Mawaziri
wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamejadiliana mjini
Brussels kuhusu mikakati endelevu kufuatia ushindi wa Donald Trump
katika uchaguzi wa Marekani uliomalizika hivi majuzi.
Mawaziri
hao wamezungumzia kuhusu mbinu bora ambazo zitaweza kutumika katika
kufikia makubaliano ya kibiashara, uhusiano na Urusi pamoja na
kuhakikisha dhamira ya Marekani kuelekea Jumuiya ya Kujihami ya NATO
yote hayo yakiwa ni mambo muhimu ambayo kwa sasa yamo katika mizani
kufuatia ushindi wa Trump ambao haukuwa matarajio ya Umoja wa Ulaya.
Mkutano
huo ambao haukuwa rasmi umefanyika mjini Brussels ambapo mawaziri wa
nchi za nje walijadili jukumu la Marekani katika maswala ya kisiasa ya
Umoja wa Ulaya baada ya ushindi wa rais mteule wa Marekani Donald Trump
wiki iliyopita.
Trump
alizungumza mengi juu ya Umoja wa Ulaya wakati wa kampeni zake ambayo
yamezigutusha nchi za umoja huo, kiongozi huyo aligusia kwenye hotuba za
kampeni yake juu ya uwezekano wa Marekani kujiondoa kutoka kwenye
ushirika wa NATO na kuzitaka nchi za Umoja wa Ulaya zijipangie zenyewe
mikakati yake ya usalama huku akitumia wakati mwingi kumsifu rais
Vladimir Puttin wa Urusi.
NATO: Marekani na Ulaya zahitajiana
Mkuu wa
sera za Umoja wa Ulaya Federica Moghrerini amesema "Kuna haja kwa watu
wa Ulaya kuimarisha mikakati ya ulinzi, usalama na ushirikiano licha ya
mabadiliko katika uongozi wa Marekani. Ni muhimu tuzungumze na tufanye
maamuzi sasa, huli lingekuwa angalizo kwa utawala wowote ule. Tuone
utawala ujao utachukua hatua gani katika swala la ulinzi, hili litakuwa
swala muhimu kwa siku za usoni na kwa vyovyote vile swala hili ni muhimu
kwetu."
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini
Wakati
huo huo Bibi Mogherini amemshutumu waziri wa mambo ya nje wa Uingereza
Boris Johnson ambaye hakuhudhuruia kikao hicho, ameifungamnisha hatua
hiyo na kura ya maoni ya mwezi Juni ambapo raia wa Uingereza walipiga
kura ya ndio kwa nchi yao kuweza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya
wenye nchi wanachama 28. Mogherini amesema hatua hiyo ya kujitoa kwenye
umoja huo inaifanya Uingereza kuhitaji zaidi kuungwa mkono na Marekani
katika makubaliano mapya ya kibiashara.
Wizara ya
mambo ya nje ya Uingereza imekanusha shutma hizo na kutetea kutokuwepo
kwa waziri wake wa katika kikao hicho. Taarifa hizo zimesema kuwa
Uingereza haikuona sababu za muhimu za kuhudhuria kikao hicho cha ziada
na kwamba demokrasia imechukua mkondo wake na huku kipindi cha mpito
kikiendelea Uingereza itafanya kazi na serikali ya Marekani ya sasa
pamoja na ile itakayokuja ili mradi maslahi yake yatazingatiwa.
Hii leo
mawaziri hao wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kufikia
msimamo wa pamoja kuhusu Uturuki ambayo imekuwa ikiwaandama wapinzani
wake pamoja na vyombo vya habari. DW
SHARE
No comments:
Post a Comment