Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na
Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na CUTS International Geneva kupitia
ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo Sweden (SIDA), wamezindua
Ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata
mazao ya kilimo na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama jinsi
ulivyo Mpango wa Serikali kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21.
Akizungumzia ripoti hiyo,
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dkt. Tausi Mbaga Kida alisema, ripoti hiyo
imeonyesha kuwa, kama viwanda vya ndani vitaboreshwa vitawezesha kuwa na
uwezo wa kuchakata mazao mengi ya kilimo yanayozalishwa na wakulima
zaidi ya asilimia 75 ya watanzania.
Pia itasaidia kuongeza ajira,
kuwahakikishia wakulima soko la uhakika wa mazao yao, na serikali
kujiongezea vyanzo vipya vya mapato kutokana na bidhaa zitakazouzwa
baada ya usindikaji na kwa kufanya hivyo, uchumi wa wakulima,
wasindikaji, wafanyabiashara na wa Taifa kwa ujumla utaongezeka.
“Utafiti umeonyesha ili uweze
kunufaika na kilimo lazima tuweze kuongeza thamani katika mazao yetu na
hilo tutaweza kulipata pale ambapo tutakuwa na viwanda vyetu ambavyo
vitaweza kuchakata mazao yetu katika ubora na kuweza kuwafikia walaji
sehemu mbalimbali. Kikubwa katika hilo ni jinsi gani viwanda vya
usindikaji, vikubwa na vidogo, vitaweza kuwa karibu na wakulima,” alisema Dk. Kida.
Akisoma hotuba ya uzinduzi wa
Ripoti hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji (Viwanda na Biashara), Dr. Adelhem Meru, Kaimu Mkurugenzi wa
Kitengo cha Masoko na Utafiti wa wizara hio, Bwana Leo Lyayuka, alisema
Serikali inafahamu kuwa katika safari ya kuelekea katika nchi ya viwanda
ni muhimu viwanda vyetu viwe na uwezo wa kuchakata mazao ya kilimo ili
kuyaongezea thamani.
Aidha alitoa rai kwa Shirika la
kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) kushirikiana na Serikali na wadau
wengine wa sekta ya usindikaji mazao ya kilimo katika kubuni mashine
zenye uwezo wa kuchakata mazao mbalimbali na kuyauza ndani na nje ya
nchi katika thamani kubwa zaidi.
Ndugu Lyayuka alisema pia msingi
mzima katika utafiti uliopo kwenye Ripoti hio ni kuoanisha changamoto
ambazo zipo katika mabadiliko ya tabia nchi na jinsi gani zinaweza
zikaathiri uzalishaji na usalama wa chakula, biashara, na jitihada za
kuendeleza viwanda vya usindikaji.
“Ni muhimu sana kwa sera zetu
za viwanda na kilimo kuoana ili kuchagiza maendeleo haya ya sekta ya
usindikaji, huku maswala mazima ya mabadiliko ya tabia nchi yakitiliwa
mkazo kuepukana na athari zinazoweza kuletwa nazo.”
Kwa upande wa mmoja wa watafiti,
Ndugu Solomon Baregu alisema utafiti huo ni muhimu kwa Tanzania na kama
ukifanyiwa kazi kikamilifu unaweza kuisaidia nchi kuingia katika uchumi
wa viwanda.
“Utafiti huu ni muhimu na
umekuja wakati muafaka ambapo Serikali inatilia mkazo sana suala la
kujenga Tanzania ya viwanda. Sekta ya kilimo ni sekta mama ambayo kwa
kiasi kikubwa inaweza kuchochea ukuaji wa viwanda,” alisema Bwana Baregu.
Bwana Baregu aliongeza kuwa “Ni
muhimu sana Serikali kufikiria sasa kuja na sera mahususi itayoweza
kutambua ukuzaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo
(Agro-Industrial Development Policy) huku ikitilia maanani mabadiliko ya
tabia ya nchi na athari zake katika biashara, usalama wa chakula na
uchakataji mazao ya kilimo.”
SHARE
No comments:
Post a Comment