Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine
Mahiga amesema Tanzania imepokea nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya TROIKA
ya Siasa na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC) inayosimamia masuala ya Ulinzi na Usalama.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Balozi Mahiga alisema
Tanzania imepata nafasi hiyo wakati wa Mkutano wa SADC uliojadili masula
ya Ulinzi na Usalama uliofanyika hivi karibuni mjini Maputo, Msumbiji.
“Mheshimiwa
Rais John Pombe Magufuli atapokea nafasi hiyo ya kuwa mwenyekiti wa
TROIKA kutoka kwa Rais wa sasa wa Msumbiji, Filipe Nyusi, nafasi
inayodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja” alisema Balozi Mahiga.
Aliongeza kuwa Mkutano huo wa TROIKA unatarajiwa kufanyika Agosti 29 na 30 mwaka huu huko Mbabane nchini Swaziland.
Aidha,
Balozi Mahiga alisema kuwa SADC ni jumuiya iliyopiga hatua katika
kusimamia masuala ya ulinzi, usalama na diplomasia jambo ambalo haliko
katika jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo kusaidia kutatua masuala
yanayohusu hali tete za usalama katika ukanda huo.
Kwa
mujibu wa Waziri Mahiga alisema mkutano wa TROIKA ni sehemu ya
maandalizi ya kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika kinachotarajiwa kufanyika baadae mwezi huu ambapo, taarifa ya
hali tete ya usalama ya nchini Lesotho itatolewa.
Waziri
Mahiga, alisema katika mkutano wa SADC uliofanyika mapema mwezi huu
Maputo Msumbiji uliitaka nchi ya Lesotho kutekeleza masuala kadhaa
katika kutafuta suluhu ya matatizo nchini humo, ikiwemo kufanya mageuzi
ya katiba, mageuzi ya sekta ya ulinzi na usalama pamoja na kufanya
marekebisho katika sekta ya utawala. Mkutano huo wa SADC, vilevile
unatarajiwa kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili jumuiya hiyo
ikiwemo mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
kufuatia kuibuka kwa makundi mbalimbali yanayohatarisha amani mashariki
mwa nchi hiyo
Na. Immaculate Makilika na Abushehe Nondo- MAELEZO
Dar es Salaam
11.8.2016 (P.T)
Dar es Salaam
11.8.2016 (P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment