WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itazifutia usajili Taasisi zote
zisizokuwa za Kiserikali (NGO’s) zilizoko kwenye Tarafa ya Loliondo
zinazofanyakazi kinyume na katiba zake na sheria ya nchi ambapo ametoa
miezi sita zijitathimini kama zinafanya kazi ya kuhudumia jamii au la.
Pia
ameahidi kumpeleka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
katika Taraha hiyo ya Loliondo kwa lengo la kuzifanyia ukaguzi NGO hizo
ili kubaini kiasi cha fedha wanazopata kama zinalingana na matokeo ya
kazi za kijamii inazofanya katika Tarafa hiyo.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Desemba 15, 2016) wakati
akizungumza na Wakurugenzi wa NGO na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Ngorongoro kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya
kikazi mkoani Arusha.
Amesema
NGO nyingi zimekuwa zikipata bajeti kubwa ya fedha lakini masuala ya
maendeleo wanayoyafanya katika eneo hilo hayalingani na bajeti halisi
wanazopata.”Loliondo pekee kuna NGO zaidi ya 30 ila zilizokuwa ‘active’
ni 15 tu kuna nini Loliondo? Na baadhi yake zinafanya kazi ya kuchochea
eneo hili lisiwe na amani,”.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa “watu wote wanaoshirikiana na NGO hizo zinazochafua
taswira ya nchi tutawashughulikia. Mnawavalisha watoto kandambili
zilizotobona na miguu michafu kisha mnawapiga picha mnazituma kwenye
mitandao na kusema umasikini wa Tanzania ndio huo. Hatutawavumilia watu
wa namna hii,”
amesisitiza.
Amesema
NGO nyingi zimekuwa zikilalamikiwa kutokana na kufanya kazi kinyume na
mikataba yake ya usajili na miongoni mwa NGO hizo ni pamoja na PWC
inayopata sh. bilioni 2.5 kwa mwaka, UCRT inayopata sh. bilioni 1.5 kwa
mwaka, Oxfarm Tanzania inayopata sh. bilioni 1.7 kwa mwaka.
“Nitafuatilia
kwa karibu kuona kazi wanazozifanya kwani zinapata fedha nyingi kwa
mwaka. Lazima tujenge nidhamu kwa wote wanaopata fedha kwa lengo la
kuisaidia jamii. Wote wanaojihusisha na shughuli nje ya mikataba yao
wabadilike ndani ya miezi sita. Wafuate kanuni, sheria na taratibu za
nchi,” amesema.
Amesema
Serikali haiwezi kufanya kazi bila ya wadau ila haiitaji wadau
wanaofanya mambo kinyume cha taratibu, ambapo amezitaka NGO hizo
kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA) ili ziweze
kutambulika kisheria na ofisi zake kujulikana badala ya hivi sasa kuwa
na ofisi za mifukoni.
Awali,
Waziri Mkuu alizungumzia na wananchi wa kijiji cha Ololosokwan ambapo
alisema mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Tarafa la Loliondo na
wawekezaji unaolikabili eneo hilo Waziri Mkuu mesema Serikali
itahakikisha mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu unamalizika haraka.
Aidha,
amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kukutana na uongozi
wa wilaya ya Ngorongoro na kamati ya wananchi iliyoundwa kwa ajili ya
kuboresha uhifadhi ili kumaliza mgogoro huo na kisha kumpelekea taarifa.
“Haiwezekani
Waziri Mkuu aje kumaliza mgogoro wa ardhi Loliondo wakati kuna viongozi
hapa. Mimi nimemuagiza Mkuu wa mkoa aje akutane na wawekezaji na
wananchi ili kuzungumza na kuupatia ufumbuzi mgogoro huu na
atakayeshindwa ndiye nitakayemshughulikia,” amesema.
Amesema
Serikali itahakikisha migogoro ya ardhi inamalizika nchini ili
kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu. “Naomba
tushirikiane katika kutatua changamoto hii ya migogoro ya ardhi kwani
suala hili limeahidiwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM,”.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wananchi
kuingiza ng’ombe kiholela kutoka nje ya nchi kwa kuwa kitendo hicho
kinachangia kuwepo kwa migogoro ya ardhi.
Katika
kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa wilaya
hiyo, Bw. Rashid Taka kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama
ya wilaya hiyo kuimarisha ulinzi katika mipaka kwa kuongeza doria ili
kudhibiti uingiaji holela wa mifugo.
Naye
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema eneo la
Loliondo ni muhimu sana kwa ajili ya ikolojia ya wanyama pamoja na maji
kwani hifadhi ya Serengeti inategemea zaidi eneo hilo.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment