Na Hamza Temba - Rufiji, Pwani
Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya
miaka minne baina ya Hifadhi ya Msitu wa Utete na vitongoji vinavyopakana na
hifadhi hiyo vya Siasa, Nyawanje, Kindwitwi na Utunge katika wilaya ya Rufiji mkoani
Pwani.
Dk. Kigwangalla amemaliza
mgogoro huo kwa kumuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania,
Prof. Dos Santos Silayo kuunda timu ya wataalamu watakaoshirikiana na wataalamu
wa mkoa wa Pwani na wilaya ya Rufiji kwa ajili ya kufanya tathmini ya eneo
lenye mgogoro na kuanzisha mchakato wa kisheria wa kurekebisha mipaka ya eneo
hilo na hatimaye kuligawa kwa wananchi.
Dk. Kigwangalla ametoa
agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Utete,
wilaya ya Rufiji mkoani Pwani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua
migogoro baina ya hifadhi na wananchi mkoani humo

Dk Hamis Kigwangalla
“Naagiza Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, uunde timu ya wataalam waje
washirikiane na wataalam wa mkoa na wilaya, wafanye tathmini kwenye lile eneo
ambalo wananchi wamekuwa wakilima kabla hata msitu haujawa ‘gazerted’ (haujatagazwa)
kuwa hifadhi ili muone ni kwa kiasi gani mnaweza mkamega eneo na kulirudisha
kwa wananchi ili waweze kuendelea na kilimo,” aliagiza Dk. Kigwangalla.
Ameagiza pia kamati
hiyo ifanye tathmini ya eneo la chemchem ambalo ni sehemu ya hifadhi hiyo ambalo
limevamiwa kwa kiasi kikubwa na makazi ya wananchi ili waweze kurekebisha
mipaka yake na hatimaye wananchi wabaki na eneo lao la makazi na eneo litakalobakia
liendelee kuhifadhiwa.
“Kamati hiyo pia ije
ifanye tahtmini inawezaje kuhamisha mipaka ya hifadhi ili kupisha zile nyumba ambazo
zimeshajengwa pale kwa sasa na hapo sasa wananchi wawe hawana mgogoro na
hifadhi, waishi kwenye eneo lao na waiache hifadhi upande wa pili, lakini sasa
waishi kwa mujibu wa sheria kuliko ilivyo hivi sasa tunavyowachukulia kama
wavamizi;” alisema Dk. Kigwangalla.
Aidha Dk. Kigwangalla
ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kutafuta eneo mbadala la
msitu ambalo ni mali ya vijiji likabidhiwe kwa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania ili liweze kuhifadhiwa ikiwa ni fidia ya eneo hilo la Hifadhi ya Msitu
wa Utete litakalokabidhiwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na makazi.
Mbali na maagizo hayo Dk.
Kigwangalla ameagiza pia wananchi waliolima kwenye bonde katika Hifadhi hiyo wasiondolewe
katika msimu huu wa kilimo wakati zoezi la uwekaji wa mipaka likiwa linaendelea.
Hifadhi ya Msitu wa
Utete ilianzishwa kwa tangazo la Serikali Na. 1cap 132p 1351 la tarehe 1
Oktoba, 1957 ikiwa na jumla ya ekari 2,346. Desemba 2015 msitu huo ulipimwa tena
na kuchorewa ramani.
Wananchi wanaozunguka
hifadhi hiyo wamedai kuwepo katika baadhi ya maeneo hayo ya hifadhi hata kabla
ya kuanzishwa kwa hifadhi hiyo, hivyo wameiomba Serikali iwamegee maeneo katika
hifadhi hiyo ili waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo na makazi.
SHARE








No comments:
Post a Comment