VIJANA
wasomi wanaounda Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Tanzania (TAYODA)
wameeleza mafanikio wanayopata baada ya kuamua kujikita katika kilimo
cha vitunguu tangu mwaka 2013, muda mfupi baada ya kumaliza elimu yao ya
vyuo vikuu.
Vijana
hao wanaomiliki shamba lenye ukubwa wa heka 300 katika kijiji cha
Idodoma wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, wamewataka vijana wanaolalamika
kukosa ajira, kuunga mkono kauli ya hivikaribuni ya Rais Dk John
Magufuli inayowataka wafanye kazi badala ya kucheza pool toka asubuhi.
Akizungumza
na wanahabari waliotembelea shamba lao hilo hivikaribuni, Mkurugenzi wa
TAYODA, Jackson Kangoye alisema; “taasisi imefanikiwa kukuza mitaji ya
vijana walioko mitaani kwa kupitia sekta hii ya kilimo.”
Alisema
mwaka 2013 walipoanza na vijana 25 walifanikiwa kulima zao hilo katika
shamba lenye ukubwa wa heka 30, wakaendelea kupata mafanikio
yaliyowazesha kupata shamba lenye ukubwa wa heka 300 huku idadi ya
vijana wanaojishughulisha na kilimo hicho ikiongezeka hadi 230 mwaka
huu.
“Lengo
letu katika kipindi cha miaka mitatu ni kuwaingiza katika shughuli hii
vijana 2500 walioko mitaani bila kujali viwango vya elimu,” alisema.
Kangoye
alisema wakiwa shambani vijana hao ugawanywa katika makundi ya watu
watano ambapo kila kundi hupewa heka tano kwa msimu mmoja na kuzitumia
kupata mitaji.
“Tangu
tuanze kilimo hiki uzoefu wetu unaonesha kwa kila heka moja, tunazalisha
kati ya gunia 80 na 120 za zao hilo ambalo uuzwa kwa kati ya Sh 120,000
na Sh 170,000 ambazo ni sawa na wastani wa Sh Milioni 10 na Sh Milioni
20 kwa heka,” alisema.
Alisema
kiasi kinachobaki baada ya kutoa asilimia 25 ya pato lote linalokwenda
katika taasisi hiyo kwa ajili ya kusaidia vijana wengine na gharama zote
za matumizi, hutolewa kwa vijana hao kama mtaji wanaoweza kuutumia
kujiendeleza katika kilimo hicho katika mashamba yao wenyewe.
Kangoye
alisema zaidi ya vijana 120 wamekwishanufaika kiuchumi kupitia mpango
huo kwa kuanzisha miradi yao ya kilimo cha vitunguu, pilipili, tikiti na
nyanya.
"KILONGE"
SHARE
No comments:
Post a Comment