Na Greyson Mwase, Manyara
Wananchi katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamepongeza
kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua ya Rafiki Power
iliyopo chini ya kampuni tanzu ya E.ON ya Ujerumani, kwa kuwapatia
huduma ya umeme iliyopelekea kukua kwa kasi ya maendeleo katika wilaya
hiyo.
Waliyasema hayo leo katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu
kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika miradi ya umeme mkoani Manyara
yenye lengo la kuangalia utekelezaji wa miradi ya umeme, changamoto
zake na kutoa ushauri wa kitaalam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake katika kijiji cha Komolo kilichopo
wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Thadeo Bura ambaye ni mmiliki wa duka
la vifaa vidogo vya umeme jua na bidhaa nyingine, alisema kabla ya
kampuni ya Rafiki Power kuwekeza katika kijiji hicho maisha yalikuwa ni
magumu kwa kuwa hakukua na nishati ya kuwawezesha kuanzisha miradi
midogo midogo.
Alisema mara baada ya kupata umeme kupitia kampuni ya Rafiki Power,
ameweza kuanzisha duka kwa ajili ya vifaa vidogo vya umeme jua, bidhaa
nyingine na kutoa huduma nyingine kwa wanakijiji wenzake.
Alisema huduma ya umeme imewekwa kwenye baadhi ya shule na hospitali hivyo kuboresha huduma za jamii.
Naye Joseph Hango ambaye ni mmiliki wa saluni ya kunyoa nywele
aliongeza kuwa uwepo wa nishati ya umeme kupitia kampuni ya Rafiki Power
umepelekea kuongezeka kwa kipato kutokana na idadi ya wateja
kuongezeka.
Aliiomba kampuni hiyo kuendelea na juhudi za kusambaza umeme katika
maeneo mengi ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme ili kukuza uchumi wa
wilaya na mkoa kwa ujumla.
Wakati huohuo, akizungumza katika ziara hiyo Meneja Mkuu wa Kampuni
ya Rafiki Power, Joanis Holzigel alisema kuwa kampuni yake inatarajia
kuongeza uzalishaji wa umeme ambapo kaya 20,000 nchi nzima zinatarajiwa
kunufaika na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2022.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa nishati ya umeme katika uchumi wa
viwanda utakaopelekea nchi ya Tanzania kuwa kwenye orodha ya nchi za
kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, kampuni yake imeweka mipango ya muda
mfupi na muda mrefu ambapo inatarajia kufikia wateja 20,000 ifikapo
mwaka 2022.
Akitaja miradi inayotekelezwa na kampuni yake, Meneja Holzigel
alisema katika mkoa wa Arusha kampuni yake ina miradi minne katika
maeneo ya Digodigo, Soitsambu, Ololosokowani, na Malambo yaliyopo
wilayani Ngorongoro na miradi mingine miwili iliyopo katika maeneo ya
Itaswi na Kwamtoro wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.
Aliongeza kuwa, mradi mwingine mmoja unaotekelezwa na kampuni hiyo ni wa Komolo/Temeke, uliopo Simanjiro mkoani Manyara.
Meneja
Mkuu wa kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua ya Rafiki
Power, Joanis Holzigel (kushoto) akibadilishana mawazo na Mtaalam wa
Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Emillian
Nyanda (kulia) katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka
Wizarani katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi
wa miradi ya umeme.
Mmiliki wa kioski kilichonufaika na huduma ya umeme jua kupitia
kampuni ya Rafiki Power, Thadeo Bura (kushoto) akielezea manufaa ya
mradi wake katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya
Nishati na Madini katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili
ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
Moja ya kioski kilichonufaika na huduma ya umeme jua kupitia kampuni
ya Rafiki Power kilichopo katika kijiji cha Komolo wilayani Simanjiro
mkoani Manyara.
Mmiliki wa mghahawa wa chakula ambaye ni mmoja wa wanufaika wa huduma
ya umeme jua kupitia kampuni ya Rafiki Power akionesha friji inayotumia
nishati hiyo katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara
ya Nishati na Madini katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa
ajili ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
Mmiliki wa kioski kilichonufaika na huduma ya umeme jua kupitia
kampuni ya Rafiki Power, Thadeo Bura akielezea matumizi ya compressor
inayotumia nishati ya jua kwa matumizi mbalimbali, katika ziara ya
wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika
wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya
umeme.
SHARE
No comments:
Post a Comment