
Kaimu Mkurugenzi wa Maadili toka
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw.
Lambert Chialo (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
(hawapo pichani) wakati akieleza umuhimu wa watumishi wa Umma kuzingatia
maadili kazini, kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini toka Ofisi ya Rais Bi. Mary Mwakapenda.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
…………………
Na. Georgina Misama – MAELEZO
Serikali kupitia Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewaonya watumishi wa
Umma kuacha kutoa taarifa za serikali za siri na za kawaida kwa watu ambao sio
walengwa wa taarifa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo Jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Maadili kutoka Wizara
hiyo Lambert Chialo alisema kwamba kwa mujibu wa sheria ya Usalama wa
Taifa Na. 3 ya mwaka 1970 na marekebisho yake, Ibara ya 5(a) na (b),
adhabu ya uvujaji wa siri ni kifungo kisichozidi miaka 20.
“Hivi karibuni tumeshuhudia
taarifa za serikali za siri zikitumwa katika vyombo vya habari pamoja na
mitandao mbalimbali ya kijamii kitu ambacho ni kosa kisheria na ni
kinyume cha Kanuni za Maadili ambapo inasisitizwa kuwa na matumizi
sahihi ya taarifa”, alisema Chialo.
Chialo aliongeza kwamba lengo la
serikali si kuficha taarifa kwa wadau wake, bali taarifa zinazotolewa
zinapaswa kutolewa kwa utaratibu maalumu na kupelekwa kwa watu
wanaopaswa kupokea taarifa hizo (walengwa). Aidha, taarifa zinazotolewa
na taasisi husika lazima zipate idhini kwa Uongozi husika kabla ya
kupelekwa kwa wadau.
Akiongelea suala la matumizi
mabaya ya Ofisi, Chialo alisema kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa
wakitumia nafasi walizonazo kwa manufaa yao binafsi na sio ya Umma, kwa
kufanya hivyo ni kosa kisheria na watumishi watakaogundulika
watawajibishwa kwa mujibu wa Kanuni na taratibu.
Watumishi wa Umma wanapaswa
kufahamu kwamba serikali inaendelea kufatilia matendo yote yasiyo ya
kimaadili na kuchukua hatua kila inapobidi. Aidha, wananchi wanaombwa
kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili katika
taasisi za umma kila wanaposhuhudia matukio hayo.
“Tunalo dawati la msaada kwa ajili
ya kupokea maoni, malalamiko, ushauri na taarifa mbalimbali katika
kuhakikisha utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi unaboreshwa”
alisema Chialo.
Chialo alitoa rai kwa wananchi
wote kwa ujumla, kuzingatia swala la maadili kuanzia ngazi ya familia.
Aidha, inasisitizwa viongozi na wasimamizi wa kazi kuendelea kuelimisha
watumishi kuhusu suala la maadili na kuhakikisha watumishi wanaishi kwa
kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa vitendo.
SHARE
No comments:
Post a Comment