Waziri
Edwin Ngonyani akimsikiliza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na
Umeme (TEMESA) Mhandisi. Manase Ole Kujan alipofanya ziara katika idara
hiyo hivi karibuni.
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Wakala wa
Ufundi na Umeme(TEMESA) imewazuia wamiliki na waendeshaji wa karakana
teule zilizopewa mamlaka na TEMESA kutengeneza magari na vifaa vya
Serikali kutofanya matengenezo ya magari na vifaa hivyo bila kufata
utaratibu wa wakala.
Akizungumza
katika kikao kati ya TEMESA, wamiliki na waendeshaji wa karakana teule,
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Manase Lekujan amesema
karakana teule zinatakiwa kufata taratibu husika katika kufanya
matengenezo ya magari na vifaa vya Serikali.
“Tumeitisha
kikao hiki na wamiliki wa karakana teule tunazofanya nazo kazi ili
tukumbushane kuhusu kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu
zilizopo kwenye mikataba yetu, katika kuweka mpango mzuri wa kuwa na
taarifa sahihi za matengenezo ya magari na vifaa vya Serikali katika
karakana zetu ili kuondokana na changamoto zilizopo na kuongeza ufanisi
wa kazi zetu” Alisema Mhandisi Manase.
Akifafanua
kuhusu Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2011, Mwanasheria wa TEMESA, Gratian
Mali amesema sheria inatoa nafasi kwa Wakala wa Ufundi na Umeme
kutafuta karakana binafsi kusaidia shughuli za matengenezo ya magari na
vifaa vya Serikali pale ambapo karakana za Serikali zinapokuwa na kazi
nyingi au kukosa baadhi ya vifaa kwa ajili ya matengenezo na kazi hizo
hutolewa kwa vibali maalumu kutoka TEMESA.
Akizungumza
mara baada ya kikao na TEMESA mmoja wa wamiliki wa karakana ya Nduvin
Auto Works, Al Haj Masoud Msangi amesema kikao hicho kimekuwa cha
mafanikio kwani imefika wakati kwa karakana teule kutekeleza agizo la
kutengeneza magari na vifaa vya Serikali kwa kufata Sheria na taratibu
zilizopo na sio kufanya shughuli zake kiholela.
TEMESA
imeanzishwa chini ya Sheria ya Wakala Na 30 ya mwaka 1997 na
ilizinduliwa rasmi Juni 23 mwaka 2006 na ina kazi ya kufanya matengenezo
ya magari na vifaa vya Serikali,kusimamia huduma za vivuko na usimikaji
na matengenezo ya mifumo ya umeme na eletroniki. (P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment