Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inasema ina sababu za kimsingi kuamini
kuwa wanajeshi wa Marekani wamefanya matendo ya uhalifu wa kivita na
hivyo kuashiria kuwepo uwezekano wa kuwafungulia mashitaka.
Katika
ripoti yake ya awali, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda,
amesema kuwa kwa uchache kuna visa 61 vilivyorikodiwa, ambapo matukio ya
utesaji, ukatili na kuvunja heshima ya watu yanahusika. Ripoti hiyo pia
inataja visa vyengine 27 vya watu walioteswa na Shirika la Ujasusi la
Marekani (CIA) vingi vyao vikitokea baina ya mwaka 2003 na 2004.
Ripoti
hii iliyotolewa Jumatatu (14 Novemba) inahoji kwamba uhalifu unaodaiwa
kutendeka haukuwa matukio yaliyojitenga kando, bali ni sehemu ya mbinu
zilizothibitishwa na Marekani katika majaribio ya kupata taarifa kutoka
kwa mahabusu.
"Kuna
ushahidi wa kutosha kuamini kuwa uhalifu huu ulitendeteka katika
kuendeleza sera ya kupata taarifa kupitia matumizi ya mbinu za mahojiano
zinazojumuisha njia za kikatili au fujo, ambazo zingelisaidia malengo
ya Marekani nchini Afghanistan." Bensouda anasema kwenye ripoti hiyo.
Marekani yakanusha
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Elizabeth Trudeau, amesema nchi yake haiamini kuwa uchunguzi wa ICC umeidhinishwa au unafaa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Elizabeth Trudeau, amesema nchi yake haiamini kuwa uchunguzi wa ICC umeidhinishwa au unafaa.
"Marekani
imejitolea kweli kweli kwenye kuheshimu sheria za vita, na tuna mfumo
wa kitaifa wa uchunguzi na uwajibikaji ambao unakidhi viwango ya
kimataifa kwa kila hali," alisema Trudeau mara baada ya ripoti ya
Bensouda kuwekwa hadharani.
Naye
msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Kapteni Jeff Davis, alisema
maafisa wa jeshi wanangojea kupata ufafanuzi juu ya madai hayo ya ICC
kabla ya kutoa kauli yao.
Mahakama
hii iliyoanzishwa mwaka 2002 kwa ajili ya kuendesha kesi za uhalifu wa
kivita, uhalifu dhidi ya ubinaadamu na mauaji ya halaiki, inasema
itaamua hivi karibuni ikiwa iendeshe uchunguzi kamili dhidi ya wanajeshi
wa Marekani ama la.
Akiwa
wakati huo mgombea urais kwa tiketi ya Republican, Rais mteule wa
Marekani Donald Trump alisema mapema mwezi huu wa Novemba, kwamba
atarejesha mbinu ya kuadhibu kwa kutumia maji na mbinu nyengine mbaya
zaidi ya hiyo katika kuwalazimisha "magaidi" kutoa taarifa.
Ingawa
Marekani kamwe haijawahi kusaini mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama
hiyo ya ICC, lakini kwa kuwa visa vinavyotajwa vimetendeka katika ardhi
za mataifa mengine, kama vile Afghanistan, Poland, Lithuania na Romania,
ambazo ni wanachama wa ICC, mahakama hiyo inayo nguvu za kisheria
kuvichunguza.
Rais wa
zamani wa Marekani, Bill Clinton alisaini Mkataba wa Roma tarehe 31
Disemba 2000, lakini mrithi wake, George Bush aliikataa sahihi hiyo,
akidai kuwa Wamarekani wasingelitendewa vyema kwenye mahakama hiyo kwa
sababu za kisiasa.DW
SHARE
No comments:
Post a Comment