Na Hamza
Temba
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia
Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuhakikisha kuwa wananchi wote waliolima ndani ya eneo la hifadhi hiyo kinyume
cha sheria wanaondoa mazao yao pamoja na kusitisha kabisa shughuli zozote za
kibinadamu ndani ya hifadhi hiyo.
Prof. Maghembe ametoa agizo hilo jana wakati akiwa
kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyopo wilaya ya
Arumeru mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali
zinazofanywa na hifadhi hiyo ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.
Waziri wa Maliasili, Prof.
Jumanne Maghembe (kushoto) akiingia kwenye ofisi kuu ya Hifadhi ya Taifa ya
Arusha jana Mkoani Arusha katika ziara yake ya kikazi ya siku moja katika
hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro
kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA,
Dkt. Alan Kijazi. (Picha na Hamza Temba –
Wizara ya Maliasili na Utalii)
"Naagiza, kuanzia leo ni marufuku mtu yeyote
kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari hapa, atakayeonekana piga
pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani ya hifadhi tukae kimya, ni
lazima tuchukue hatua. Watangaziwe na wapewe muda wa kuondoa mazao yao, ndani
ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka", alisisitiza Prof. Maghembe baada ya kukagua
eneo hilo.
Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa
Waziri Maghembe, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga alisema eneo hilo
ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41 limekuwa na mgogoro tangu mwaka
1990 baada wananchi wa Kijiji cha Olkung'wado kuvamia eneo hilo huku wakitoa
hoja kadhaa ikiwemo madai kuwa shamba hilo ni maeneo yao ya asili waliyokuwa
wakimiliki tangu zamani.
Alisema hoja nyingine wanazozitoa ni kuwa walipewa
mashamba hayo na Serikali wakati wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka
1975 na 1976, Aidha, hoja nyingine ni kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato wakati wa ugawaji wa
mashamba hayo na kwamba TANAPA pia haina hati miliki ya mashamba hayo.
Ngada alisema hoja zote hizo zilikinzana na ukweli ya kwamba shamba hilo lilimilikishwa kwa TANAPA tangu mwaka 1980 baada ya
kutolewa tangazo kwa wadau wanaoweza kuliendeleza kufuatia muwekezaji wa awali,
James Preston Mallory kushindwa kuliendeleza na hivyo kufutiwa hati miliki na Mhe.
Rais mnamo mwaka 1979.
“Wadau mbalimbali waliomba umiliki wake ikiwemo
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Halmashauri ya Kijiji cha
Olkung'wado, lakini Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa Arusha ikaishauri
Serikali mashamba hayo yamilikiwe na TANAPA na hivyo tukaandikiwa barua rasmi
ya kukubaliwa kupewa shamba na Idara ya Ardhi Mkoa” alisema Ndaga.
Alisema TANAPA ilinunua eneo hilo lenye ukubwa wa
ekari 966 kwa lengo la kupanua hifadhi ya Taifa ya Arusha ambapo baada kupewa
shamba hilo, iliagizwa kulipa fidia ya mali zilizokuwepo, mwaka 1983 tathmini
ikafanyika na malipo yakalipwa Serikalini hatimaye TANAPA ikapewa barua ya kumiliki
ardhi mwaka 1988 (Letter of Offer). Alisema kwa upande wa Kijiji hicho cha Olkung'wado hakuna nyaraka yeyote inayoonesha
shamba hilo kupewa kijiji hicho.
Mhifadhi huyo alisema baada ya mgogoro wa muda
mrefu, wataalam wa TANAPA walifanya survey katika shamba hilo ili kubaini maeneo yaliyo na
shughuli nyingi za kibinadamu na yale yenye umuhimu zaidi kiikolojia,
mapendekezo yalitolewa kuwa maeneo yenye shughuli nyingi za kibinadamu yaachwe
kwa wananchi na yale yenye umuhimu kiikolojia yaendelee kuhifadhiwa, Bodi
ya TANAPA iliridhia ekari 366 zipewe wananchi na ekari 600 ziendelee
kuhifadhiwa.
“Baada ya kikao cha wadau wa uhifadhi
kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru tarehe 11 Mei, 2017 ambacho
kilijumuisha Madiwani, mwakilishi wa Mbunge, katibu tarafa, watendaji wa kata,
wenyeviti na watendaji wa vijiji, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na
wataalam wa halmashauri, ilifikiwa maazimio ambapo wajumbe waliridhia maamuzi
ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kuwapa wananchi ekari 366 ya shamba hilo na
kubakiwa na ekari 600” alisema Ndaga.
Aliongeza “Kikao hicho pia kiliridhia TANAPA kuweka
vigingi vya mpaka katika shamba hilo ambapo tarehe 14 Mei, mwaka huu, 2017 zoezi
hilo lilianza na jumla ya vigingi 26 viliwekwa”.
Alisema hata hivyo kumekuwepo na taarifa kuwa
baadhi ya wanakijiji wa Kitongoji cha Momella walifungua kesi mahakamani
wakidai wakidai kuwa kijiji cha Olkung'wado kimenyang'anywa ardhi yao na TANAPA, hata
hivyo Serikali hiyo ya Kijiji imekana kwa maandishi kuhisika na ufunguzi wa
kesi hiyo wakidai imefunguliwa na mtu binafsi na sio Serikali ya Kijiji hicho.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt.
Alan Kijazi alimuhakikishia Waziri Maghembe kuwa maagizo yote aliyoyatoa
ya kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo yatafanyiwa kazi
na atapewa mrejesho wa utekelezaji wake.
SHARE
No comments:
Post a Comment