Mwenyekiti wa kamati
ya Usajili Zacharia Hans Poppe, mmoja wa wanachama na viongozi maarufu
wa Klabu ya Simba, ameamua kuachia ngazi kwenye kamati ya utendaji.
Uamuzi wake wa kuondoka kamati ya utendaji, moja kwa moja unamuondoa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa kamati ya usajili.
Hans Poppe amesema
kuwa, ameondoka baada ya jopo lililoongozwa na Rais wa Simba, Evans
Aveva kuingia mkataba na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportsPesa
ambao wamesaini mkataba wa Sh bilioni 4.9 kwa miaka mitano.
Akizungumza katika
mahojiano maalum , Hans Poppe amesisitiza, ameamua kukaa pembeni na huyu
ndiye amekuwa injini ya usajili katika kikosi cha Simba akipambana na
Mahasimu wao wakubwa nchini Yanga
“Nitabaki kama
mwanachama wa kawaida wa Simba. Nitaendelea na shughuli zangu nyingine,”
alisema na alipoulizwa sababu za kujiuzulu alisema.
“Mambo yamekwenda
kwa uficho, mkataba umekuwa ukifichwa. Kamati ya utendaji imetaarifiwa
siku moja kabla ya kusainiwa. Ilikuwa Alhamisi, Ijumaa wamesaini, nini
kinafichwa.
“Mimi nakaa pembeni,
nimeshaandika na barua. Sitaki kuwa sehemu ya watu wasio waungwana.
Angalia hata Mo Dewji hakuwa akijua, lakini huyu mtu mwaka mzima ndiye
katukopesha mishahara.
“Dewji alisema,
mkitaka kusaini mkataba kama mmepata mdhamini mniambie. Maana na yeye
tulimpa jukumu la kutafuta mdhamini, hata mimi nilipewa jukumu hilo
lakini leo unasikia wenzako wameingia mkataba na mdhamini mpya.
“Kabla tumekuwa tukishirikiana kwa kila jambo, kwenye shida na raha. Vipi leo, nini kimefanya tusiwe pamoja?
“Kawaida walitakiwa
waje na mkataba, tuujadili na kuangalia vipengele. Kama kuna sehemu
zikarekebishwe au kuongezwa vifanyiwe kazi, mwisho wakija tuseme hapa
sawa, basi usainiwe. Nani atakataa mdhamini kama unaona ana faida na
klabu?” alihoji Hans Poppe.
SHARE
No comments:
Post a Comment