TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama cha Wanahabari Wanawake –TAMWA kinavipongeza
vyombo vya habari hapa nchini kwa ushirikiano wa hali na mali katika kutoa taarifa
za kuelimisha umma juu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele
chake kilikuwa ni tarehe 8 Machi, 2017 ulimwenguni kote.
Vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika Siku
muhimu ya Wanawake Duniani kwani vilihakikisha vinatoa taarifa za kuhabarisha,
kuhamasisha na kuelimisha taifa ambapo kumekuwa na mwamko wa jamii kutambua
thamani ya mwanamke hapa nchini tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Siku ya Wanawake duniani kupitia vyombo vya habari
mwaka huu wa 2017 ikiwa na kauli mbiu iliyosema “Tanzania
ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi” imewafanya wanawake kupata mwamko
katika siku yao hiyo na kukaa pamoja ili kujadili namna wanavyoweza kuondokana
na changamoto wanazokumbana nazo hasa katika kufanya kazi za kuleta maendeleo
kwao, familia na taifa kwa ujumla.
Kuwa vyombo vya habari vina nguvu ya kuleta mabadiliko
chanya, vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ambayo imekuza uelewa
miongoni mwa jamii hasa kwa wanawake wametambua umuhimu
wa kuhamasishana ndani ya jamii, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Taasisi za
Serikali, Vyama vya Siasa, Wabia wa Maendeleo na wadau wengine hapa Tanzania ili
kuongeza wigo wa fursa za kiuchumi kwa wanawake na kuwawezesha kushiriki na
kunufaika na hatua za maendeleo.
Aidha; TAMWA inajivunia nguvu kubwa ya vyombo vya
habari hapa nchini kwani imekuwa ikitoa mafunzo kwa waandishi mbalimbali wa
habari ambapo Mpaka sasa zaidi ya waandishi 500 wameongezewa uelewa wa jinsi ya kuandika habari za uchunguzi na zenye
kuleta mbabadiliko ya kimaendeleo, kuleta usawa na kupinga ukatili wa kijinsia
hapa Tanzania ambapo tunaamini na hao wamekuwa chachu kwa wengine.
Vuguvugu la Siku ya Wanawake lilianza
mwanzoni mwa miaka ya 1900 kupitia kwa wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda
nchini Marekani walioandamana kupinga mazingira duni ya kazi zao, walilalamikia
ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika
ajira. Kutokana na hali hiyo, Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1945; tarehe 8
Machi ikaridhiwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.
Edda
Sanga
Mkurugenzi
Mtendaji
SHARE
No comments:
Post a Comment