WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amenunua hisa za kampuni ya Vodacom
Tanzania Plc zenye thamani ya sh. milioni 10 pamoja na nyingine za sh. milioni
10 kwa ajili ya mke wake, Mary Majaliwa.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo hii Ijumaa, Mei 5, 2017
wakati akizungumza na waandishi wa habari mbele ya wakuu wa Masoko ya Hisa na
Dhamana; Soko la Hisa la Dar es Salaam, viongozi wa Baraza la Uwezeshaji na
kampuni ya Vodacom katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini
Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amewasihi Watanzania walioko ndani na nje ya nchi
wachangamkie fursa ya kununua hisa hizo ili waweze kuwa wamiliki wa kampuni
kupitia hisa zao. “Hii ni fursa kwa Watanzania kumiliki kampuni. Ukinunua hisa,
unashiriki kikamilifu kumiliki kampuni na pia unaboresha uchumi wako binafsi.
Ninawasihi Watanzania wote tumieni fursa hii kununua hisa hizo kabla muda
haujaisha,” alisisitiza.
Alisema watumishi wa umma wamepewa ya kununua hisa hizo kupitia
mipango iliyowekwa na Makatibu Wakuu wao lakini pia amewasihi viongozi
mbalimbali wa Serikali na taasisi wachangamkie fursa hiyo ili nchi iweze kupata
kodi kupitia makampuni hayo.
“Hii ni fursa kwa kila Mtanzania, kwa viongozi kwa taasisi na
mashirika ya umma, taasisi binafsi, wajasiriamali wadogo kama akinamama lishe
au madereva wa bodaboda. Watanzania walioko nje ya nchi (Diaspora) nao pia
wanunue hisa kwani watakuwa wanachangia uchumi wa nchi na wakati huo wanaweka
akiba nyumbani,” aliongeza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo,
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango uwekezaji kwenye hisa ni njia
mojawapo ya kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi.
“Huko mtaani ukisema uchumi wa nchi unakua, watu wanabisha
wakidai kuwa hawaoni unakua kwa sababu hawana fedha mifukoni. Hii ni fursa
nyingine ya kuwawezesha kukua kiuchumi, ninaomba waichangamkie,” alisema.
Alisema sekta ya mawasiliano ni miongoni mwa sekta inayokua kwa
kasi hapa nchini kwani katika robo tatu ya mwaka, sekta hiyo imekua kwa
asilimia 11.3. “Niwasihi Watanzania wenzangu, tununue hisa za Vodacom ili
tuweze kuboresha uchumi wetu,” alisema.
Alisema anatoa ombi maalum kwa wafugaji kukubali kuuza mifugo
yao na kununua hisa ili kupunguza idadi ya mifugo yao, jambo ambalo alisema
litapunguza migogoro baina yao na wakulima.
“Wakulima wa vitunguu, alizeti, maua au wafugaji wa samaki nao
pia wanaweza kununua hisa na kuwa na mitaji kwa ajili ya shughuli zao.
Ninawasihi wote watumie fursa hii ili kumiliki kampuni,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Soko la
Mitaji na Dhamana, Bi. Nassama Masinda alisema amefurahishwa kuona Waziri Mkuu
akinunua hisa za kampuni ya Vodacom katika soko la awali.
Alisema uuzwaji wa hisa hizo ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha
ya mwaka 2016 kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa makampuni ya
simu za mikononi hapa nchini. “Marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki
na Posta sura ya 306 yanazitaka kampuni za simu na mawasiliano ya kielektroniki
kuuza si chini ya asilimia 25 ya hisa zao kwa umma wa Tanzania kupitia masoko
ya mitaji (IPO).”
Alisema baada ya hapo hisa hizo zinapaswa kuorodheshwa kwenye
soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya
Mitaji na Dhamana, sura ya 79. Kampuni ya Vodacom ilitoa hisa milioni 560 kwa
umma kwa bei ya sh. 850 kila moja na hivyo kutarajia kukusanya sh. bilioni 476.
Alisema hivi sasa, wawekezaji kwenye masoko ya mitaji ni watu
500,000 tu ikilinganishwa na Kenya ambayo ina wawekezaji milioni 1.7; Uganda
(40,000) na Rwanda (14,000). “Vodacom ina wateja milioni 6.2, iwapo nusu ya
wateja wake wote watashiriki ununuzi wa hisa, idadi ya wawekezaji kupitia
masoko ya mitaji na dhamana itaongezeka kwa asilimia 1,140. Na haya yatakuwa ni
mageuzi makubwa katika sekta ya masoko ya mitaji si hapa nchini tu bali katika
Afrika Mashariki,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Dodacom, Bw. Ian Ferrao alisema mauzo ya hisa
yanayofanywa na kampuni hiyo ni makubwa mara nne ya mauzo ambayo yamewahi
kufanyika hapa nchini.
Alisema kampuni hiyo ambayo imekwishafanya kazi kwa miaka 17
hapa nchini, imewekeza zaidi ya sh. trilioni mbili katika mtandao wa
mawasiliano nchini Tanzania.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MEI 5, 2017.
SHARE
No comments:
Post a Comment