Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wanafunzi
wa shule za Msingi mkoani hapa wametakiwa kuwa makini na kutokuwa na
tamaa ya kuomba “lift” au kupewa chipsi au kushawishiwa kwa namna yoyote
ile na watu ambao hawafahamiana nao pindi wanapokwenda shule au
wanaporudi majumbani kwao.
Hayo
yalielezwa na Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa
Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu wakati alipokuwa akitoa elimu ya
Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia katika vipengele vya ubakaji,
ulawiti na vipigo kwa wanafunzi 63 wa Elimu Maalum kitengo cha viziwi
katika shule ya Msingi Meru iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.
Alisema
baadhi ya wanafunzi wanajikuta wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa
kijinsia kama ubakaji na ulawiti baada ya ushawishi mdogo mdogo kwa
kupewa lift, kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi na
kadhalika.
Mkuu
wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa
Polisi Happyness Temu akiwa katika picha ya pamoja na Walimu na
Wanafunzi wa shule ya Msingi Meru kitengo cha elimu maalum.
“Baadhi
ya vitu ambavyo vinasababisha ushawishi na hatimaye wanafunzi
wanafanyiwa ukatili wa kubakwa au kulawitiwa bila hata wao wenyewe
kudhani kama hali hiyo inaweza kutokea ni pamoja na lift za magari au
pikipiki, kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi.”. Alisema Mkuu
huyo wa Dawati Happyness Temu.
“Sio
watu wote wana nia mbaya katika utoaji wa “lift” ila kuna wachache si
wema na hawawezi kujulikana yupi mwema na yupi mbaya hivyo wazazi
wanatakiwa wawafuatilie kwa ukaribu na kuwaeleza uhalisia wa mabadiliko
ya maisha watoto wao ili kuwaepusha na watu wenye nia mbaya dhidi yao”.
Aliongeza Mkaguzi huyo wa Polisi Happyness Temu.
Wakiongea
kwa lugha ya ishara na kutafsiriwa na walimu wa shule hiyo Veila Wilson
na John Maukiri, baadhi ya wanafunzi walionyesha kufurahia elimu hiyo
na kupata ufahamu juu ya hatua wanazoweza kuchukua katika kujiepusha na
vitendo vya ukatili na unyanyasaji na pia walifahamu hatua za kuchukua
mara watakapofanyiwa ukatili wa aina yoyote.
Mwalimu
Veira Wilson katikati akiwa anaongea kwa ishara wakati anawatafsiria
wanafunzi wa elimu maalum (Viziwi) uelimishaji uliokuwa unatolewa na
Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa
Polisi Happyness Temu ambaye yupo kulia kwake na kushoto kwake ni
Mwalimu John Maukiri .
Baadhi
ya wanafunzi hao walikiri kufanyiwa hasa ukatili wa vipigo majumbani
mwao huku mkuu huyo wa Dawati kuahidi kuwasilikiza walalamikaji na
kufuatilia kwa ukaribu kwa nia ya kukomesha tabia hiyo.
Naye
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambayo inamchanganyiko wa wanafunzi wa elimu
ya kawaida na elimu maalum Bw.Musa Luambano, alilishukuru Jeshi la
Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto kwa kutoa elimu
hiyo kwa wanafunzi hao ambayo itawasaidia kujua hatua za kuchukua pindi
wanapofanyiwa ukatili lakini pia wao watakuwa mabalozi kwa wengine
katika kuwaelimisha.
Alisema
kitendo cha Jeshi la Polisi kufika katika shule hiyo na kutoa elimu kwa
wanafunzi wa kitengo cha elimu maalum ni ishara ya hatua nzuri katika
kuongeza ushirikiano kati ya Jeshi hilo na wanafunzi wa aina hiyo na
kutoa wito kwa ofisi mbalimbali kupeleka watumishi wao ili waweze
kujifunza elimu ya lugha ishara ambayo itaweza kuwasaidia katika
kuhudumia makundi yenye uhitaji maalum kama vile viziwi.
Mkuu
wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa
Polisi Happyness Temu akitoa somo juu ya ukatili na unyanyasaji wa
jinsia kwa wanafunzi wa elimu maalum katika shule ya Msingi Meru iliyopo
halmashauri ya jiji la Arusha.
Mkuu
wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa
Polisi Happyness Temu akiagana na wanafunzi wa shule ya Msingi Meru
kitengo maalum mara baada ya kuwaelimisha juu ya ukatili na unyanyasaji
wa kijinsia.
SHARE
No comments:
Post a Comment