FRANK MVUNGI- MAELEZO,
DODOMA.
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswaada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya
298 (The Public Service Act) itakayowezesha muda wa kustaafu kwa
Wahadhiri waandamizi, Maprofesa na Madaktari Bingwa kuwa miaka 60 kwa
hiari na lazima miaka 65.
Akizungumza wakati akiwasilisha muswaada huo Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Mhe. George Masaju amesema kuwa marekebisho katika jedwali
yanapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 25A ambacho kinaainisha kuhusu
umri wa kustaafu ambapo kwa sasa sheria ilivyo haina masharti hayo
isipokuwa umri wa kustaafu umetajwa katika sheria zinazoanzisha mifuko ya
hifadhi za jamii.
Aliongeza kuwa, uzoefu umeonyesha kuwamba Maprofesa na Wahadhiri
waandamizi wa vyuo Vikuu vya Umma pamoja na madaktari Bingwa wa
Binadamu wa Hospitali za Umma wamekuwa wakihitajika kuendelea kutoa huduma,
utaalamu na uzoefu wao licha yakufikisha umri wa miaka 60 kwa sasa ya kustaafu
na hivyo kulazimika kuajiriwa na Serikali kwa mikataba.
Hatua yakuwaajiri wataalamu hao kwa mikataba baada ya kustaafu imetajwa
kuongeza gharama kubwa kwa Serikali ambapo muswaada ulipitishwa
unawezesha Serikali kuokoa Kiwango kikubwa cha fedha zilizokuwa zikitumika
katika kuwalipa wataalamu wao mara baada ya kustaafu ili waweze kufanya kazi kwa
mikataba.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi na Teknplojia mhe. Profesa
Joyce Ndalichako alisema kuwa anaunga mkono hoja yakuongeza umri wa
kustaafu kutoka miaka 60 kwa lazima hadi 65 na kutoka miaka 55 kwa hiari hadi
miaka 60.
Aliongeza kuwa Serikali inayo mikakati ya makusudi yakuwaendeleza
wataalamu wa kada zenye uhaba wataalamu wabobezi ili kuziba pengo
lililopo.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wake wa 10 kikao
cha 1 limepitisha muswaada wa marekebisho ya sheria mbalimbali nne ambazo ni
Sheria ya Ufilisi, sura ya 25, Sheria ya Bajeti, sura ya 439, Sheria ya Ardhi,
sura ya 113 na Sheria ya Utumishi wa Umma, sura ya 238.
SHARE
No comments:
Post a Comment