Julian Msacky
OKTOBA 15, mwaka huu nilikuwa nazungumza na Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashir Ali kuhusu umuhimu wa watu kupenda
kusoma vitabu.
Wakati tukiwa katika mazungumzo yaliyotokana na makala
yake aliyoandika kuhusu Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Dk. Ali alifunga mjadala
wa mazungumzo kwa kusema maneno yafuatayo:
"Ahsante. Tusichoke kupiga kelele kwani kazi ya
kujenga taifa haiwezi kukamilika ikiwa tutashindwa kujenga utamaduni wa kupenda
kusoma vitabu na magazeti yenye maarifa na
taarifa kuhusu mapambano ya ukombozi wa taifa letu
na watu wake"
Ni ukweli usiofichika kuwa kama tunataka kujenga
taifa la watu wenye uelewa mpana (wide scope) wa mambo ni lazima tuhimize
watoto wetu kusoma vitabu.
Lakini pia, kazi hiyo haitafanikiwa vizuri kama sisi
wenyewe (wazazi na walimu) hatutakuwa na utamaduni huo.
Ili kufanikisha hilo nilimshauri Dk Ali tuanzishe
Kampeni ya Reading Books Everywhere.
Hii ikiwa na maana kila tutakapokuwa tuwe na kitabu
cha kujifunza jambo lolote ili kushibisha ubongo wetu maarifa ambayo yatakuwa
mtaji mzuri kwa taifa letu.
Unapojenga taifa la watu wanaosoma vitabu maana yake
hata shughuli wanazofanya zitakuwa na mabadiliko makubwa. Watazifanya kitaalamu
zaidi.
Na hili la mwisho ni changamoto kubwa inayotukabili
kama taifa. Mambo yetu mengi hayafanikiwi kwa sababu hatupendi kusoma vitabu.
Matokeo yake vichwa vyetu tunajaza mambo ya ovyo
ovyo ambayo hayatusaidii. Kwa maana hiyo tukianzisha kampeni hiyo ni imani yangu
taifa letu litabadilika katika mambo mengi.
Tutajenga mijadala yenye afya tunapojadili masuala
muhimu yanayogusa ustawi wa nchi na watu wake. Si hivyo tu.
Hata mikataba tutakayoingia kati ya nchi wahisani
itafanyika kwa uangalifu mkubwa tofauti na sasa kwa sababu bongo zetu zitafanya
kazi vizuri.
Kampeni hiyo ni lazima iende pamoja na kuhakikisha
shule zetu zina vitabu vya kutosha. Si bora vitabu tu, bali vikidhi viwango vya
kutumiwa katika shule zetu.
Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha vitabu vyetu haviwachanganyi
watoto au kuwaondoa kwenye reli.
Wote tunafahamu kuwa kabla ya Jumuia ya Afrika
Mashariki (EAC) haijavunjika mwaka 1977, Tanzania, Uganda na Kenya walikuwa
wanatumia vitabu vya aina moja.
Kulikuwa na vitabu vinafahamika kama East Africa Book
One, Two, Three, Four, Five na Six. Vilikuwa vya kumjenga mwanafunzi kufahamu
kwa usahihi Lugha ya Kiingereza.
Ni ukweli usiofichika kuwa watu wengi waliosoma
vitabu hivyo miaka hiyo wanazungumza vizuri Kiingereza bila tatizo lolote
pamoja na Kiswahili.
Kwa kusema hivi sina maana kuwa Kiswahili tukiweke
pembeni hapana.
Hapa nina lengo la kuhakikisha tunasoma vitabu vya
aina mbalimbali ili vitusaidie kupanua wigo wetu kama Watanzania kwa ustawi wa
mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa kufanya hivyo maana yake mfugaji atasoma kitabu
kinachohusu masuala ya ufugaji.
Akifanya hivyo kitamsaidia kufuga kisasa na kuachana
na mfumo wa kienyeji ambao unasababisha hasara kubwa kuliko faida.
