Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
Na Hassan Silayo-MAELEZO
Kuanzia
02 Machi, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli alianza ziara ya kikazi ya siku 4 katika Mikoa ya Pwani, Lindi
na Mtwara iliyolenga kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na
kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Ziara
hiyo kwa kiasi kikubwa imeonesha dira na mwelekeo wa serikali ya awamu
ya tano hasa katika utekelezaji wa miradi inayolenga kuwaletea wananchi
maendeleo bila kujali Imani,kabila na itikadi za vyama vyao vya siasa.
Siku
ya kwanza ya ziara yake Rais Dkt. Magufuli aliweka jiwe la msingi la
kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Tanzania Goodwill Ceramic
Tiles Ltd. kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani ambacho ni kikubwa Afrika
Mashariki na Kati kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu
ya kwanza.
Akiongea
katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda chenye uwezo
wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku Rais Magufuli
alifurahishwa na teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae
inayotumiwa na kiwanda hicho na kuhoji kama kuna haja ya serikali
kuendelea kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi.
Rais
Magufuli alisema kuwa “Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi
hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati
wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake
hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa
ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi".
Akiwa
njiani kuelekea Mikoa ya Lindi na Mtwara Rais Magufuli alizungumza na
wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya
Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika
tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji
kabla ya mwisho wa Mwezi wa tatu na kupiga marufuku utozaji wa ushuru
kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.
Aidha,
Rais Dkt. Magufuli anawataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo
kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha katika kipindi hiki mvua
zinaponyesha huku akiweka bayana kuwa Serikali haitatoa chakula cha
msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula
katika maeneo yao.
Akioneshwa
kutoridhishwa na utekeleaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi
alipotembelea ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao
ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015 Rais Magufuli
aliagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya
ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India
Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo
itakapokamilisha mradi huo unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za
ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi
ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.
Katika
kuthibitisha amedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda Rais
Dkt. Magufuli aliitaka Wizara ya Nishati na Madini Wizara ya Nishati na
Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka
iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na
ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji
kusimama mara kwa mara.
Aidha,
Dkt. Magufuli aliitaka Wizara hiyo kuhakikisha wanamega eneo lenye
makaa ya mawe katika eneo la Ngaka lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani
Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote ili iweze kuzalisha yenyewe makaa
ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo Mkoani Mtwara.
Kiwanda
hicho kinachomilikiwa na Alhaji Aliko Dangote tangu kianze kuuza saruji
bei ya bidhaa hiyo sokoni imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko
mmoja wa kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/- na ununuzi wa magari 580
yatasaidia kusafirisha saruji nchi nzima kwa gharama nafuu ambayo
watanzania wengi wataimudu.
Wakati
akikamilisha Ziara yake Mhe. Dkt. Rais Magufuli alifanya mkutano wa
hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara ambapo alisema Serikali
ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Nchi kwa
nguvu kubwa kwa manufaa ya wananchi.
Rais
Magufuli alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutilia
mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa barabara,
uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa viwanda
vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia
kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.
Aidha,
Rais Dkt. Magufuli alioneshwa kusikitishwa na Mkoa wa Mtwara kufanya
vibaya kielimu na kuwataka kuweka msisitizo katika elimu kwani juhudi za
Serikali kuwapelekea maendeleo hazitakuwa na maana kama wananchi
watakuwa hawana elimu.
Ziara
hiyo ya Rais Dkt. Magufuli imeonesha mwelekeo wa Tanzania tunayoitaka
hasa katika maeneo ya usimamizi wa miradi na utekelezaji wake kwa
maslahi ya umma.
SHARE
No comments:
Post a Comment