Washirika
wa kisiasa wa Kansela Angela Merkel - chama cha Christian Social Union
CSU, wameongeza shinikizo kwake akaze sheria za uhamiaji na ukimbizi kwa
kutaka kipaumbele wapewe wahamiaji Wakristo.
Chama
hicho cha CSU pia kimetaka kupigwa marufuku kwa vazi la Kiislamu
linalofunika sehemu au uso mzima la Burqa, kukomesha mfumo wa uraia wa
nchi mbili, kuweka sheria kali zinazowataka wageni kujumuika katika
jamii na kujifunza Kijerumani na vile vile kuweka kiwango cha mwisho cha
waomba hifadhi wanaoweza kukubaliwa kuwa laki mbili kwa mwaka.
Chama
hicho ambacho mara kwa mara kumeshambulia msimamo laini wa Merkel kuhusu
wakimbizi, ambao ulipekelea kupokelewa kwa wakimbizi milioni moja
katika taifa hilo kubw azaidi kiuchumi katika Umoja wa Ulaya mwaka
uliyopita -- kinapanga kuwasilisha waraka huo katika mkutano unaofanyika
siku ya Ijumaa.
Hatutaki Waislamu!
Hatua
hiyo inakuja siku chache baada ya chama cha mrengo mkali wa kulia
kinachopinga uhamiaji na Uislamu cha Alternative für Deutschland - au
Chama Mbadala cha Ujerumani - AfD kukishinda chama cha Merkel cha
Christian Democratic Union CDU, katika uchaguzi wa jimbo, na ukiwa
umesailia karibu mwaka mmoja kabla ya Ujerumani kufanya uchaguzi mkuu.
Merkel,
ambaye umaarufu wake wa muda mrefu umeshuka kufuatia mgogoro wa
wakimbizi, siku ya Jumatano alivionya vyama vya siasa dhidi ya
kujishusha hadhi kwa kuchukuwa msimamo wa chama cha AfD wa kueneza chuki
dhidi ya Uislamu.
Lakini
washirika wake wa CSU, chenye makao yake katika jimbo la kusini lenye
wahafidhina wengi wa kikatoliki la Bavaria, wameendelea na ukosoaji wao
katika waraka huo wa kurasa tano.
"Tunasema
wazi kabisaa kwamba wahamiaji wanaotufaa ni wale wenye utamaduni sawa
na wa kwetu wa Kikristo na maadili ya Kimagharibi. Tunapata shida kuona
idadi kubwa ya watu wa imani na maadili tofauti wakija Ulaya na
Ujerumani, na tunajua hisia za watu kuhusiana na suala hilo," alisema
katibu mkuu wa CSU Andreas Scheuer, na kuongeza kuwa "laazima Ujerumani
ibakie kuwa Ujerumani."
Mbunge CDU aishambulia CSU
Mbunge
mwandamizi kutoka chama cha CDU Michael Fuchs amekosoa msimamo huo wa
chama cha CSU akisema katika mahojiano ya televisheni, kuwa kila mtu ana
haki ya kuja Ujerumani wakiwa wakimbizi wa kweli na iwapo wanatokea
katika maeneo hatari, bila kujali iwapo mtu anatokea Aleppo nchini
Syria, awe wa madhehebu ya Yazidi, Muislamu au Mkristo.
Wakati
huo uhalifu dhidi ya wageni -- yakiwemo mashambulizi, matamshi ya chuki
mtandaoni na mashambulizi ya moto dhidi ya makaazi ya wakimbizi
umeripotiwa kuongezeka nchini Ujerumani. Mwenyekiti wa baraza kuu la
Waislamu la Ujerumani Aiman Mazyek, alisema idadi ya mashambulizi ya
kimwili na kimaneno dhidi ya Waislamu imeongezeka katika namna isiyo
kifani.DW
SHARE
No comments:
Post a Comment