
Mahakama
ya kimataifa ya uhalifu ICC imefuta kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya
William Ruto Jumanne (05.04.2016) ikisema hakukuwa na ushahidi wa
kutosha wa ushiriki wake katika vurugu za baada ya uchaguzi wa
2007/2008.
Jaji
aliyesimamia kesi hiyo alisema yumkini sababu ya kukosekana kwa ushahidi
ilikuwa uingiliaji wa mashahidi na ushawishi wa kisiasa. Tangazo la
mahakama hiyo linaonyesha mara ya pili ambapo mahakama ya ICC imekubali
kushindwa katika jitihada zake za kuwashtaki wanaodaiwa kupanga na
kufadhili vurugu zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 na
kuwalazimisha wengine 600,000 kuyakimbia makazi yao nchini Kenya.
Naibu
Rais William Ruto alishtakiwa sambamba na mtangazaji wa redio Joshua
Sang, kwa makosa ya mauaji, kuwalazimisha watu kuyahama makaazi yao na
utesaji kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ushiriki wao katika vurugu
hizo. Kesi dhidi ya Sang pia ilihitimishwa siku ya Jumanne.
Televisheni
za nchini Kenya ziliwaonyesha wawili hao wakipunga mikono hewani
kusherehekea ushindi huku wafanyakazi wa ofisi ya Ruto wakimkumbatia
kumpongeza. Picha hizo pia ziliwaonyesha mamia ya watu katika mji wa
Ruto wa Eldoret wakishangilia.
'Ni thibitisho la kutokuwa na hatia!
Rais wa
Kenya Uhuru Kenyatta alisema kufungwa kwa kesi hiyo ni uthibitisho
kwamba naibu wake pamoja na mwandishi habari Sang hawakuwa na hatia.
"Ni
bahati mbaya kwamba ICC iliwapa Wakenya matumaini ya uongo, na matokeo
yake imesababisha ukataji tamaa mkubwa. Tutafanya kila kitu kuwafidia
Wakenya pale mahakama hii ilipowaangusha," alisema Kenyatta katika
taarifa.
Kesi
dhidi ya Kenyatta katika mashtaka sawa na hayo ilivunjika Desemba 2014
baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa kulikuwepo na uingiliaji katika
mashahidi, na kukosa ushirikiano kutoka kwa utawala mjini Nairobi.
Wakati
huo, mwendesha mashtaka mkuu Fatou Bensouda, aliilaumu Kenya kwa kuzuwia
uchunguzi wake na kuitaja siku hiyo kuwa ya giza katika utoaji haki
dhidi ya uhalifu wa kimataifa. Wakenya watatu wameshtakiwa kwa kuingilia
mashahidi.
Kuvunjwa moyo kwa waathirika
Wakili
anayewawakilisha waathirika wa machafuko hayo katika mahakama ya ICC
Wilfred Nderitu, alisema kufutwa kwa kesi hiyo kabla ya kutolewa hukumu
lilikuwa jambo la kuvunja moyo, na kuwataka waendesha mashtaka kukata
rufaa.
"Hakuna
shaka kwamba uamuzi huu utakuja kama jambo la kuvunja moyo kwa
waathirika," alisema Nderitu wakati akizungumza na waandishi wa habari
mjini Nairobi. "Ni matumaini yangu kwamba waendesha mashtaka watakata
rufaa."
Elizabeth
Evenson, wakili mwandamizi wa kimataifa kutoka shirika la kutetea haki
za binaadamu la Human Rights Watch, alisema kushindwa kwa waendesha
mashtaka kuwashtaki waliopanga uhalifu dhidi ya Wakenya, "kunawaacha
waathirika wakiwa wamenyimwa haki na msaada wanavyovihitaji."
Alisema kesi ya Ruto itakumbukwa kwa juhudi zilizoripotiwa juu ya kuwahonga mashahidi.
Mchambuzi
wa masuala ya kimataifa kutoka Kenya Agina Ojwang aliiambia DW katika
mahojiano kuwa kutokuwa makini kwa ICC mwanzoni mwa kesi hiyo - katika
kuwalinda mashahidi ndiyo kumechangia kesi hiyo kushindwa, ambapo
alitaja kuuawa kwa baadhi ya mashahidi hao katika mazingira ya
kutatanisha, na wengine kupotezwa kabisa.
Mashtaka yanaweza kufunguliwa upya
Katika
uamuzi wao siku ya Jumanne, wajumbe wawili wa jopo la majaji waliamuru
kesi hiyo ifutwe, ingawa walisema mashtaka yanaweza kufunguliwa tena
ikiwa kutakuwa na ushahidi wa kutosha.
Kulingana
na taarifa ya mahakama, jaji msimamizi Chile Eboe-Osuji alisema kesi
hiyo inaweza kuelezwa na matukio yalioonyesha kutiwa madoa mchakato wa
mashtaka kwa kuingilia mashahidi na ushawishi wa kisiasa, ambavyo
vilionekana kuwatishia mashahidi.
Majaji wa
rufaa watoa hukumu mwezi Februari kwamba matamshi yaliyotolewa na
mashahidi watano ambao baadaye walibadilisha maelezo yao au kukataa
kutoa ushahidi dhidi ya Ruto na Sang, yasingeweza kutumiwa kama
ushahidi, uamuzi ambao huenda uliharakisha kuvunjika kwa kesi hiyo.
Awali,
waendesha mashtaka wa ICC waliwashtaki Wakenya sita kwa makosa
yanayohusiana na ghasia za baada ya uchaguzi, na mashtaka dhidi ya watu
hao wote sita yameondolewa.
Waathirika wataka fidia
Zephania
Mwangi, ambaye babu yake alikatwa hadi kufa na kundi la watu wenye
hasira katika eneo la mabanda lililoshuhudia kuripuka kwa vurugu baada
ya uchaguzi wa mwaka 2007, alisema mahakama ya ICC inapaswa kuwafikiria
waathirika.
"Kama mtu
alipoteza mali au ndugu, wanapaswa kufidiwa angalau ili waweze kurejea
katika maisha yao ya kawaida," alisema kabla ya kuchapishwa kwa uamuzi
wa majaji wa mahakama hiyo.
Madai ya
uingiliaji mkubwa dhidi ya mashahidi unatilia mkazo tatizo kubwa
linaloikabili mahakama hiyo, iliyoundwa kwa lengo la kuwashtaki
washukiwa wanaochukuliwa kuhusika na unyama. Hilo linamaanisha kuwa
wakati mwingine kuwashtaki wanasiasa na kutegema polisi wao na vyombo
vingine vya usalama kwa kutoa ushirikiano. BBC
SHARE
No comments:
Post a Comment