
Naibu waziri wa ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi Angelina mabula akizungumza mara baada ya kukagua
mradi wa nyumba za shirika la nyumba la taifa (NHC) wakati wa ziara yake
mkoa wa Mara.
……………….
Na Mwandishi Maalum- Mara
Naibu waziri wa ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi Angelina mabula amezishauri halmashauri za mji na
wilaya ya Musoma mkoa wa Mara kununua nyumba zilizojengwa na shirika la
nyumba la taifa (NHC) kwa ajili ya watumishi wake.
Mabula ametoa ushauri huo
alipotembelea nyumba hamsini zilizojengwa na shirika la nyumba la taifa
(NHC) katika eneo la Buhare katika manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Amesema, ni jukumu la serikali
kuhakikisha watumishi wake wanakuwa na makazi bora na rahisi kwao hasa
pale mtumishi anapohitajika kwa haraka katika kutekeleza majukumu yake.
Naibu waziri wa ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi alisema, alitegemea halmashauri za Musoma
zingezichukua nyumba hizo zilizojengwa na shirika la nyumba kama ambavyo
imefanyika katika maeneo mengine ya Geita na Uyui.
Amezitaka halmashauri za mji na
wilaya ya Musoma kulitumia shirika la nyumba la Taifa (NHC) katika
kujenga nyumba zake pamoja na kupanga katika nyumba za shirika hilo.
Aidha, alizitaka halmashauri
kuhakikisha zinapeleka huduma muhimu kama maji na miundo mbinu katika
maeneo ambayo shirika la nyumba la taifa linaendesha miradi yake ili
kupunguza gharama za ujenzi na hivyo kuleta unafuu wakati wa kuuza
nyumba na kupanga.
Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi ameshauri pia nyumba za shirika hilo ambazo
serikali imeshindwa kuzinunua zitangazwe kwa wananchi ili wale wenye
uwezo waweze kuzinunua kwani ni nyumba bora na za kisasa.
Naye Meneja wa Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) Frank Mambo, amemueleza Naibu Waziri wa ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba 50 wenye lengo la
kuwapatia wananchi makazi bora ulianza mwaka 2014 na unatarajia
kukamilika Machi 2018. Amesema mradi huo unahusisha nyumba za makazi,
maduka, zahanati na maeneo ya kupumzikia.
SHARE
No comments:
Post a Comment