
Waasi
wanaoungwa mkono na Uturuki wamekabiliana na vikosi vinavyoungwa mkono
na Wakurdi kaskazini mwa Syria, huku jeshi la Uturuki likiendeleza
kampeni yake ndani ya ardhi ya Syria.
Serikali
ya Uturuki, ambayo yenyewe inapambana na uasi wa Wakurdi ndani ya ardhi
yake, inasema kampeni yake nchini Syria inahusiana pia na kuwazuwia
Wakurdi kutwaa maeneo zaidi ndani ya Syria sambamba na kuwarejesha nyuma
wapiganaji wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS).
Uturuki
inataka kuwazuwia wapiganaji wa Kikurdi kujiimarisha ndani ya Syria
karibu na mpaka wake, jambo ambalo inahofia litakipa nguvu chama cha
Wakurdi, PKK, ambacho kimekuwa kwenye vita vya miongo mitatu sasa
kuwania utawala wake wa ndani.
Vyanzo
kutoka vyombo vya usalama vya Uturuki vinasema ndege mbili chapa F-16
zililishambulia eneo linalodhibitiwa na wanamgambo wa YPG wa Kikurdi,
ambao ni sehemu ya muungano wa wapiganaji wanaoungwa mkono na Marekani,
Syrian Democratic Forces (SDF). Vyanzo hivyo vinasema ndege hizo
zilishambulia pia maeneo sita yanayodhibitiwa na IS.
Askari wa Uturuki auawa
Jeshi la
Uturuki lilisema askari wake mmoja aliuawa na watatu wengine kujeruhiwa
pale kifaru chao kiliposhambuliwa kwa roketi ambalo lilirushwa kutoka
eneo linalodhibitiwa na wapiganaji wa YPG. Jeshi lilijibu mashambulizi
hayo kwa kulitwanga eneo hilo kwa mizinga.
Waasi
nchini Syria wanaopingana na uingiliaji kati huu wa Uturuki wanasema
kuwa jeshi la Uturuki lilivishambulia vikosi vyenye mafungamano na YPG
lakini hakukuwa na vikosi vya Wakurdi kwenye eneo hilo. Waasi wanaoungwa
mkono na Uturuki walipambana na wapiganaji wenye mafungamano na SDF
karibu na mji wa Jarablus.
Vikosi vinavyopingana na Uturuki vilisema Uturuki imetuma vifaru vyake kwenye mji huo, ingawa serikali mjini Ankara ilikanusha.
Kwenyewe
nchini Uturuki, watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kikurdi walirusha
makombora katika uwanja wa ndege wa mji mkubwa wa kusini mashariki wa
Diyarbakir.
Kwa
mujibu wa shirika la habari la Dogan, makombora yapatayo manne
yalilengwa kwenye kituo cha ukaguzi cha polisi kilichopo nje ya ukumbi
wa kupumzika, ambapo wafanyakazi na abiria walilazimika kuhamishiwa
sehemu salama.
Diyarbakir ni mji mkuu katika eneo la kusini mashariki mwa Uturuki linalokaliwa kwa kiasi kikubwa na Wakurdi.DW
SHARE








No comments:
Post a Comment