Mwandishi Wetu, TJNCDF
SEHEMU kubwa ya milo anayokula binadamu
huwekwa chumvi ili kuleta ladha nzuri ya kumvutia mlaji. Chumvi inahitajika
mwilini lakini wataalamu wa afya wanasema watu wengi wanaugua na kufa kutokana
na kiungo hicho.
Je, kiungo hicho kina athari gani?
Kinapaswa kutumika namna gani? Madhara gani kinasababisha? Je, kama imekuathiri
ufanyeje?
Daktari wa Magonjwa ya Binadamu, Shita
Samwel anasema chumvi ni muhimu sana kwa mwili wa mwanadamu kwakua huwa na
kiambata kiitwacho sodium ambacho ni muhimu kwa kazi za kimwili.
Kupima shinikizo la damu
“Chumvi ina sodiamu ambayo in muhimu mwilini. Hutumika kupitisha fahamu kwenye
mfumo wa fahamu, ukunjikaji au kujivuta kwa misuli na udhibiti wa kiwango
sahihi cha maji mwilini,” anasema Dk. Samwel.
Anasema chumvi ina tabia ya kuvuta maji
kwenda mahali ilipo hivyo mwili hutumia sodium kwa ajili ya kudhibiti wingi wa
maji katika damu na tishu za mwilini.
Pale chumvi inapozidi, anasema figo huwa na
kazi ya kuitoa kwa njia ya mkojo lakini inapotumika kwa kiwango kikubwa
hushindwa kuitoa yote hivyo huendelea kubaki mwilini na ndipo matatizo
mbalimbali hujitokeza.
Dk Samwel anasema miongoni mwa matatizo
yanayosababishwa na chumvi nyingi ni shinikizo la damu, kiharusi, moyo kuwa
mkubwa, valvu za moyo kuathirika na kifo.
Kuhusu shinikizo la damu, Dk Shita anasema
msukumo wa damu mwilini hutegemea uwapo wa chumvi lakini inapokuwa imezidi
msukumo wa damu nao unakuwa juu na hali inakuwa ya hatari pale mhusika
anapokuwa ana shinikizo la damu au matatizo ya moyo.
“Ukila kiasi kikubwa cha chumvi zaidi ya
uwezo wa figo zako kuhimili chumvi iliyozidi hubaki mwilini, kutokana na tabia
ya sodium kuvuta maji na kuzidisha kiwango cha maji kinachotakiwa kwenye
damu. Hali hiyo itasababisha ujazo
wa damu kuongezeka hivyo shinikizo la damu kuwa juu,” anafafanua.
Hali ya msukumo mkubwa wa damu huweza
kuleta madhara mengi ndiyo maana wataalamu wa afya hushauri watu wenye shinikizo
la damu kupunguza shumvi kwenye vyakula hasa ya kuongeza mezani.
Anasema kwa bahati mbaya watu wengi hawajui
kama wana shinikizo la damu au matatizo ya moyo hadi pale wanapochunguzwa
hospitalini wanapoenda kutibiwa mambo mengine.
Magonjwa
ya moyo na kiharusi anasema, ingawa yanaweza kusababishwa na mambo mengine
lakini chumvu inaweza kuzidisha matatizo hayo.
Athari
za magonjwa haya ya moyo na kiharusi anasema zinazidi iwapo mgonjwa atatumia
chumi kwa sababu chumvi husababisha msukumo wa damu kuongezeka na mishipa ya
damu kushindwa kutanuka.
Hali
hii anasema inaweza kusababisha mafuta kurundikana kwenye mishipa ya damu na
kuifanya mishipa hiyo kuwa migumu, kwa kitaalamu “atherosclerosis”.
Katika
mazingira haya anasema mishipa ya ateri huweza kuharibika na kuwa myembamba au
kusinyaa na kuta za zake kukakamaa.
Mazingira
hayo anayaelezea kuwa huufanya moyo kuwa na kazi ngumu ya kusukuma damu hivyo
kuuweka mwili katika hatari yakupata shambulizi la moyo la ghafla, moyo
kushindwa kufanya kazi na kiharusi.
Tafiti
za Chuo cha Afya ya Jamii cha Havard zinaonyesha ya kuwa utumiaji chumvi kupita
kiasi unaongeza asilimia 23 ya
kupata kiharusi na asilimia 14 kupata magonjwa ya moyo.
Matatizo
mengine ni kama vile moyo kuwa mkubwa na kuathiri valve zake, kwani uwepo wa
ujazo mkubwa katika mzunguko wa damu hulazimu moyo kufanya kazi ya ziada ili
kuleta mzunguko sahihi unaotakiwa na mwili. Kadiri muda unavyosonga na uwepo wa
hali hii moyo kuongezeka ukubwa na valve za moyo huwa nyembamba. Hali hii
huleta dalili kama vile maumivu ya kifua, kushindwa kupumua na kuwa na mchoko
sugu. Pia kifo cha ghafla na moyo kushindwa kufanya kazi huweza kutokea.
Pia
chumvi husababisha magonjwa mengine kama ya figo, mwili kuvimba, tindi kali
kuwa nyingi tumboni na udhaifu wa mifupa.
Matumizi
sahihi ya chumvi
Moja
ya nyenzo kuu zakupambana na tatizo hili, Dk. Samwel anasema ni kubadili
mienendo na mifumo ya kimaisha kwa kuepuka ulaji wa vyakula vyenye chumvi
nyingi au kuongeza chumvi kinapopelekwa mezani.
Sawia
na upunguzaji wa chumvi mtaalamu huyo wa afya anashauri kupunguza matumizi ya
viwango vikubwa vya vyakula vya wanga, mafuta na sukari.
Anasema
vyakula vingi vinavyotumika hasa maeneo ya mijini ni vya kukaanga kwa mafuta
kama vile mandazi, chapatti, mihogo, viazi, chipsi, kuku, ndizi, mayai na nyama
za kukausha.
Dk
Samwel anasema vyakula hivyo ni chanzo cha matatizo mengi ya kiafya kwa
binadamu hasa magonjwa yasio ya kuambukiza kama vile shinikizo la damu,
kiharusi, matatizo ya moyo, kisukari na athari za viungo kama vile figo.
Mambo ambayo mtu akijihisi anayo anapaswa
kuenda hospitali kwa uchunguzi zaidi ni upumuaji wa shida, kuhisi mapigo ya
moyo yasiyo ya kawaida, maumivi ya kifua, ganzi, maumivu ya kichwa, pumzi
kukata na kuchoka ghafla wakati ukitembea.
Je, ni kiasi gani unatakiwa kula chumvi kwa
mlo? Dk. Samwel anasema chumvi isizidi 500mg kwa kila mlo mmoja. Upimaji
unaotumika anasema ni ule wa kufinya kwa kidole cha shahada na gumba.
Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa
Habari Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa
kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA).
Maoni au ushauri tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam au tjncdf@gmail.com
SHARE
No comments:
Post a Comment