WATU
sita wamekufa na mmoja kujeruhiwa katika matukio mawili tofauti
yaliyotokea mkoani Rukwa likiwemo la mkazi wa Kijiji cha Ilonga, Kata ya
Mambwe Nkoswe wilayani Kalambo, David Sakanyanya (26) aliyemuua bibi
yake, Sikilieli Nampunje (55) kwa kumpiga risasi wakigombea mashamba ya
urithi kwa zaidi ya miaka mitatu.Aidha, wavuvi watano wamekufa maji na
mmoja kujeruhiwa baada ya mtumbwi kupinduka wakati wakivua samaki katika
Ziwa Rukwa lililoko katika Wilaya ya Sumbawanga. Kaimu Kamanda wa
Polisi wa Mkoa, Polycarp Urio alithibitisha kutokea kwa matukio hayo
mawili, akieleza kuwa mtumbwi uliokuwa ukitumiwa na wavuvi hao sita
ulipinduka baada ya kukumbwa na dhoruba na kusababisha mtumbwi huo
kuzama.
Urio
aliwataja marehemu hao kuwa ni Paschal Kizepa (30), mkazi wa kijiji cha
Santauki, Peter William (45) wa kijiji cha Mtowisa, Edward Emily (40)
wa kijiji cha Kalakala, Frank Kadima (36) wa Uzia na Saliboko Damas (28)
mkazi wa kijiji cha Lwanji, vyote viko katika Bonde la Ziwa Rukwa
wilayani Sumbawanga.
Mvuvi
aliyejeruhiwa ametambuliwa kuwa ni Florence Mpomwa (27), mkazi wa
kijiji cha Kipa na miili ya marehemu imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa
ajili ya maziko. Kuhusu mkasa wa mjukuu kumuua bibi yake kwa kumpiga
risasi, alisema mauaji hayo yalifanyika juzi wakati Nampunje alipokwenda
kumshtaki mjukuu wake, David Sakanyanya (26) kwa uongozi wa kata akidai
kuwa ameporwa mashamba yake na mjukuu wake huyo.
Mume
wa marehemu, Abbas Kapunda alisema mkewe aliuawa kwa kupigwa risasi na
mjukuu huyo akiwa njiani kwenda nyumbani akitokea shambani. “Ghafla
tulisikia mlio kwa bunduki ulioambatana na mayowe ya kuomba msaada ndipo
tulikimbia hadi kwenye eneo la tukio … nilishuhudia mke wangu Sikilieli
akiwa anagaagaa chini huku akivuja damu kwa wingi.
Mashuhuda
walitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ulioutaarifu uongozi wa kata nao
ukaitaarifu polisi, askari polisi walifika eneo hilo la tukio muda mfupi
tu …. mke wangu alikimbizwa katika Zahanati ya Kalembe, lakini
alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu,” alidai Kapunda.
Naye
Moses Alfred ambaye ni mmoja wa ndugu wa marehemu, alidai chanzo cha
kifo cha ndugu yao (Sikilieli) kuwa na mgogoro wa mashamba kati yao.
Alisisitiza kuwa, wakati wa uhai wake Sikilieli alikuwa akifuatilia haki
yake ya mashamba aliyoachiwa na baba yake mzazi ambaye kabla ya
kufariki dunia (baba huyo), aligawa mashamba kwa watoto wake, lakini
wengine hawakuridhika ambapo walimnyang’anya kwa madai kuwa hana uwezo
wa kumiliki mashamba hayo.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Ilonga, Peter Munga alisema familia hiyo imekuwa na
mgogoro huo kwa takribani miaka mitatu; huku Kaimu Kamanda Urio akieleza
kuwa mtuhumiwa ameshakamatwa na anaendelea kuhojiwa.
IMEANDIKWA NA PETY SIYAME- habarileo SUMBAWANGA
SHARE
No comments:
Post a Comment