Na Venance Matinya, Mbeya
SERIKALI imeahidi
kufanya utafiti ili kubainia Taasisi za Elimu ambazo bado zinaendeleza
Unyanyasaji wa Kijinsia kwa wanawake na kuchukua hatua stahiki zitakazotoa
fundisho kwa maeneo mengine.
Naibu Spika Dk Tulia
Ackson alitoa ahadi hiyo alipofungua Mkutano wa nne wa Kamati ya Wanawake Taifa
ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya juu nchini(THTU) uliofanyika
jijini Mbeya.
Dk Tulia alisema
Serikali imekuwa ikifanya kila juhudi kuhakikisha unyanyasaji wa kijinsia
unakomeshwa katika Taasisi za Elimu lakini kwakuwa bado kuna malalamiko ipo
haja ya kufanyika kwa utafiti ili kubaini maeneo ambayo yanaendeleza tabia
hiyo.
Alisema hakuna mwanamke
aliye mwanafunzi au mfanyakazi anayetakiwa kuendelea kunyanyasika kwa kwa
kulazimishwa kufanya mapenzi ili aweze kufaulu au kupanda cheo na popote palipo
na mazingira hayo ni lazima pafanyiwe kazi ili kurekebisha.
Hata hivyo Dk Tulia
amewasihi watumishi na wanafunzi wa kike kutambua kuwa wao ndiyo walio na
maamuzi ya kukataa unyanyasaji wa namna hiyo kwa kuweka misimamo yenye kulenga
kulinda heshima na utu wao ndani ya jamii.
Kwa upande wake Katibu
wa Kamati ya Wanawake Taifa ya THTU, Amina Mdidi alizitaja changamoto zinazoendelea
kuwakabili wafanyakazi wanawake kwenye taasisi za Elimu ya juu kuwa ni pamoja
na Uhaba wa vitendea kazi,mazingira yasiyo rafiki na ongezeko la makato kwenye
mishahara.
Ameshauri pia Serikali
kupitia upyaa mitaala ya masomo kuanzia shule za msingi ili kuwezesha wanafunzi
kujifunza kwa Nadharia na vitendo hatua aliyosema itawajengea uwezo wanafunzi
wa kujiajiri kupitia ujasiriamali na pia uzalendo kwa Taifa lao.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa
THTU,Dk Emeria Mgonzibwa alisema Sera ya Viwanda inayoendelea kupiganiwa na
Rais Dk John Magufuli na Waziri wa Viwanda Charles Mwijage itawezekana pale
Taasisi za Elimu ya juu zitakapotoa wahitimu walio na ujuzi wa kutosha na
wanaoweza kuajiriwa na kujiajiri.
Mwisho.
SHARE
No comments:
Post a Comment