TRA

TRA

Sunday, February 11, 2018

Elimu ya kisukari kwa watoto ni njia bora kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


Mwandishi Wetu, TJNCDF


WATU wengi huamini kuwa ugonjwa wa kisukari huwapata watu wenye umri zaidi ya miaka 30 na ndiyo maana jamii nyingi hazioni umuhimu wa kuwachunguza watoto iwapo wameathirika.


Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) kinaonya kwamba hiyo ni imani potofu kwa sababu inawezekana watoto wengi walio na kisukari wasigundulike na kupoteza maisha na pia ni nafasi nzuri ya kuelimisha uma kuhusu ugonjwa huu.


hivyo jamii inapaswa kubadilika kwa kuwa uchunguzi kwa watoto juu ya ugonjwa huo n I muhimu kwa maendeleo endelevu kimaisha.




Ili kuondoa mawazo hayo potofu, TDA iliendesha mpango maalumu wa kupima kisukari na kuelimisha wanafunzi juu ya umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi pamoja na kuwa na uelewa juu ya ugonjwa huo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza ambayo yanatokana na mitindo mibaya ya kimaisha.

Elimu hiyo ilitolewa katika shule za sekondari za wasichana za Kisutu na Jangwani ikiwa ni sehemu ya TDA kuelimisha umma katika program zake kuelekea Siku ya Ugonjwa wa Kisukari Dunini, ambayo huadhimishwa kila mwaka Novemba 14.
Mratibu wa Shirikisho la Vyama Vinavyopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA) mkoa wa Dar es Salaam, Happy Nchimbi anasema kuwa huu ni mkakati wa kuelimisha jamiin ili iwe na uelewa wa kutosha juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, hususani kisukari.


“Kasi ya watu kuugua magonjwa yasiyo ya kuambukiza imeongezeka kwa kiwango kikubwa katika miaka ya karibuni na hali inaonyesha kuwa kwa sasa yanasababisha vifo vingi kuliko magonjwa ya kuambukiza,” anasema Nchimbi.

Mbali na kisukari, anayataja baadhi ya magonjwa mengine  yasiyo ya kuambukiza kuwa ni shinikizo la damu, maradhi ya moyo, selimundu, kiharusi, pumu na matatizo ya kinywa.

Mbali na upimaji huo, Nchimbi alisema wataelimishwa juu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kubadili tabia za ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari na wanga kwa wingi.

“Pia watafundishwa juu ya utaratibu mzuri wa kufanya mazoezi na kuhakikisha uzito wao unawiana na urefu wao kulingana na ushauri wa kitaalamu,” alisema Nchimbi.

Meneja Mradi wa Ugonjwa wa Kisukari kwa Watoto, Hariet Mganga anasema tatizo la kisukari kwa watoto hapa nchini kwa sasa ni kubwa na linahitaji mikakati ya kudumu ili kukabiliana nalo.

Anatoa mfano kuwa katika kliniki za kisukari 34 walizozisajili Tanzania nzima wanahudumia watoto 2488 wenye ugonjwa wa kisukari.

Anasema mtoto akigundulika mapema inakuwa rahisi kuudhibiti ugonjwa huo na akawa anaishi vizuri hadi kufikia malengo yake ya kimaisha.

Hata hivyo, anasema wWagonjwa wa kisukari wanaweza kuishi maisha marefu iwapo watafuata vyema kanuni za afya za kukabili ugonjwa huo.

Nini maana ya kisukari kwa watoto?

Kwa kawaida ugonjwa wa kisukari umegawanyika katika makundi mawili; aina ya kwanza na y a pili. Aina ya kwanza inafahamika kama ugonjwa wa kisukari cha utotoni na aina ya pili ni ya ukubwani.

Kabla ya kufafanua aina hizo za kisukari ni vyema ukafahamu ni nini maana ya jumla ugonjwa wa kusikari. Mwenyekiti wa TDA, Profesa Andrew Swai anasema kwa ufupi kuwa kisukari ni ongezeko kubwa na la muda mrefu la kiwango cha sukari aina ya glukosi ndani ya damu.

Anasema kKwa kawaida homoni ya insulini inayozalishwa na kongosho hudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. ili kiwe katika uwiano mzuri kwenye mfumo wa damu.

Anafafanua kwamba iIkitokea insulini haizalishwi au inazalishwa  kidogo au ubora wake ni duni, ndipo tatizo la kisukari hujitokeza.
Kimsingi kisukari cha utotoni kinatokana na insulini kutozalishwa kabisa au kwa inazalishwa kiasi kisichotoshalakini haina ubora unaotazamiwa. Mara nyingi hutokana na kuugua kwa kongosho kutokana na kongosho kushambuliwa na kinga ya mwili kama vile ni kitu kigeni mwilini, kwa sababu ambazo bado hazieleweki. Kongosho haliponi na mtoto huwa tegemezi wa insulini kutoka nje ya mwili maisha yake yote.
Watu wengi hupatwa na ugojwa huu wakiwa na umri chini ya miaka thelathini. Mari nyingi katika kipindi kifupi, mtoto huwa na hali mbaya ya kukojoa mara kwa mara, kiu na njaa nyingi, na Ugonjwa huu mto huzaliwa nao. Kisukari cha aina hii mara nyingi hatimaye husababisha mgonjwa kukonda na kudhoofika. Hali hiyo humfanya mtoto awe tegemezi wa insulini nje ya mwili maisha yake yote.
Kisukari cha ukubwani kwa kawaida hujitokeza kuanzia umri wa miaka 30.  na kuendelea baada ya kutokea athari kwenye mfumo wa udhibiti wa sukari mwilini.

