TRA

TRA

Saturday, April 29, 2017

Duterte: kusini mashariki mwa Asia kuna tishio la madawa haramu

No comments:
Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, leo amewaonya viongozi wa Asia ya Kusini-Mashariki kwamba wanakabiliwa na tishio kubwa la madawa haramu linaloweza kuharibu jamii zao, huku akitoa wito wa ushirikiano wa pamoja.


                          Rodrigo Duterte

Duterte anayelaaniwa na jumuiya ya kimataifa kwa operesheni yake ya ukandamizaji ya kupambana na madawa la kulevya iliyosababisha vifo vya maelfu ya watu, pia amesisitiza kwamba watu wa nje wasiingilie mambo ya ndani ya Asia ya Kusini-Mashariki. 

Katika hotuba yake kwa viongozi waliohudhuria Mkutano wa kilele wa ASEAN wa nchi za kusini mashariki mwa Asia, Duterte alizungumzia mila ya eneo hilo ya kutotaka kuingiliwa katika mambo yake. 

Kiongozi huyo wa Ufulipino aligusia pia mahusiano na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya, ambao wamekuwa wakionyesha wasiwasi juu ya mauaji ya kiholela yanayofanyika katika vita vyake dhidi ya madawa ya kulevya.

Macedonia yatumbukia kwenye mgogoro mzito

No comments:


Macedonia imetumbukia katika mpasuko na mgawanyiko mkubwa wa kikabila kundi la Waalbania waliochache likilengwa
Kiongozi wa upinzani nchini Macedonia ameukataa mwito uliotolewa na rais wa nchi hiyo wa kufanyika mazungumzo ya dharura kati ya viongozi wa chama ikiwa ni masaa kadhaa baada ya waandamanaji wengi wao wakiwa ni wafuasi wa chama tawala cha kihafidhina kulivamia bunge na kuwashambulia wabunge wa upinzani.
Taarifa zilizotolewa na afisa mmoja wa chama cha Social Demokratic zinasema kwamba kiongozi mkuu wa upinzani, Zoran Zaev, hatohudhuria mazungumzo, lakini hakutowa maelezo zaidi kuhusiana na hilo. Afisa huyo hakutaka kutajwa jina kwa sababu hana mamlaka ya kulizungumzia suala hilo mbele ya waandishi habari.
Polisi inasema watu 102 wamejeruhiwa wengi wakiondoka na majeraha madogo kufuatia vurugu zilizozuka.Zaev ni miongoni mwa wahanga wa vurugu hizo pamoja na kiongozi wa chama kingine kidogo cha upinzani cha  waalbania na maafisa 22 wa polisi pia wameumizwa. Rais wa nchi hiyo, Gjorge Ivanov, ametowa mwito wa utulivu kwa kusema:
"Kila mmoja anapaswa kubeba dhamana ya vitendo vyake na kila mtu anapswa kutambua juu ya hatua zitakazochukuliwa kutokana na hili. Hii ni hali inayoweza kupatiwa ufumbuzi kwa misingi ya kuheshimu mfumo wa sheria wa Jamhuri ya Macedonia."
Macedonia iko katika dimbwi la mgogoro mkubwa wa kisiasa ulioanza na kadhia ya udukuzi  wa mawasiliano ya simu miaka miwili iliyopita  pamoja na uchaguzi ambao haukukamilika mwaka jana ukazidi kuitumbukiza hali katika mvurugano. Waziri wa mambo ya ndani amejiuzulu.
Mazedonian Präsident Gjorge Ivanov PK (picture-alliance/abaca/A. Fazlagikj )                      Rais Gjorge Ivanov

Taifa hilo la kusini mashariki mwa Ulaya, Macedonia pia linazidi kugawika kwa misingi ya kikabila huku waandamanaji wakipinga mipango ya upinzani ya kutaka kutoa madaraka makubwa zaidi  kwa Waalbania walio wachache, ambao ni robo ya idadi jumla ya wananchi wa taifa hilo.
Umoja wa Ulaya umelaani vurugu na ghasia za alhamisi mkuu wa seza za nje wa Umoja huo Federico Mogherini amesema  msingi wa demokrasia unapaswa kuheshimiwa.
''Tunazichukulia vurugu siku zote kuwa ni kitu kisichokubalika na hasa zinapotokea katika nyumba ya demokrasia,bungeni na sisi tunaamini kwamba  kila mmoja mjini Skopje anabidi kuiheshimu katiba na demokrasia na kujaribu kuiondoa nchi katika mgogoro huu mkubwa unaoweza kuwa hatari.''
Katika nchi jirani ya Serbia, Waziri Mkuu Aleksander Vucic ameitisha mkutano wa dharura  juu ya usalama kutokana na vurugu hizo.
Kadhalika kiongozi wa chama cha kihafidhina, Nikola Gruevski, amelaani ghaisa hizo lakini anasema mahasimu wake kisiasa ndio waanzilisshi wa chokochoko. Akizungumza katika makao makuu ya chama chake leo hii Gruevski alisema chama cha Social Democrats wamevunja sheria na katiba kwa kumchagua spika mpya wa bunge ambae ni mwanasiasa kutoka kabila la Waalbania licha ya kuwepo mvutano kwa miezi kadhaa katika juhudi za kuunda serikali mpya nchini humo.
Urusi inasema kwamba Umoja wa Ulaya na Marekani ndio fitna wakubwa katika mgogoro huo. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imetowa taarifa leo ikisema nchi za Magharibi ndio waingiliaji wakubwa wa mambo ya ndani ya Macedonia na ndio chanzo kikubwa cha mgogoro wa kisiasa  nchini humo.

Je vita vya Korea Kaskazini vyanukia

No comments:
Marekani ikiionya Korea Kaskazini kutoijaribu Kijeshi,utawala wa Korea Kaskazini nao unajibu mapigo kwa jeuri kubwa Kuongezwa kwa wanajeshi, majibizano ya maneno ya vitisho na kitisho cha vita vya kinyuklia yanazidi kuongeza wasiwasi kaskazini mashariki mwa Asia.
Marekani, kwa upande mmoja, inaimarisha juhudi zake katika eneo la kimkakati na Korea Kaskazini haionekani kusalimu amri wakati diplomasia na juhudi za kuzuia shambulio la nyuklia zikigongana. Kimsingi kunashuhudiwa wingu zito limeifunika rasi hiyo ya Korea.
Ikiwa ni kauli za jeuri na  kujiamini zinazotolewa na serikali ya Korea Kaskazini au upepo wa kishindo unaovuma upande wa Trump au majaribio ya kawaida ya makombora na mazoezi ya kijeshi, yote yanasababisha wasiwasi kote ulimwenguni huku hali ikionesha dalili za mambo kuelekea kufikia katika kiwango kibaya.
Ubabe wa Marekani unapojaribiwa
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, alitowa hotuba yake wiki iliyopita akiwa katika ndege ya USS ambayo ilitumiwa na Ronald Reagan huko Japan na kusema kwamba upanga umeshawekwa tayari.
Kauli hiyo imeonekana moja kwa moja kulenga kuionya Korea Kaskazini kutothubutu kuijaribu Marekani kijeshi akiongeza kusema kwamba "Marekani itajibu kwa kutumia nguvu kubwa ikiwa itashambuliwa."
Siku chache baadaye, katika hatua za kujibu mazoezi ya kijeshi ya wanamaji kati ya Marekani na Japan, gazeti rasmi la serikali Korea Kaskazini la Rodong Sinmun likaandika kwamba vikosi vya kimapinduzi viko tayari kuizamisha meli ya kubeba ndege za kijeshi za Marekani inayoendeshwa kwa nguvu za kyuklia kwa kombora moja tu.
Na hiyo ni baada ya kuripotiwa kwamba meli hiyo ya Marekani ya kundi la USS Carl Vinson itatia nanga  katika bahari ya pwani ya Rasi ya Korea, Korea Kaskazini ilijibu kwa kusema kwamba kupelekwa kwa zana hizo ni kitendo cha hatari kabisa kinachofanywa na wale wanaopanga kuanzisha vita vya nyuklia.
Kikosi hicho cha Vinson kitaungana na USS Michigan, nyambizi iliyosheheni makombora aina ya 144 Tomahawk ambayo ilishawasili katika bandari ya Korea Kusini ya Busan tangu Jumanne wiki hii.
Hali isiyoweza kupuuzwa
Hata hivyo, hadi wakati huu wasiwasi uliopo haujafikia kiwango cha kubadili mambo yalivyo ingawa kuna kitisho kinachozidi kuongezeka katika kanda hiyo ambacho hakiwezi kupuuzwa.
Uwezo wa jeshi la Korea Kaskazini unazidi kuimarika na hakuna ishara yoyote inayoonesha kwamba utawala huo utabadili msimamo wake wa jazba na mabavu, ambao kimsingi unauona ni muhimu kwao na unaostahili kuwepo kwa ajili ya kuuwezesha  kuendelea kuwepo.
Wiki hii pia, nchi hiyo ilionesha nguvu zake za kijeshi wakati ikiadhimisha miaka 85 tangu kuasisiwa jeshi la nchi hiyo ambapo zana nzito nzito zilioneshwa.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini, KCNA, hilo lilikuwa ni tukio kubwa kuwahi kufanyika la maonesho ya nguvu za kijeshi likihusisha mizinga na makombora ya masafa marefu 300 pamoja na nyambizi zinazoweza kutumiwa katika kushambulia meli za kivita.
KCNA halikuishia hapo tu, bali lilikwenda mbali zaidi na kuandika kwamba mazoezi hayo ya kijeshi yameonesha ni kwa jinsi gani Korea Kaskazini ina uwezo wa kuwamiminia mvua ya makombora bila hesabu wale lililowaita ''mabeberu'' yaani Marekani na "wafuasi wao wachafu."

