Naibu mwana mrithi wa Ufalme Saudi Arabia Mohammed bin
Salman mwenye umri wa miaka 31 amepandishwa cheo na kuwa mwana mrithi wa
ufalme kuchukuwa nafasi ya binamu wake katika tangazo la ghafla
Jumatano (21.06.2017)
Agizo la Ufalme limesema mwana mrithi wa ufalme Mohammed bin Nayef
mkuu wa kupiga vita ugaidi anayehusundiwa na serikali ya Marekani kwa
kuanzisha mashambulizi ya mabomu dhidi ya kundi la Al-Qaeda mwaka 2003
hadi mwaka 2006 ameondolewa katika nyadhifa zote na nafasi zake
kuchukuliwa na Mohammed bin Salman ambaye anakuwa naibu waziri mkuu na
kuendelea kushikilia nyadhifa za waziri wa ulinzi,mafuta na nyenginezo.Uamuzi wa Mfalme Salman kumpandisha cheo mtoto wake huyo wa kiume na kuimarisha madaraka yake umeidhinishwa na wajumbe 31 kati ya 34 wa Baraza la Utii linaloundwa na wajumbe waandamizi wa familia tawala ya Al Saud kwa mujibu wa agizo la kifalme lililotangaza hayo.
Wachambuzi wanasema mabadiliko hayo yanamuwezesha mwana mfalme Mohammed bin Salman kuendelea haraka na mpango wake wa kupunguza utegemezi wa mafuta wa Saudi Arabia ikiwa ni pamoja na kubinafsisha kwa nusu kampuni ya mafuta ya taifa ya Aramco.
Kuupa nguvu mpango wa mageuzi ya kiuchumi
John Sfakianakis mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Ghuba chenye makao yake mjini Riyadh anasema "Mabadiliko hayo ni kuupa nguvu mpango wa mageuzi ya kiuchumi,Dira ya 2030 na mabadiliko kamili ya mtizamo ambayo inayapitia Saudi Arabia na Mwana Mfalme Mohammed bin Salman ni muasisi wake."Amesema ni muhimu kwa mpango wake huo kuona unafuata dira yake inatekeleza na kuidumisha.
Bernad Haykel profesa wa masomo ya mashariki ya kati katika chuo kikuu cha Princenton anasema uamuzi wa mfalme umekusudia kuweka safi safu ya urithi wa ufalme kuepuka mapambano ya kuwania madaraka kati ya mtoto wake huyo wa kiume na Mohammed bin Nayef.
Ameongeza kufafanuwa kwamba "Ni mchakato wa kukabidhiana madaraka uliofanyika kwa utulivu bila ya umwagaji damu....na kwamba kutakuwepo na ufasaha zaidi kwa suala hilo hivi sasa. Hapo kabla kulikuwa na vurugu kidogo ambapo kila mtu alikuwa akiaguwa kile kitakachotokea.Sasa inajulikana wazi.
Kwa mujibu wa Haykel ufafanuzi huo unapunguza hatari, hakuna tena swali la nani atakayeongoza.
SHARE
No comments:
Post a Comment