Rais wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, amesema kuwa taasisi za
Serikali pamoja na yeye mwenyewe wataheshimu katiba ya nchi, ambapo
ameahidi nchi hiyo kufanya uchaguzi ulio huru na haki.
Akihutubia
bunge la kitaifa na baraza la seneti, rais Kabila amepongeza
makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kutokana na mazungumzo ya kitaifa
yaliyosimamiwa na mpatanishi wa umoja wa Afrika, Edem Kodjo.
Rais
Kabila amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni, sasa ndio
yanakuwa moyo wa nchi kuelekea mbele. "Makubaliano yaliyofikiwa ni
ishara kuwa nchi ya Kongo ina uwezo wa kutatua mambo yake yenyewe bila
kusaidiwa na mataifa kutoka nje," alisema rais Kabila ambaye muda mwingi
alikuwa akishangiliwa na vijana walioingia bungeni.
Edem Kodjo, mpatanishi wa mzozo wa kisiasa nchini DRC.
Rais
Kabila ameongeza kuwa, yeye kama rais jukumu lake ni kuhakikisha
anailinda katiba ya nchi hiyo na kwa kuanzia, atahakikisha analinda
makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni, ambayo yamepelea kuundwa kwa
Serikali ya mseto kuelekea uchaguzi mkuu.
Aidha
amewataka wanasiasa wa upinzani ambao hawakushiriki kwenye mazungumzo ya
kitaifa, waende ofisini kwake na kwamba atakuwa tayari kuwapokea ili na
wao watie saini makubaliano ambayo amesema yatatatua sintofahamu ya
kisiasa inayoshuhudiwa nchini humo.
Kiongozi
huyo amewakashifu wanasiasa wa upinzani ambao amedai wanatumiwa na
baadhi ya nchi za magharibi kuchochea vurugu nchini humo, ambapo ameapa
kupambana nao.
"Sitakuwa
tayari kuona vijana wanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kufanya vurugu,
wakati wanaowatuma wanatumia mwanya huo kujificha nyuma yao, wakitaka
kuona taifa la kongo likitumbukia katika machafuko," alisema rais
Kabila.
Kwenye
hotuba yake rais Kabila pia, ameyaonya mataifa ya magharibi
yanayoingilia masuala ya ndani ya nchi yake, ambapo amesema mataifa hayo
yasitarajie kuwa yatashinda ama kufanikiwa kuchochea vurugu nchini
humo.
Kuhusu
Mustakabali wake, rais Kabila ameendelea kusisitiza kuwa ataheshimu
katiba ya nchi na taasisi zake, kauli ambayo ni wazi inaashiria kuwa
hatawania tena urais wakati kipindi chake cha mpito kitakapomalizika,
akimaliza uvumi uliokuwepo kuwa, huenda akatangaza nia ya kuendelea
kusalia madarakani.
Rais
Kabila amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni yamefikiwa na
wanadamu na sio malaika na kwamba bado kuna nafasi ya huko mbeleni
makubaliano hayo kufanyiwa marekebisho kwa mustakabali wa taifa hilo.
Kuhusu
Usalama: Kwenye hotuba yake rais Kabila amezungumzia suala la usalama wa
mashariki mwa nchi hiyo, ambapo amesema umeendelea kuimarika licha ya
changamoto ambazo bado zimeendelea kushuhudiwa.
Rais
Kabila amekiri kuwa suala la usalama kwenye eneo la mashariki bado ni
changamoto, na kwamba kundi la FDLR na lile la wapiganaji wa kiislamu wa
ADF-NALU ndio makundi yaliyosalia na ambayo yanatatiza usalama kwenye
eneo hilo.
Kiongozi
huyo akawahakikishia wananchi wake kuwa, jeshi la nchi hiyo pamoja na
kikosi maalumu cha umoja wa Mataifa, wanaendelea na operesheni za
kuwasambaratisha wapiganaji hao ambao amesema ndani ya siku chache
zijazo watakuwa wamemalizwa.
Mustabali
wa Uchaguzi: Hata hivyo baadhi ya raia wa DRC ambao wamezungumza na
idhaa hii punde baada ya kumaliza hotuba yake, mbali na kupongeza hatua
ambazo nchi yao imepiga toka kuingia madarakani kwa rais Kabila, wapo
waliokosoa.
Wakosoaji
wake wanadai kuwa walitarajia kuona kiongozi wao akitamka waziwazi kuwa
hatawania tena kiti hicho kwenye uchaguzi ujao, suala ambalo hata hivyo
rais Kabila hakusema wazi na badala yake akasisitiza kuheshimiwa kwa
katiba.
Kwa
upande mwingine wapo raia ambao wao wanaona kuwa hotuba ya rais Kabila
ilijikita katika masuala mtambuka ya nchi hiyo, hasa uchaguzi na
maridhiano ya kisiasa ambayo wamesema kupitia makubaliano yaliyotiwa
saini nchi hiyo itaandaa uchaguzi ulio huru na haki.
Uchaguzi
uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, sasa hautafanyika
tena chini ya makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni na badala yake
sasa, uchaguzi mwingine utaandaliwa na Serikali ya mpito itakayotangazwa
hivi karibuni na unatarajiwa kufanyika mwaka 2018.
Masuala
ya Kijamii na Uchumi: Rais Kabila amezungumzia maendeleo ya elimu nchini
humo, ambapo amesema kuwa wakati akiingia madarakani bajeti ya elimu
ilikuwa ni asilimia 6 pake yake na sasa anapoelekea kuhitimisha mihula
yake, bajeti ya elimu imefikia asilimia 16.
Kuhusu
miundombinu rais Kabila amekiri kuwa nchi yake bado inakabiliwa na
changamoto ya miundombinu imara, akikiri kuwa usafiri pekee uliokuwa
unatumiwa muda mwingi ni usafiri wa anga, lakini sasa amefanikiwa
kujenga barabara imara kwenye maeneo mengi ya nchi na sasa yanafikika
kwa urahisi.
Rais Kabila pia amesema huduma za Afya zimeendelea kuimarika sambamba na upatikanaji wa umeme wa uhakika nchi nzima.RFI
SHARE
No comments:
Post a Comment