Korea kaskazini yaendelea na ukaidi yafyatua kombora jingine

No comments:

Korea kaskazini imefanya jaribio la kombora leo Jumamosi (29.04.2017)Korea ya kusini na jeshi la Marekani zimesema,ikikaidi onyo la Marekani na,China, zilizojaribu kwa miaka kadhaa kudhibiti mpango wa silaha wa nchi hiyo.

Nordkorea provoziert mit weiterem Raketentest (Getty Images/AFP/Str.)        Makombora ya Korea kaskazini yakifyatuliwa

Jaribio  hilo  lililofanywa  katika  eneo kaskazini mwa  mji  mkuu  wa Korea  kaskazini , Pyongyang, linaonekana  kuwa  limeshindwa, maafisa  wa  Marekani  na  Korea  kusini wamesema, katika  kile ambacho  ni jaribio  la  nne  mfululizo  la  Korea  kaskazini kushindwa  tangu  mwezi  Machi.
Jaribio  hilo linakuja  wakati  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Marekani Rex Tillerson amelionya baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa  kwamba  kushindwa  kuudhibiti mpango  wa  kinyuklia  na  makombora  wa  Korea  kaskazini  kunaweza  kusababisha "matokeo  mabaya".
UN Sicherheitsrat - US-Außenminister Rex Tillerson zu Nordkorea (Reuters/L. Jackson) Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson

Maafisa  wa  Marekani , wakizungumza  kwa  masharti ya  kutotajwa majina, wamesema kombora  hilo huenda  ni  la  masafa  ya  kati  linalofahamika  kama KN-17 na  linaonekana kuwa liliripuka  na  kuvunjika  katika  muda  wa  dakika  chache  tangu  pale lilipofyatuliwa.
Korea kusini  imesema nchi  hiyo  ya  kaskazini  inacheza  na  moto  na  kuionya  kwamba itakabiliwa  na  vikwazo  vikali  zaidi  ya  Umoja  wa  Mataifa.
Ukiukaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa
Jeshi  la  Korea  kusini  limesema  kwamba  kombora  hilo , lililofyatuliwa  kutoka  katika jimbo  la  Pukchang  katika  mwelekeo wa  kaskazini  mashariki, lilifikia  umbali  hewani  wa kilometa 71  kabla  ya  kuvunjika vunjika  dakika  chache  wakati  likiruka. Limesema kurushwa  kwa  kombora  hilo  ni  ukiukaji  wa  wazi  wa  maazimio  ya  Umoja  wa  Mataifa na kuionya  Korea  kaskazini kutochukua  hatua  bila  kufikiria.
US Navy Destroyer USS Mason - DDG 87 (picture-alliance/dpa/A. Delgado) Moja kati ya meli za kivita za Marekani USS Mason - DDG 87