MMiongoni mwa sababu zinazochangia kutokea kwa ugonjwa huu ni urithi wa vinasaba vyenye mwelekeo wa ugonjwa pamoja na lishe isiyofaa, duni. Kula sana na kunenepeana sana au kuwa na uzito kupita kiasi na kutoushughulisha mwili.

 Kutokufanya mazoezi au kazi ngumu kunaelezewwa na wataalamu kuwa husababisha takribani asilimia 55 ya wagonjwa wa kisukari cha aina ya pili au kisukari cha ukubwani.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa chanzo kingine cha tatizo hili ni hali ya ujauzito. Kisukari cha ujauzito hutokea kwa asilimia nne ya wajawazito. Hata hivyo aina hii ya kisukari hutoweka baada ya mama kujifungua.

Tatizo jingine linalohusishwa na kutokea kwa kisukari ni hali ya uzee.  Takwimu kadhaa zinaonyesha kuwa asilimia 20 ya wazee katika Amerika ya Kaskazini wana kisukari, na kote duniani ugonjwa huu huongezeka kadiri umri unavyoongezeka. hali ambayo inahusishwa na kubweteka, Vitu vinavyochangia hali hii ni kutokufanya mazoezi wakati wa uzee nau kuzeeka kwa kongosho. Hata hivyo ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi husababisha sukari kuu juu kwenye damu na hali hii ikiendelea kwa muda mrefu huathiri kongosho kwa kulifanya lifanye kazi ya ziada kuishusha sukari. Hili linaweza kilifanya kongosho lizeeke mapema na kisukari kutokea.

Kwa mujibu wa ripoti ya IDF ya Julai 2003, tatizo jingine linalohusishwa na vyanzo vya ugonjwa wa kisukari ni matumizi makubwa ya tumbaku na pombe.
Dalili kubwa za ugonjwa huu ni pamoja na kukojoa sana, kupata kiu na kunywa maji mara kwa mara, kuhisi njaa mara kwa mara na kula sana.

Dalili nyzingine ni kuchoka, kutokwa jasho jingi, kupungua uzito wa mwili, kupata hisia za ganzi na kuungua miguuni au mikononi. Kwa wanawake, kisukari kinaweza kusababisha muwasho sehemu za siri.

Lakini ni muhimu kukumbuka kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba asilimia 25 hadi 50 ya wagonjwa wa kisukari hawaonyeshi dalili na hugunduliwa kwa bahati kupitia vipimo vya maabara wakati wa uchunguzi wa kawaida wa afya zao kwa matatizo mengine.
Profesa Swai anasema kisukari kisipodhibitiwa mapema kinaweza kusababisha athari mbalimbali kama vile upofu, , uoni hafifu, upungufu wa hamu na nguvu za tendo la ndoa, figo kushindwa kufanya kazi zake vizuri na ugonjwa wa moyo.

Madhara mengine, anasema ni shinikizo la damu, kiharusi, kutokea kwa vidonda visivyopona mapema na matatizo ya mishipa ya fahamu na hisia. Miguu inaweza kuathirika kwa sababu ya kuharibika kwa mishipa ya damu na ya fahamu na kusababisha vidonda na hata miguu kuoza na kuhitaji kukatwa.
Vile vile kisukari husababisha kupungua kwa kinga ya mwili na hivyo ikawa ni rahisi mgonjwa kupata maambukizi kadhaa yakiwemo ya kifuu kikuu, ngozi, njia ya mkojo na ukeni.

Mbali na matibabu ya hospitalini, wagonjwa wa kisukari hushauriwa kuudhibiti ugonjwa huo kwa kubadili mtindo wa maisha na kupangilia vizuri matumizi ya vyakula kila siku.

Miongoni mwa mambo wanayoshauriwa ni kupunguza ulaji wa vyakula vyenye wingi wa wanga na kula kwa wingi matunda na mboga mboga, kupunguza au kuacha kutumia vyakula au vinywaji vilivyoongezwa sukari, kutumia sukari au mafuta kwa kiasi kidogo hasa yale yatokanayo na wanyama, kula nafaka bila kukoboa, kupunguza au kuacha kabisa pombe, kushughulisha mwili angalau kwa dakika 30 kwa siku na kula kwa kiasi bila kunenepa.
mengi; hasa yanayotokana na wanyama.

Maelezo hayo ya wataalamu yanaonyesha wazi kwamba jamii ikielimishwa juu ya ugonjwa wa kisukari kuanzia utotoni ni njia bora zaidi ya kujenga kizazi chenye uelewa wa kutosha wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Hali hiyo pia inaweza kuwafanya wengi wasipate magonjwa haya kwa kubadili mitindo ya namna wanavyoishi kwa kuepuka ulaji wa vyakula hatarishi, kuepuka uene na kushughulisha mwili.
 

Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA). Maoni au ushauri tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam au tjncdf@gmail.com

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger