Mpambano
wa
kukata
na shoka
Julian Msacky
“IRAN imesema itashambulia Israel na imelisema hili waziwazi.
Inataka ivamie Mashariki ya Kati, imetishia Ulaya, imetishia nchi za Magharibi
na imetishia dunia”
Hii ni kauli ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Nyetanyahu
wakati akizungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May mjini London.
Nyetanyahu hakuishia hapo bali aliendelea kusema,
“ninazungumza na wewe (May) kuhusu hili ili hatua zichukuliwe dhidi ya Iran”.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Waziri Mkuu huyo wa Israel
alikwenda mbali zaidi na kutaka mataifa “yashikamane”na kuomba Rais wa
Marekani, Donald Trump aingilie kati.
Ifahamike kuwa tangu Rais Trump aingie madarakani kumekuwa na
jitihada za chini kwa chini za Israel kutaka kupanua makazi yake.
Kwa mfano, hivi sasa inafikiria kuanzisha makazi mapya 6000
ingawa haifamiki yatatoka eneo la Palestina au la. Huu ni mgogoro mwingine.
Wakati ikifanya hivyo Nyetanyahu ameendelea kuzunguka maeneo
mbalimbali ili kutafuta uungwaji wa masuala yake.
Miaka ya hivi karibuni alitembelea pia Afrika na kuahidi
misaada mbalimbali na uwekezaji katika mataifa kadhaa.
Ikumbukwe pia Waziri Mkuu huyo wa Israel ameomba Iran izidi
kuwekewa vikwazo na hili linaonekana kuungwa mkono na Serikali ya Trump.
Hofu iliyopo sasa ni kuwa endapo mvutano huu utaendelea ipo
hatari ya dunia kushuhudia tena mapigano zaidi eneo la Mashariki ya Kati.
Ni kwa nini Iran inaandamwa? Ni baada ya kufanya jaribio la
kurusha kombora la masafa marefu jambo ambalo limeishtua Marekani pamoja na Israel.
Kwa hatua hiyo, Trump alisema lazima iangaliwe kwa umakini
mkubwa na hicho ndicho anachohubiri Netanyahu.
Itakumbukwa kuwa wakati wa uongozi wa Rais Barack Obama
uhusiano kati ya Rais wa Iran, Hassan Rouhani ulikuwa wa kutia matumaini.
Hata hivyo, uhasama umeanza kurejea tena kati ya nchi za
magharibi na Iran kama ilivyokuwa enzi za Rais Mahmoud Ahmadinejad.
Je, mpambano huu wa kukata na shoka kati ya mataifa hayo
utaleta tija eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla? Kama la, nini
kifanyike?
Ugomvi uliopo ni wa silaha za nyuklia. Ugomvi huu
ulisababisha baadhi ya viongozi kuondoka madarakani au kufa.
Kwa msingi huo kitisho cha usalama ndicho kinachosababisha
viongozi wa mataifa hayo kushikana sharubu.
Iran inaambiwa marufuku kujihusisha na urutubishaji wa silaha
za nyuklia kwa ni hatari kwa usalama wa dunia.
Hata hivyo, inajitetea kuwa nyuklia ni kwa mtumizi salama na
si vinginevyo, lakini Marekani inasema hiyo ni danganya toto.
Swali ni nani mkweli? Au ni nani kati ya Israel, Marekani,
Iran au Korea Kaskazini asiyemiliki silaha hatari?
Tunadhani mvutano uliopo kati ya mataifa hayo utamalizika kwa
kuzingatia mikataba iliyopo kuhusu silaha hizo.
Kwa maana nyingine ni kuwa busara lazima itumike kukabiliana
na silaha za nyuklia bila kuhatarisha usalama wa n chi nyingine.
Hii ina maana kuwa mapambano yanayoendelea sasa kati ya
mataifa hayo hayana afya kwa nchi moja bali waathirika ni wengi.
Tuliona wakati majasusi wa Marekani wakichunguza silaha
zilizoitwa na maangamizi nchini Iraq ni nini kilitokea.
Hadi Saddam Hussein anatiwa kitanzini hakuna silaha za
maangamizi zilizopatikana nchini humo.
Ni kwa msingi huo ninashauri kuwa mikataba iliyopo kuhusu
silaha za nyuklia ikiheshimiwa itasaidia zaidi kuliko kutanguliza nguvu na
jazba.
Kutanguliza mabavu kuna athari nyingi, ikiwemo kuvamia nchi
na kusababisha vifo na uharibifu wa mali mbalimbali.
Ndiyo kusema Marekani na Israel ni vizuri zikajifunza kupitia
matukio yaliyopita hata kama agenda ya uvamizi ni nyingine.
Yaliyotokea Iraq tumeyaona. Yaliyotokea Libya tumeyaona. Nchi
hizi zimegeuka magofu kutokana na kuchakazwa na vita.
Mataifa makubwa yasifikishe tena nchi nyingine huko. Angalia
Syria watu wanavyochinjana kama kuku.
Ni nani yupo nyuma ya mgogoro huo? Ni nani anafaidika na damu
zinazomwagika? Ni nani huyo?
Hivi sasa Iran na Korea Kaskazini ndizo zinazoonekana kama tishio
kwa usalama wa duniani.
Ni ukweli usiopingika kuwa kila nchi inatakiwa ihakikishe
inatumia vizuri silaha ilizonazo na si vinginevyo.
Kama alivyowahi kusema msomi mmoja wa Canada kuwa njia
alizotumia Rais George Bush kupambana na ugaidi ni mbaya.
Alifananisha njia hiyo sawa na kuzalisha zaidi viranga na
ndivyo ilivyo pia mapambano dhidi ya silaha za nyuklia.
0718981221, msackyj@yahoo.co.uk
SHARE
No comments:
Post a Comment