Utawala  wa  rais  wa Marekani  Donald Trump  unaweza  kuchukua  hatua  dhidi  ya  jaribio hilo  la  kombora  la  Korea  kaskazini  kwa  kuharakisha  mipango  yake kwa  ajili  ya vikwazo  vipya  vya  Marekani  dhidi  ya  Pyongyang, ikiwa  ni  pamoja  na  uwezekano  wa hatua  dhidi  ya maeneo  mahususi  ya  Korea kaskazini  na  China, afisa  wa  Marekani ameliambia  shirika  la  habari  la  Reuters jana.
Wakati Korea  kaskazini  inachukua  hatua kwa  kukaidi  mbinyo  kutoka  Marekani  na mshirika  wake  mkubwa  China, Marekani  inaweza  kufanya  luteka mpya  ya  jeshi  la  majini na  kuweka  meli  zaidi  za  kijeshi  na  ndege  katika  eneo  hilo  kwa  nia  ya  kuonesha uwezo  wa  nguvu  zake , afisa  huyo  amesema , kwa  masharti  ya  kutotajwa  jina.
US Flugzeugträger USS Carl Vinson (Reuters/U.S. Navy photo/M. Castellano) Meli iliyobeba ndege za kivita za Marekani USS carl Vinson
Vikwazo vipya
Afisa  huyo  amesema  vikwazo vyovyote  vipya  vinaweza  kuwekwa  katika  siku  chache zijazo na  vinaweza  kulenga  idadi  kadhaa  ya  maeneo  ambayo  tayari  yametathminiwa  na serikali  ya  Marekani  kwa  ajili  ya  hatua  kama  hizo, wakati  utawala  huo  wa  Marekani unaendelea  kutayarisha  mpango  mkubwa  zaidi  wa  vikwazo.
Maeneo  lengwa  ya vikwazo hivyo , afisa  huyo  amesema , yanaweza  kuwa  taasisi  za  kifedha  na  makampuni  muhimu ya  Korea kaskazini  pamoja  na  China, hatua  ambayo  huenda  ikaikasirisha  China.
USA Präsident Donald Trump bei der NRA - National Rifle Association (Reuters/J. Ernst)               Rais wa Marekani Donald Trump

Wakati  rais  Trump  amemsifu  rais  wa  China Xi Jinping kwa  kuashiria ongezeko  la ushirikiano kuhusiana  na  suala  la  Korea kaskazini , afisa  huyo  amesema  Beijing  bado "inahitajika  kuchora  aina  fulani  ya  msitari mchangani" na  Pyongyang kuhusiana  na mpango  wake  wa  kinyuklia.
Hatua  za kijeshi  chini  ya  hatua  zinazofanyiwa  tathmini  ni  pamoja  na  kuonesha  uwezo wa  nguvu  za  Marekani  katika  eneo  hilo  zenye  lengo la  kuizuwia  Korea  kaskazini  na kuihakikishia  Korea  kusini  mshirika  mkubwa  wa  Marekani  kuhusu  usalama  wake, ameeleza  afisa  huyo  wa  Marekani.

Papa Francis aanza ziara nchini Misri

No comments:


Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameanza ziara nchini Misri, katika juhudi za kuhimiza maelewano kati ya Wakristu na Waislamu na kuepusha ghasia zinazofanywa kwa kutumia jina la Mungu.
Ägypten Papst Franziskus in Kairo | mit Abdel Fattah al-Sisi (Reuters/The Egyptian Presidency) Papa Francis akisalimiana na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri mjini Cairo

