Rais
Mstaafu na Kamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Kugharamia Fursa
ya Elimu Duniani (UN Education Commission on Financing Global
Education Opportunity) Desemba 8, 2016, alikutana na Rais wa Msumbiji,
Mheshimiwa Filipe Nyusi alipomtembelea jijini Maputo, Msumbiji.
Katika
nafasi yake ya Mjumbe Maalum wa Kamisheni hiyo, Rais Mstaafu
amemkabidhi Rais Filipe Nyusi Ripoti ya Kamisheni hiyo yenye
mapendekezo ya namna Dunia inavyoweza kukabili janga la Elimu kwa
kuwekeza katika Mpango wa Kizazi cha Elimu (A Learning Generation).
Mpango huo unalenga kuleta mapinduzi makubwa ya Elimu katika nchi
zinazoendelea ndani ya Kizazi Kimoja (miaka 30). Azma kuu ya Mpongo huo
ni kuwezesha ifikapo mwaka 2040, watoto wote kote duniani wawe wanapata
elimu iliyo sawa, na kwa kiwango cha ubora unaolingana dunia nzima.
Rais
Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi Mhe. Rais Filipe Nyusi
ripoti ya Kamisheni ya UN ya Elimu jijini Maputo, Msumbiji.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, kwa sasa, hali ya elimu katika nchi zinazoendelea
inalingana na ile ambayo nchi zinazoendelea zilikuwapo miaka 70
iliyopita. Aidha, ripoti inasisitiza kuwa, ikiwa nchi zinazoendelea
zitaendelea kwa kasi ya sasa, itazichukua nchi hizo kati ya miaka 90 na
110 kufikia viwango vya sasa vya nchi zilizoendelea.
Aidha,
ripoti inatahadharisha kuwa takribani ajira bilioni 2 zitakufa ifikapo
mwaka 2050 kutokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo asilimia 70 ya
kazi hizo ziko katika nchi zinazoendelea. Hivyo, nchi zinazoendelea
zinapaswa kuangalia upya aina ya elimu na stadi zinazotolewa ili
kuendana na wakati ujao.
Rais
Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimpitisha Mhe. Rais Filipe Nyusi
katika ripoti ya Kamisheni ya Elimu kuhusu Mapendekezo Mahsusi kwa nchi
ya Msumbiji.
Kwa
ajili hiyo, Kamisheni inapendekeza njia mpya na bora za kufanya mageuzi
katika elimu ikiwemo kuongeza usimamizi, kupanua fursa, kuingiza ubinifu
na teknolojia na kuongeza uwekezaji katika elimu kwa kushawishi
ushiriki wa Jumuiya ya Kimataifa na Sekta Binafsi. Iwapo mapendekezo
hayo yatatekelezwa, nchi zinazoendelea zinaweza kufidia pengo hilo ndani
ya miaka 30 ijayo. Rais Mstaafu ameiomba Msumbiji kujiunga na Mpango
huo.
Kwa
upande wake, Rais Nyusi amepokea kwa furaha taarifa hiyo na kuelezea nia
na dhamira ya nchi yake ya kujiunga na Mpango wa Kizazi cha Elimu.
Kufuatia mazungumzo yao, mapema baadae Rais Mstaafu alikutana na Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Adriano Maleane, Naibu Waziri wa Elimu ya
Juu, Sayansi na Elimu ya Fundi Mhe. Leda Hugo na Naibu Waziri wa Elimu
Mhe. Armingo Ngunga kujadili mapendekezo mahsusi ya Kamisheni kwa nchi
ya Msumbiji.
Rais
Mstaafu na Mjumbe wa Kamisheni ya Elimu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa
katika mazungumzo na Mhe. Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, jijini Maputo.
Ziara
ya Rais Mstaafu itamfikisha katika nchi 14 barani Afrika ambapo
zimechaguliwa katika awamu ya kwanza ya mpango huo. Tayari
amekwishazitembelea nchi za Uganda, Malawi, Ethiopia na Msumbiji.na
kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa nchi hizo.
Mhe.
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete katika mkutano wake na Waziei wa Fedha na
Mipango, Naibu Waziri wa Elimu, Naibu Waziri wa Elimu ya Juu wa Serikali
ya Msumbiji.
Rais
Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na Waziri wa
Fedha na Mipango, Naibu Waziri wa Elimu, Naibu Waziri wa Elimu ya Juu wa
Msumbiji.
SHARE
No comments:
Post a Comment