Julian Msacky
WAKATI wa uhai wake, Mwalimu Julius Nyerere alitupa somo
muhimu kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne.
Uongozi bora, siasa safi, ardhi na watu. Huu ni mtaji muhimu
kwa nchi yoyote inayotaka kupiga hatua kimaendeleo.
Kwa nchi yangu Tanzania Mungu ameijalia ardhi na watu. Vitu hivi
viwili vipo vya kutosha, lakini vinatumika inavyotakiwa?
Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Ni kwa namna gani vinatumika vizuri kuharakisha maendeleo ya nchi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
Ni kwa namna gani vinatumika vizuri kuharakisha maendeleo ya nchi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
Tuelewe vipi kwa mfano tunapoambiwa uchumi wetu umekuwa
lakini neema hiyo haionekani kwa wananchi?.
Ni baba gani anakuwa tajiri (uchumi mzuri), lakini familia
yake inaishi maisha ya kubangaiza asubuhi hadi jioni?
Tunadhani uchumi unapokua unatakiwi uonekane kwa wananchi wa
kawaida lakini kama si hivyo lazima yawepo maswali.
Mwananchi asiyeweza kumudu milo mitatu kwa siku utamwambia
uchumi wa nchi umekua wakati lishe inamshinda.
Kwenye ardhi yetu tunaitumia ipasavyo? Tunaitumia vizuri kwa
ajili ya kilimo bora kama tunavyoimba au imejikalia tu?
Kama tungetumia ardhi yetu vizuri leo hii habari za ukosefu
wa chakula ingetoka wapi? Habari ya njaa ingetoka wapi?
Binafsi naamini ardhi yetu haijatumika vizuri ndiyo maana
wafugaji na wakulima wanavimbiana kila kukicha.
Kwa ardhi tuliyonayo tunashindwa nini kuipangilia vizuri ili
wafugaji wafuge kwa amani na utulivu ndani ya nchi yao?
Ukubwa wa ardhi uliopo ni aibu kuona wakulima na wafugaji
wanashikana mashati kwa sababu hii na ile.
Hili ni eneo ambalo hajaweza kulitumia vizuri kiasi kwamba
watu wanajazana mijini kwa sababu ya ubunifu mdogo.
Kwa miaka mingi sasa tumeshindwa kuifanya ardhi yetu
kuwakomboa wananchi kiuchumi kwa sababu haijapimwa.
Tatizo ni kwamba uongozi bora haupo. Tunapokosa uongozi bora
maana yake mambo yetu yanafanyika ovyo ovyo.
Yanakuwa hivyo kwasababu viongozi hawajitambui. Hawajui
majukumu yao kwa wananchi ni yapi. Kwa hili kuna ombwe.
Matokeo yake idara nyingine zinajiendesha kwa kulegalega na
kimazoea na hivyo kujishindwa kusonga mbele.
Kwa mfano, ngazi ya halmashauri zetu hiki kinachoitwa uongozi
bora upo kwa jina au tumekuwa maharibi wa kuzunguka ofisini?
Ni ofisa gani wa halmashauri leo hii anajua mkulima analima
kitu gani? Ni ofisa gani anajua mfugaji anafuga nini na kwa vipi?
Tembelea wananchi uone wanavyopata hasara kwa kukosa wa kumwelekeza
alime nini kwenye eneo lake.
Ardhi iliyotakiwa kulima muhogo analima chai. Ardhi
iliyotakiwa kulima viazi analima katani. Ni tatizo kweli kweli.
Nenda kwa wafugaji. Wanapoteza mifugo kwa magonjwa
yanayoepukika kwa vile tu amekosa kuelekezwa tiba ni nini.
Ndiko tulikofikia kama nchi wakati tunatamani kuwa nchi ya
viwanda. Kwa hali hii itawezekana kweli?
Mahali ambapo wakulima wanalima wasichoweza kuvuna na kufuga
wasichoweza kupata. Hii ni shida.
Tunahitaji uongozi bora ili kutuondoa hapa tulipo. Uongozi
bora haupimwi kwa matamko au lugha kali majukwaani.
Uongozi bora hupima kwa namna watendaji wanavyotimiza
majukumu yao kama sheria na taratibu za kazi zilivyo.
Ikumbukwe mahali pasipo na uongozi bora (good leadership)
hata ashuke malaika ni vigumu kupata maendeleo.
Kuna umuhimu suala hili likasisitizwa kuanzia shuleni ili
taifa liondokane na ukame wa viongozi bora.
Tukiwa na viongozi bora kilimo kitakwenda vizuri, wafugaji
watafuga vizuri, elimu itakuwa bora na mambo mengine mengi.
Ili yote hayo yawezekane ni lazima tuwe na siasa safi. Kwa
maana ya kukubali mawazo tofauti ili kusonga mbele.
Kupitia siasa tutashauriwa namna gani tuunganishe nguvu
kukabiliana na changamoto zilizopo.
Ni muhimu kwa sababu haijawahi kutokea mawazo ya wateule
wachache yakaleta rutuba katikati ya kundi la watu.
Ndiyo maana hata Yesu aliwashirikisha wanafunzi wake ili
kutengeneza fikra pana kwa lengo la kuinjilisha vizuri.
SHARE
No comments:
Post a Comment