TRA

TRA

Tuesday, May 2, 2017

Tatizo lenu Serikali mlitanguliza vyeti

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !

Said Mwishehe

JAMANI leo naomba niseme mapema kuwa tatizo la Serikali kwa watumishi wa umma ilitanguliza zaidi vyeti ili kutoa ajira badala ya kuangalia mtu ana nini kichwani.

Hapa ndipo nilipokumbuka barua iliyoandikwa na moja ya walimu kutoka mkoani Tabora miaka saba iliyopita akieleza cheti huwa hakifanyi kazi.

Anayefanya kazi ni mtu na huyo ndiyo wa kutazamwa ana nini kichwani na si kwenye mfuko amebeba lundo la vyeti (vya kughushi? ) kwa kiwango gani.

Nafahamu umuhimu wa elimu katika nchi yetu. Naheshimu mifumo ambayo imewekwa katika eneo la elimu. Ni vema kila anayetaka elimu akafuata mifumo hiyo ili kupata elimu bora.

Sina tatizo na jitihada za serikali katika kusimamia watumishi wake kuwa na sifa za kielimu ambazo zinahitajika kwa kila kiwango cha kitaaluma.

Pamoja na jitihada hizo za Serikali ukweli utabaki pale pale vyeti havifanyi kazi bali anayefanya kazi ni mtu na hapa ndipo ambapo ilipaswa kuwekwa mkazo zaidi ili kumsaidia mtumishi wa umma badala ya kuhangaika na vyeti vyake.

Kwa Ujinga Wangu msingi wa watumishi wa umma kufoji vyeti ni kutokana na Serikali kutanguliza zaidi vyeti katika kutoa ajira badala ya kuangalia uwezo wa mtu.

Mjadala mkubwa ambao upo kwenye nchi yetu kwa sasa ni baada ya watumishi 9,932 kubainika walifoji vyeti vya elimu.

Hivyo hawatakiwi kuendelea kuwa kazini na sheria inaeleza mtumishi ambaye atabainika amefoji vyeti atafungwa miaka saba jela. Nikiri kuondolewa kwa watumishi hao zaidi ya 9,000 kuna faida na hasara yake kwa Serikali.

Natambua faida kubwa kwa Serikali ni kuokoa fedha ambazo zilikuwa zinalipwa kwa watumishi wa umma ambao walipata nafasi ya utumishi wa umma kumbe hawakuwa na sifa.

Pia kuna hasara ambayo naiona kwa Serikali baada ya kuwaondoa watumishi hao. Naamini mbali ya kuwa wamefoji vyeti vyao vya elimu lakini wapo wataalamu wazuri tu na huenda wengine ndiyo walikuwa walimu wa watumishi wenye elimu iliyotimia.

Kwa Ujinga Wangu nimekuwa nikifuatilia aina ya wasomi wetu tena wengine wenye elimu ya juu, wapo vizuri kwenye vyeti vyao lakini kwenye utendaji wa kazi hakuna wanachokifanya.

Pia tunafahamu namna ambavyo elimu yetu inatolewa wapo ambao wanapata alama nzuri si kwa sababu ya kuwa na uwezo kichwani.

Bali anapata alama za juu kwa sababu tu mwalimu ni rafiki yake, mjomba wake, baba yake mdogo na wakati mwingine anapata alama nzuri za somo kwa sababu anayefundisha ni mpenzi wake.

Hivyo anaajiriwa mtu ambaye cheti chake cha elimu ni kizuri lakini uwezo wa kufanya kazi haupo lakini pembeni yake kuna mtu ambaye hana alama nzuri kwenye cheti chake cha elimu au alifoji cheti ila ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi.

Kwa Ujinga Wangu, mfumo wetu wa utoaji ajira ndiyo umesababisha watu kuamua kufoji cheti ili apate kazi. Kwa mfano kijana wa miaka 12 anaanza kuendesha gari nyumbani kwao na kupata uzoefu wa kutosha.

Anapofikisha miaka 20 anakwenda kuomba kazi akiwa na leseni yake ya udereva lakini ili apate kazi anaambiwa awe na cheti cha kidato cha nne.

Kwa kuwa anajua kabisa anajua vizuri udereva anakwenda kufoji cheti ili apate kazi na matokeo yake mwisho wa siku anaingia kwenye mkumbo wa watumishi waliofoji vyeti vya elimu.

Kwa Ujinga Wangu huyu kijana angechukuliwa kwa uwezo wake wa udereva wala asingekuwa na muda wa kwenda kuhonga baraza la mitihani ili apewe cheti cha elimu ambayo hakuwa nayo.

Kwa Ujinga Wangu nilitegemea Serikali ingejikita kwenye kuangalia zaidi uwezo wa mtu kwenye kichwa chake kwenye kufanya jambo fulani kwenye utumishi wa umma.

Pamoja na yote hayo, tuangalie suala la msingi huyu mtu ana nini kichwani kwa sababu anaweza kuja mtu ana vyeti vizuri na jina lake halisi lipo kwenye cheti kama tunavyotaka sasa hivi lakini kichwani hakuna kitu.

Hii ni kwa sababu uzoefu umeonesha mfumo wetu wa elimu umezungukwa na makando kando mengi ambayo hayataweza kufanyiwa kazi ndani ya miaka 10 au 20 tukapata ufumbuzi wake.

Hebu tujiulize wenye matatizo haya ya kufoji vyeti chanzo chake ni nini? Je, hatuoni wapo wataalamu waliosababisha gharika hilo na sasa wanahukumiwa bila wenyewe kuwajibishwa.

Kwa mfano mfanyakazi anapokwenda kuomba ajira anapeleka vyeti kwa ofisa muajiri ambaye anavipitia na kujiridhisha. Hivyo akiona muhusika ana sifa anajibiwa au anapewa ajira.






Sasa hao maofisa ambao wametoa ajira kwa watu ambao wamefoji vyeti wamepewa adhabu gani kwani kinachoonekana walikuwa si makini katika kuchunguza vyeti kabla ya serikali kuingia gharama ya kuanza kulipa mishahara na mafao mengine.

Kwa Ujinga Wangu nadhani mchakato wa uhakiki ungeaanzia kwa maofisa uajiri na si kwa watumishi ambao wameambiwa wasionekane kazini kuanzia Aprili 29, 2017.








 Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma 
  na Utawala Bora, Angella Kairuki

Hii ni kwa sababu wangekuwa makini kujiridhisha kuhusu vyeti kuanzia Baraza la Mitihani na vyuo walivyosoma yote hayo yasingejitokeza na kuleta madhara kama yaliyotokea sasa kwani watumishi hao wamepoteza kazi.

Kwa Ujinga Wangu ninavyoona bado hatujapata suluhu ya tatizo lenyewe na badala yake tunapapasapapasa na kuacha tatizo halisi likiwa palepale. Tujiulize waliotoa vyeti hivyo kwa watumishi hao si wapo?

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger