

Ndugu zangu,
Tumeona,
kuwa Idi Amin ameishi kwa anasa na mashaka makubwa. Amin hakumuamini mtu
yeyote. Nguvu yake kubwa ilikuwa kwenye jeshi na askari kanzu. Wengi wa
askari wake walitoka kabila lake la Kakwa na Wanubi wa Sudan.
Idd Amin
aliongea lugha kadhaa lakini hakuna lugha aliyoimudu barabara isipokuwa
lugha ya kabila lake la Kakwa. Aliongea Kiswahili , cha tabu kidogo.
Aliongea Kiingereza, cha tabu kidogo. Kiarabu alijua kidogo pia. Kiganda
hivyo hivyo.
Alipokuwa
akihutubia hakuonyesha kuwa anakaribia kumaliza hotuba yake. Mara
nyingi alimaliza hotuba huku watu wakidhani anaendelea.
Inasemwa,
kuwa alifanya hivyo kwa sababu za kiusalama. Idd Amin alijua wengi
hawakujua lugha yake ya Kikakwa. Kwa vile walinzi wake wa karibu ni wa
kabila lake, basi, alipokaribia kumaliza hotuba yake aliingiza maneno ya
lugha ya kabila lake ili kuwaandaa walinzi wake mara atakaposimama
ghafla na kuondoka ukumbini.
Kikosi
chake cha makachero kilikuwa kinahofiwa sana. Vilikuwa vikosi viwili;
Public Safety Unit ( Usalama wa Taifa) na State Research Bureau. Hicho
cha mwisho ndio kilikuwa kiboko ya vyote.
Kiliundwa
na mabayaye kutoka kabila la Idd Amin. Vijana waliokuwa na elimu ya
chini na wengi aliwatoa mitaani. Ndani ya kikosi hicho kulikuwa pia na
watu kutoka makabila ya Lugbara ( kabila la mama yake Amin) Madi na
Wanubi wa Sudan.
Makachero
hao walikuwa na mazoea ya kuvaa mashati ya vitenge. Enzi hizo Uganda,
jirani yako akikuambia kuwa umefuatwa nyumbani na watu wanaovaa
'Chitenge', na wakakukosa, basi, cha kufanya si kuwasubiri warudi tena.
Unachotakiwa ni kuchukua kinachochukulika na kuutafuta mpaka wa nchi
jirani ya karibu na ulipo.
Jamaa hao
wavaa ' Chitenge' walitisha sana. Inasemwa, kuwa kila mmoja katika
kikosi hicho alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Idd Amin.
Katikati ya Jiji la Kampala walikuwa na ofisi zao. Ni katika majengo
kadhaa. Yalitumika pia kama vituo vya kuwatesa wapinzani au waliodhaniwa
wangekuwa wapinzani wa Idd Amin. Ilitokea mtu akapita mitaa ya Kampala
na kusikia sauti za watu wanaolia kwa kuteswa. Ilikuwa ni mambo ya
kawaida.
Wengi
waliteswa hadi kufa. Mara nyingi walitupwa Ziwa Victoria na kuachwa
wakiliwa na samaki. Kuna simulizi za wakazi wa kando ya ziwa kuamka na
kukuta lori likiwa na walichodhani ni samaki wakubwa. Watu walikimbilia
kuwahi kununua samaki hao. Walishangaa kuona ni miili ya binadamu
iliyopelekwa kutupwa ziwani.
Pamoja na
yote hayo, Idd Amin alikuwa mume wa wake wanne. Alikuwa na mabibi wa
pembeni pia. Inasadikiwa, kuwa idadi ya watoto wa Idd Amin ilifikia
hamsini!
Katika
watoto wote wa Amin , inasemwa kuwa, Idd Amin alimpenda sana Moses (
Pichani). Na katika wake zake wote, alipempenda sana Nadina ( Pichani)
Mara
nyingi Amin alionekana akiwa na mtoto Moses. Alimpenda kiasi katika umri
mdogo kumvalisha magwanda ya jeshi. Moses alianza kushika bastola
katika umri mdogo pia. Hivyo hivyo mkewe Nadina, Idd Amin alimpenda sana
Nadina. Amin alionekana mara kwa mara akiwa na Nadina kando yake.
Naam.
Simulizi juu ya Idi Amin ni nyingi. Tukijaaliwa, kesho tutachambua
ukweli juu ya madai kuwa Idd Amin alimwua mwanawe kipenzi Moses kwa
sababu za kishirikina . Inasemwa pia, kuwa aliwahi kumwua mmoja wa wake
zake kwa sababu za kishirikina. Je, kuna ukweli katika hayo?
Nitakusimulia..
Maggid,
Iringa.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment