Kaimu
Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna ( wa pili kutoka
kulia) akielezea majukumu ya kampuni hiyo mbele ya Waziri wa Nishati na
Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wa Wizara ya
Nishati na Madini pamoja na Taasisi zilizopo chini yake.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akielezea fursa za uwekezaji katika sekta ya gesi nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna akisisitiza jambo katika kikao hicho.
Kaimu
Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna (kushoto) na
Mwenyekiti wa Kampuni ya Pan African Energy Nchini Patrick Rutabanzibwa
(kulia) wakinukuu maelekezo kutoka kwa Wiziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amelitaka Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini
(TPDC) kufanya kazi katika mtindo wa kisasa ili nishati ya umeme iweze
kuwa ya uhakika kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.
Profesa
Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake na Kampuni ya Pan African
Energy kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilichoshirikisha pia
watendaji kutoka wizara ya nishati na madini, TANESCO, TPDC na Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema
mahitaji ya gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika ni makubwa,
hivyo hakuna sababu ya kuwepo kwa upungufu wa nishati ya umeme
nchini wakati kuna gesi ya uhakika.
Alifafanua
kuwa haiwezekani shirika la TPDC likadai kuwa kuna gesi ya kutosha kwa
ajili ya kuzalisha umeme, wakati kuna upungufu wa umeme nchini.
Alisema
serikali ina mpango wa kuhakikisha kuwa wananchi wote hasa waishio
vijijini wanaunganishwa na umeme wa uhakika kupitia Wakala wa Nishati
Nchini (REA) hivyo ni jukumu la mashirika hayo kuhakikisha yanabuni
miradi na kukaribisha wawekezaji mbalimbali katika uzalishaji wa umeme
wa uhakika ili wananchi wote waweze kuunganishwa na huduma ya umeme.
Alisisitiza
kuwa amekwishawaalika wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza
kwenye uzalishaji wa Megawati 1000 za umeme kwa ajili ya kuingizwa
kwenye gridi ya taifa, hivyo ni vyema shirika la TPDC likahakikisha
gesi ya uhakika inapatikana ili umeme uweze kuzalishwa mara moja.
“
Lengo la serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ni kuhakikisha
kuwa ifikapo mwaka 2025 Megawati 10,000 zinazalishwa, hivyo sekta ya
nishati kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kutoka kwenye kundi la
nchi masikini duniani na kuingia kwenye kundi la nchi za kipato cha
kati, kama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, inavyofafanua,”alisema
Profesa Muhongo.
Wakati
huo huo, Profesa Muhongo aliitaka kampuni ya Pan Afrian Energy
kuhakikisha inatatua changamoto zote inazozikabili kwa kipindi cha
miezi mitatu kabla ya kukutana naye Juni 01 mwaka huu kwa ajili ya
kupokea mapendekezo ya kampuni hiyo katika kuzalisha gesi ya uhakika.
Alisisitiza
kuwa kutakuwepo na utaratibu wa kukutana na kampuni hiyo kila baada ya
miezi mitatu kwa ajili ya kujadili utendaji kazi wa kampuni hiyo, na
serikali ipo tayari kutoa msaada pale kampuni itakapokwama.
Aidha,
Profesa Muhongo aliitaka kampuni hiyo kuweka utaratibu wa kuajiri
vijana wa kitanzania wanaomaliza masomo ndani na nje ya nchi baada ya
kupata ufadhili kutoka serikalini.
“
Kwa sasa tuna vijana wengi waliohitimu mafunzo kwa ngazi ya shahada
za uzamili katika masuala ya mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali
ndani na nje ya nchi kama Norway, Uingereza na China, hivyo ni vyema
wakapata ajira katika kampuni ya Pan African Energy, ili nao waweze
kufaidika na elimu na uwepo wa uwekezaji katika shughuli za utafutaji na
uchimbaji wa gesi na mafuta nchini,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna,
akielezea mafanikio ya uwekezaji kupitia kampuni yake, alieleza kuwa
kampuni hiyo imefanikiwa kutoa ajira 87 kwa watanzania na kuboresha
huduma za jamii kama vile kutoa huduma ya umeme bure katika eneo la
Kilwa kilipo kituo chake za kuzalisha gesi.
Aliendelea
kusema kuwa kampuni ya Pan African Energy imejenga zahanati pamoja na
kutoa mafunzo kwa waajiriwa wake lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa
kampuni hiyo inakuwa na wataalam wazawa.
SHARE
No comments:
Post a Comment