Dunia
imepatwa na mshangao mwengine kwenye siasa za kimataifa baada ya Waziri
Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, kujiuzulu kufuatia kushindwa kwenye kura
ya maoni, huku masoko ya hisa yakiporomoka.
Akiwa
ziarani nchini Ugiriki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, ambaye
huenda akawa rais wa taifa hili kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya,
Frank-Walter Steinmeier, anasema nchi yake inatiwa wasiwasi sana na
mgogoro wa kisiasa unaoiandama sasa Italia, akisisitiza kuwa ni lazima
utatuliwe haraka.
"Uamuzi
wa jana nchini Italia, kwa maoni yangu, unaogofya lakini ulikuwa wa
wazi. Umma wa Italia umeyakataa mapendekezo ya mageuzi ya serikali ya
Renzi. Jinsi mambo yanavyopaswa kuwa Italia sasa, yanapaswa kuamuliwa
mjini Rome. Si jambo rahisi baada ya Renzi kutangaza kujiuzulu, lakini
niseme tena kuwa huu ni mzozo wa kiserikali, si mzozo wa dola na si
mwisho wa ulimwengu wa kimagharibi, lakini pia si maendeleo mazuri kwa
mgogoro mzima wa Ulaya, kiujumla," aliwaambia waandishi wa habari mjini
Athens.
Wakati
Steinmeier akijaribu kuzitenganisha athari za mzozo huo na hali halisi
ndani ya bara la Ulaya, masoko ya hisa hayaoni hivyo, kwani muda mchache
tu baada ya Renzi kutangaza uamuzi wake wa kujiuzulu, hisa ziliporomoka
vibaya kwenye masoko ya Ulaya.
Kampeni za Matteo Renzi kutaka madaraka makubwa zaidi kwa serikali kuu hazikukubaliwa na wapigakura.
Mjini
Milan, kulirikodiwa anguko la asilimia mbili, ingawa taarifa za
kushindwa kwa mgombea urais wa mrengo mkali wa kulia nchini Austria
zilikuwa zimeanza kulipa uhai soko hilo.
Uamuzi wa
wapigakura wa Italia umeiporomosha sarafu ya euro hadi kwenye thamani
ya dola 1.056, kikiwa ni kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea tangu
mwezi Machi mwaka jana. Hata hivyo, masoko ya hisa mjini Frankfurt,
Paris na London yanaripotiwa kutikisika kidogo sana asubuhi ya leo, na
baadaye kurudi kwenye nafasi yake ya kawaida.
Hali kama
hii ya masoko ya hisa kutikisika kutokana na maamuzi ya wapigakura,
ilishuhudiwa pia mara mbili mwaka huu - kwanza mwezi Julai baada ya
Waingereza kuamua kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya kwenye kura ya maoni
ya Brexit na kisha mwezi Novemba, baada ya Wamarekani kumpa ushindi
mkubwa mgombea urais wa Republican, Donald Trump.
Rais Mattarella ataka utulivu
Hayo
yakiendelea, mjini Rome kwenyewe, Rais Sergio Mattarella, ametoa wito wa
utulivu, mara tu baada ya Renzi kutangaza kujiuzulu. Shirika la habari
la ANSA linasema rais huyo ambaye asubuhi ya leo alikuwa na mazungumzo
kwa njia ya simu na Renzi, alitaka watu wangojee maamuzi ya kisiasa,
kwani "nchi inahitaji mazingira ya kisiasa kuwa ya utulivu na
kuheshimiana."
Asilimia
59 ya wapiga kura wameukataa mpango wa kuifanyia mabadiliko katiba ya
nchi yao, ambao ulitaka kuyaweka madaraka makubwa kwenye serikali kuu na
ambao ulikuwa ukipigiwa chapuo na Renzi. Idadi ya waliojitokeza kupiga
kura ni asilimia 65.5 na hivyo kulifanya anguko la Renzi kuwa kubwa
zaidi.
Sasa
taifa hilo kubwa kwenye pwani ya Bahari ya Kati linakabiliwa na moja
kati ya mawili: ama chama cha Renzi cha PD kiunge mkono kundi lenye
wajumbe wengi bungeni na kuunda serikali ya mpito, ama kuitishwa kwa
uchaguzi mpya.
Muungano
wa vyama vya upinzani vinavyopingana na Umoja wa Ulaya, M5S,
unashinikiza uchaguzi wa mapema, huku Renzi mwenyewe akiondoa kabisa
uwezekano wa kubakia kuongoza serikali ya mpito kuelekea uchaguzi huo.DW
SHARE
No comments:
Post a Comment