MKAKATI wa utawala wa Trump kupambana na IS
hautofautiani sana na wa Obama. Na hilo halitazamiwi kubadilika wakati
wa mkutano wa kimataifa kuhusu suala hilo.
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka muungano wa kimataifa unaopambana
dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS wanakutana mjini
Washington baadae leo kujadili juhudi za kupambana na kundi hilo la
kigaidi. Mkutano huo unatoa fursa kuonyesha hatua zilizopigwa katika
utekelezaji wa mmoja ya ahadi za rais Donald Trump - ambayo ni
kulisambaratisha kabisaa kundi hilo.Trump amewaagiza Majenerali wake kubuni mkakati wa kusambaratisha kile kinachoitwa khilafa ya kundi hilo, na washirika wa muungano dhidi ya IS wanataka kujua zaidi katika mkutano huo wa siku moja. Mkutano huo unaofanyika katika wizara ya mambo ya kigeni utamruhusu waziri msiri wa mambo ya kigeni Rex Tillerson kujitoa katika kivuli cha Trump, na kuweka mamlaka yake katika upande wa diplomasia wa juhudi hizo za pamoja.
Lakini mpango wa Trump wa kupunguza asilimia 28 kwenye bajeti ya diplomasia na misaada ya kigeni ya wizara hiyo unamaamisha kuwepo na rasilimali ndogo tu kwa ajili ya utulivu wa baada ya migogoro -- pendekezo ambalo limezusha wasiwasi. Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanataraji Washington itathibitisha tena dhamira yake kwa mpango wake wa kurudisha amani katika kanda hiyo baada ya ushindi katika uwanja wa vita.
Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alipokutana na Rais Trump katika ikulu ya White House Machi 20, 2016.
'Mwisho wa IS unakaribia'Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alikuwa mjini Washington siku chache tu kabla ya mazungumzo hayo, na alisema ushindi dhidi ya IS uko karibu ikiwa washirika watashikana pamoja. "Tumetoka safari ndefu sana tangu miaka miwili iliopita. Hakuna aliedhani tungekuwa Mosul hii leo. Na tumekomboa sehemu kubwa ya Mosul. Na sasa vikosi vyetu vinasonga mbele kwa ujasiri mkubwa," alisema Abadi wakati wa ziara yake Washington.
Muda mfupi baada ya kuapishwa mwishoni mwa mwezi Januari, Trump aliipa wizara ya ulinzi Pentagon muda wa siku 30 kupitia upya hatua zilizopigwa katika mapambano dhidi ya IS na kubuni mpango mpana wa kulifuta kabisaa kundi hilo. Akiwa mgombea Trump alikosoa kasi ya mtangulizi wake Barack Obama katika mapambano dhidi ya IS, na alidai kuwa na mkakati wa siri wa kuimaliza kabisaa.
Hakuwahi kutoa ufafanuzi juu y mkakati wake huo na mpaka ameendelea kutumia mkakati wa Obama ambao unajikita zaidi katika kufanya uchunguzi na mashambulizi ya kulenga shabaha yanayoongozwa na vikosi vya Marekani kwenye ngome za wapiaganaji wa IS, huku wakitoa mafunzo kwa vikosi vya ndani kuendesha mashambulizi ya ardhini na kushikilia maeneo yaliotekwa.
Mwezi uliopita Pentagon ilikabidhi muswada wa awali wa mpango wake uliorekebishwa wa kupambana dhidi ya IS. Msemaji wa Pentagon Jeff Davis alisema waraka huo utaunda msingi wa mazungumzo ya leo, na maoni kutoka kwa washirika yatajumlishwa.
SHARE
No comments:
Post a Comment