Lilian Lundo, Dodoma
Serikali imesema kila
Mtanzania anajukumu la kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kutotumia bidhaa
zenye madhara kwa Tabaka hilo katika biashara na shughuli za kila siku
za majumbani.
Hayo yameelezwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January
Makamba kupitia taarifa aliyoitoa leo, kwa vyombo vya habari juu ya Siku
ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni inayofanyika kila mwaka,
Septemba 16.
“Kwa kuzingatia kauli
mbiu ya mwaka huu ni muhimu tuzingatie kwamba juhudi za kila mmoja wetu
zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni
yanayosababishwa na bidhaa tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za
biashara ,” amefafanua Makamba kupitia taarifa hiyo.
Makamba amesema kuwa
kila mwananchi anatakiwa kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa
marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na
viyoyozi vilivyokwisha tumika (mitumba) na ambavyo vinatumia vipoozi
aina ya Chlorofluorocarbons (R11 na R12).
Vile vile amewataka
Watanzania kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo “Ozone
friendly” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali
zinazomong’onyoa Tabata la Ozoni.
Aidha amewaasa
Watanzania kuepuka kutupa hovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima
moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni aina ya ” CFCs” na
“halon”. Ila wanapotaka kutupa wanatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu
kutoka kwa mafundi ama mamlaka zinazohusika.
Pia mafundi wa majokofu
na viyoyozi wametakiwa kuhakikisha kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi
kutoka kwenye viyoyozi na majokofu wanayohudumia badala ya kuviacha
huru visambae angani.
Mafundi hao wanatakiwa
kutoa elimu kwa wateja wao kuhusu njia rahisi ya kutambua uvujaji wa
vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wavyotumia.
Kitaifa, maadhimisho ya
Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yatafanyika kwa njia ya
uelimishaji Umma kuhusu Tabaka la Ozoni, faida zake, madhara ya
kuharibika kwa Tabaka hilo na matumizi salama ya bidhaa zenye kemikali
rafiki kwa Tabaka hilo.
Kauli mbiu ya mwaka huu
katika kuadhimisha siku hiyo ni “Kutunza na Kulinda Viumbe Hai Duniani” (
Caring for All Life Under the Sun).
SHARE
No comments:
Post a Comment