Mara tu baada ya kuwasili mjini Cairo mchana wa leo, Papa Francis amepokelewa na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kwa heshima za kijeshi, huku makasisi wakijipanga mstari kumsalimia. Baadaye ametembelea chuo kikuu maarufu cha Kiislamu cha Al-Azhar, ambako amefanya mazungumzo na Mufti Mkuu Ahmed al-Tayeb, yaliyoelezewa kama yenye kukamilisha mchakato wa kuboresha mahusiano kati ya Wakatoliki na Waislamu wa madhehebu ya Sunni. Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege kabla ya kutua mjini Cairo, Papa Francis amesema ziara yake ya masaa 27 itakuwa ya kusajiisha umoja na udugu. Ujumbe huo pia ndio alioutoa kwa watu wa Misri, kabla ya kufunga safari kuizuru nchi yao.
''Kwa moyo wenye furaha na shukrani nitaitembelea nchi yenu, ambayo ni kitovu cha ustaarabu na zawadi wa Mto Nile, nchi ya jua na ukaribu, ambako maaskofu na manabii waliishi, na ambako Mungu mwenye rehema na uwezo, aliitoa sauti yake'', alisema Papa Francis na kuongeza, ''Ninayo furaha ya kweli kuja kama rafiki, na kama mjumbe wa amani katika nchi ambayo miaka 2000 iliyopita, iliipa hifadhi familia takatifu iliyokuwa ikikimbia kitisho cha mfalme Herod.''
Mjadala kati ya waislamu na wakristo
Ägypten Besuch vom Papst Franziskus in Kairo (Reuters/Egypt TV/A. Abdallah Dalsh) Ulinzi uliimarishwa mjini Cairo wakati wa ziara ya Papa
Katika ziara yake hiyo fupi, Papa Francis atakutana kwa pamoja na viongozi wa Kiislamu na wa Kikristu, kabla ya kulitembelea kanisa lililoshambuliwa kwa mabomu mwezi Desemba mwaka jana. Watu 29 walipoteza maisha katika shambulio hilo. Shambulio jingine kwenye kanisa la Koptiki mwezi huu wa Aprili liliuwa waumini 45.
Makanisa yote nchini Misri yamewekewa ulinzi wa ziada, kwa hofu kuwa mashambulizi mengine yanaweza kufanywa wakati huu wa ziara ya Papa Francis. Licha ya wasiwasi kuhusu usalama lakini, Papa Francis anatarajiwa  kutumia gari la kawaida tu katika shughuli zake.
Wakati ya ziara yake hii nchini Misri, Papa Francis atahutubia mkutano wa kimataifa kuhusu amani ambao umeandaliwa na chuo cha al-Azhar, ambacho ni kituo cha maarufu cha elimu kwa zaidi ya miaka 1000, chenye msikiti wenye historia ya fahari kubwa.
Kukosoa makosa ya Papa Benedikt wa XVI
Francis ni Papa wa kwanza kuitembelea Misri tangu ziara nyingine ya kihistoria iliyofanywa nchini humo na Papa John Paul wa II mwaka 2000. Uhusiano kati ya Misri na makao makuu ya Kanisa Katoliki uliingia doa enzi za Papa Benedikt wa 16, ambaye kufuatia shambulizi jingine kwenye kanisa la Koptik mwaka 2006 alitoa kauli iliyochukuliwa kama yenye kuunganishi dini ya Islamu na ghasia, kauli iliyokosolewa na chuo cha Al-Azhar kama uingiliaji wa mambo ya ndani ya Misri.
Wakristu wa madhehebu ya Koptik ni asilimia kumi ya wakazi wote milioni 92 wa Misri, na wamekuwa wakilengwa na mashambulizi ya mara kwa mara. Rais wa sasa wa Misri, japo anachukuliwa kama mtu anayetawala kwa mkono wa chuma amekuwa rafiki wa wakristu walio wachache nchini humo, na mwaka 2015 alikuwa rais wa kwanza wa Misri kushiriki katika ibada ya Krismasi.

Siku 100 akiwa rais: Ahadi tano kuu za Trump

No comments:

Donald Trump aliahidi kutimiza ahadi zake za kampeni mara tu  atakapokuwa rais wa Marekani lakini inaoneka kama kuanza kutimizwa kwa ahadi hizo kwa haraka kulitumbukiza serikali kwanye kinamasi.

