati za
Rais John Magufuli za kukabiliana na wizi wa rasilimali za nchi, ambapo
mapema wiki hii alipokea ripoti kutoka kamati mbili za Bunge,
zilizochunguza biashara za madini ya Tanzanite na almasi na kubaini
udanganyifu, uzembe, rushwa na ubadhirifu mkubwa.
Ripoti za Kamati hizo zilizoundwa na
Spika wa Bunge, Job Ndugai zilitanguliwa na ripoti kuhusu Tume mbili
zilizoundwa na Rais ili kuchunguza kiwango cha madini ya dhahabu,
kinachopatikana kwenye mchanga wa masalia ya dhahabu (Makinikia)
unaosafirishwa nje ya nchi na athari zake kiuchumi, tume zilizobaini
Taifa kuhujumiwa kwa kiwango kisichovumilika.
IMEANDIKWA NA EVANCE NG'INGO- habarileo
SHARE
No comments:
Post a Comment