Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto), akifafanua jambo
wakati akikagua mchoro wa Bandari kavu ya Kwala –Vigwaza Mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa
Eng. Charles Salu Ogare anayesimamia ujenzi wa bandari kavu ya
Kwala-Vigwaza Mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA) Eng. Deusdedit Kakoko akifafanua jambo kwa Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa alipokagua
maendeleo ya ujenzi wa bandari kavu ya Kwala –Vigwaza Mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa mwenye kofia ya njano akiwa katika
majukumu ya ukaguzi wa ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza
inayojengwa mkoani Pwani.
Muonekano wa bandari kavu
inayojengwa na mkandarasi Suma-KJT katika eneo la Kwala-Vigwaza
inayotarajiwa kuanza kutumika Januari mwakani ikiwa katika hatua
mbalimbali za ujenzi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini , Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
……………………..
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na kasi
ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Kwala Vigwaza Mkoani Pwani na
kumtaka mkandarasi Suma JKT kuongeza kasi na kuzingatia ubora.
Akizungumza mara baada ya kukagua
ujenzi huo ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kushirikiana na
Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS)
kuhakikisha wanaunganisha kwa haraka ili reli na barabara zinazoingia
katika bandari kavu hiyo zinakamilika na hivyo kuiwezesha bandari kavu
hiyo kuanza kutumika ifikapo Januari mwakani.
“TPA, TRL na TANROADS uzuri wote
mko kwenye wizara moja shirikianeni na hakikisheni kilomita 15 za
barabara inayoingia kwenye bandari kavu hii na kilomita moja ya reli
zinajengwa haraka,” Amesema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa amemtaka
Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko kuhakikisha ujenzi wa
bandari kavu ya Kwala-Vigwaza unazingatia ubora na viwango vilivyopo
katika mkataba ili kuiwezesha kuhudumia zaidi ya makontena milioni moja
kwa mwaka na hivyo kupunguza msongamano katikati ya Jiji la Dar es
Salaam.
“Hakikisheni eneo la bandari kavu
linakuwa na maegesho ya kutosha, taa, maji ya uhakika, gari la zimamoto,
uzio na mashine ya ukaguzi wa mizigo scanner itakayowezesha kupima kila mzigo unaopandishwa na kushushwa katika eneo hili,” amesisitiza Profesa Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng.
Kakoko amesema TPA imejipanga kuhakikisha ujenzi huo unatumia gharama
nafuu na mifumo yote ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA
inakuwepo katika bandari hiyo ili kuiwezesaha kufanya kazi kisasa na kwa
ufanisi zaidi.
“Tukifanikiwa kuhamia hapa mzigo
uliokuwa unasafirishwa kwa siku saba sasa utatumia siku tatu kufika
Mwanza hali itakayovutia wasafirishaji wengi kutumia bandari ya Dar es
Salaam na hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuibua fursa za ajira,” amesema
Eng. Kakoko.
Bandari Kavu ya Kwala –Vigwaza
inayojengwa na Mkandarasi SUMA JKT ambapo takribani kiasi cha shilingi
bilioni 9 kinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ili kuboresha huduma
za usafirishaji katika bandari ya Dar es Saalaam ambapo zaidi ya hekta
500 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo ambapo kwa kuanza hekta 120 sawa
asilimia 24 zinajengwa katika awamu ya kwanza.
SHARE
No comments:
Post a Comment