Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro ametoa onyo akisema wamejiweka tayari kukabiliana na watu, wakiwemo wanasiasa wanaohamasishana kuandamana nchi nzima kinyume cha sheria.
Sirro alisema hayo jana mjini Bariadi baada ya kukutana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Simiyu alikokuwa ziarani kukagua utayari wa askari wa jeshi hilo.
“Kuna makundi ya vijana wanaojiita wana mapinduzi wanahamasishana na kupanga kuandamana nchi nzima wakiratibiwa na chama kimoja cha siasa, tumejipanga kuwadhibiti na tutawakamata wote bila kujali vyeo na madaraka yao,” alisema.
Sirro aliwataka wazazi na walezi kuwaonya na kuwazuia vijana wao kushiriki maandamano yasiyo na kibali kwa sababu hakuna atakayevunja sheria atakayesalimika bila kuchukuliwa hatua stahiki.
“Kuvunja sheria ni jambo rahisi lakini madhara yake ni makubwa. Wananchi wasijiingize kwenye mambo yakiwemo uhalifu ambayo mwishowe huwagharimu,” alisema.
SHARE
No comments:
Post a Comment