Hii ina maana kuwa si lazima kuwa na mifugo mingi
ndipo uwe tajiri. Unaweza kuwa na ng'ombe 20 na ukafugaji kitaalamu na kupata
faida lukuki na kuepuka uharibifu wa mazingira.
Ufugaji wa aina hiyo unamsaidia mfugaji kuacha
kutangatanga na mifugo.Tunapofuga kitaalamu kuna faida nyingi.
Kwanza tunakuwa tumejiajiri, lakini pia tunakuwa na kipato cha uhakika kwa ajili ya familia
zetu. Mfumo huo wa ufugaji unakwenda sanjari na kulima kitaalamu.
Ilivyo sasa tunalima kwa mazao ili mradi siku
ziende. Kwa maana hiyo usomaji wa vitabu utatusaidia mambo mengi. Ndiyo maana
ninasisitiza kampeni hiyo.
Kwa kufanya hivyo maana yake tutakuwa na uelewa
mzuri hata wa chimbuko la dini zetu (Ukristo na Uislamu) na namna gani
tuziendeshe katika jamii yetu.
Jamii isiyo na maarifa ni sawa na jamii iliyo
gizani. Tunataka tuondoke kwenye giza hilo kwa kusoma vitabu.
Tukisoma vitabu kwa kina ikiwa ni pamoja na kupitia
katiba za mataifa mengine jamii itakuwa na upeo mpana kuandaa katiba inayokidhi
kiu ya wengi.
Hata tunapokataa katiba hii na ile tutakuwa na hoja
za kutosheleza badala ya kudandia hoja za wengine. Faida za kusoma vitabu ni
nyingi.
Wakati ninaandika makala haya nilipofungua intaneti
nilikutana na jambo linahusu mada hii ya kusoma vitabu. Nilikutana na watu
waliosoma vitabu vingi kwa mwaka huu.
Wengine wamesoma vitabu 25. Miongoni mwa vitabu
ambavyo Watanzania wenzetu wamefanikiwa kusoma ni pamoja na
The truth shall make you free- Gustavo Gutiérrez.
Kwa maana Ukweli Utawaweka Huru. Sowing the mastard
seed cha Yoweri Museven, The 21 Irrefutable Laws of Leadership cha John C.
Maxwell, Hisa, Akiba na Uwekezaji cha Emilian Busara, YES, In My Life Time cha
Profesa Haroub Othman na vingine vingi.
Kuna umuhimu wa kubadilika na kuanza kusoma vitabu
ambavyo ni nyenzo muhimu kwa kizazi hiki hasa tunapozungumzia dhana ya sayansi
na teknolojia.
Tusikubali kuwa maskini wa fikra. Tutafute mitaji
kwa kusoma vitabu. Tuwaige wenzetu wa dunia ya kwanza ambao wakiwa wanasafiri
wanatembea na vitabu.
Badala ya kupotezea fikra zetu zote kwenye Facebook,
Instram, Twitter, WhatSap na mitandao mingine ya kijamii, tuvikumbuke pia
vitabu ambavyo vina maarifa lukuki.
Mitandao hiyo inatudumaza kifikra na kiakili. Hebu
tubadilike kwa sababu hata waasisi (founders) wa hiyo mitandao hawaipi nafasi
kwa kiwango hicho.
Kama kweli walikuwa wanaipa nafasi, wasingesafiri na
vitabu wanapokuwa safarini.
Wasomi na waandishi wa habari wawe mstari wa mbele
kupigania kampeni hiyo ili kujenga taifa la watu wanaopenda kusoma vitabu.
Kwa kufanya hivyo ile dhana kwamba ukitaka kumficha
Mtanzania jambo liweke kwenye maandishi, litakwisha kwa vile wanasoma vitabu
ambavyo vina hazina ya mambo mengi mazuri.
msackyj@yahoo.co.uk,
0718981221
SHARE
No comments:
Post a Comment