Donald Trump aliahidi kutimiza ahadi zake za kampeni mara tu  atakapokuwa rais wa Marekani lakini inaoneka kama kuanza kutimizwa kwa ahadi hizo kwa haraka kulitumbukiza serikali kwanye kinamasi.
Donald Trump akiwa kama mgombea alikuwa hana mjuto na alikuwa na majigambo wakati akiahidi ukuta kwenye mpaka wa Mexico utajengwa na utakuwa wa kupendeza,mpango wa afya wa Obama ni balaa utatenguliwa na kuondolewa, wamarekani wanaofanya kazi kwa bidii ambao wameunguliwa na mfumo wa serikali watarudishiwa kazi zao na utu wao.
Trump bafo ana siku 1,300 zilizobakia madarakani kutimiza ahadi zake alizozitowa katika rodha ya kampeni. Lakini hakuna atakayekanusha ametimiza sehemu kubwa ya ahadi hizo katika siku 100 za kwanza.
Hivi ndivyo hali iiliyo kwa sasa:
1)Kumuweka jaji mhafidhina katika mahakama ya juu : Hili bila ya shaka ni ushindi mkubwa kabisa wa Trumph hadi sasa na linatilia mkazo sababu ya Warepublikan waliokuwa na mashaka kuamuwa kumeza nyongo yao wenyewe na kumpigia kura.Kiti kilicho wazi katika mahakama hiyo ya juu na uwezakano wa nafasi nyengine zaidi kujazwa iikuwa ni hatari kubwa kumchaguwa Mdemokrat. Kama vile ilivyo kwa majaji wenzake mhafidhina wa jimbo la Colorado Neil Gorsuch amechaguliwa kushika wadhifa huo maisha.
Maisha katika mpaka wa Mexico
Grenzanlagen USA Mexiko (Reuters/M. Blake) Mpaka unaoitenganisha Marekani na Mexico.
Kuutenguwa mpango wa afya wa Obama na kuuweka mwengine: Huku ni kushindwa kabisa katika siku zake 100 za kwanza madarakani.Sheria ya huduma za afya ya Obama daima ilikuwa na utata-ilianza kuongezeka umashuhuri wake mara tu baada ya Trump kushinda uchaguzi hapo mwezi wa Novemba mwaka jana na kuja kuwa tatizo kwa Warepuplikan ambao sera yao kuu tokea kupitishwa kwa Sheria hiyo ya kumudu huduma za afya yaani mpango wa afya wa Obama ni kujaribu kuutenguwa.Lakini licha ya kuusakama mpango huo kwa miaka saba ule wakati wa kufanikiwa kwao ulipowadia sheria ya Huduma za Afya ya Marekani (GOP) ambayo ilikusudiwa kuwa mshindani wa mpango wa Obama ulikuja kuanguka kwa ghafla na kuondolewa hata kabla ya kupigiwa kura.
3.Kujenga Ukuta:Trump aliahidi kupambana vikali katika suala la wahamiaji,iwe kisheria au venginevyo.Mbali na wito wake wa kuajiri mawakala wapya 10,000 wa uhamiaji chini ya usimamizi wake mamlaka ya Utekelezaji wa masuala ya Uhamiaji na Forodha(ICE) imeongeza misako yao na kuamua kuwarudisha makwao wahamiaji walioko nchini humo kinyume na sheria hatua ambayo imejumuisha kuzitenganisha familia na kuwarudisha makwao watoto ambao walikuwa na bado kisheria wanahifadhiwa chini ya sera za utawala uliopita.
Na kwa suala la ukuta wenyewe ? Mkuu wa bajeti wa Trump amesema kwamba kupata fedha kwa ajili ujenzi wa ukuta huo katika bajeti ya mwakani kwa serikali jambo hilo ni la "lazima."
Kituo cha matangazo cha "Fox News" kimetangaza ujenzi wa ukuta huo yumkini ukaanza mapema katika kipindi cha kiangazi mwaka 2017.  Lakini suala la kugharimia ujenzi wa ukuta huo linaendelea kuwazozaniwa kati ya rais na bunge la Marekani.
Marekani kwanza
USA Washington - President Donald Trump bei griechischer Unabhänigkeitsfeier (Reuters/C. Barria) Rais Donald Trump wa Marekani.
4.Kuwapiga marufuku Waislamu kuingia Marekani: Sinema ya siku 100 ya kwanza madarakani kwa Trump ilianza hasa wakati aliposaini amri ya rais yenye kuamuru kupiga marufuku kuingia nchini humo kwa raia wowote wale kutoka nchi saba zenye idadi ya kubwa ya Wislamu wawe na viza  au hata kadi za kijani za ukaazi wa Marekani.Maandamano yalizuka katika viwanja vya ndege vyote vikuu nchini Marekani na kesi za madai zikafunguliwa.Warepaplikan waliungana na hata baadhi ya Wademokrat walishutumu amri hiyo ya rais.Wakati mahakama huko San Francisco ilipogunduwa kwamba amri hiyo imekiuka katiba,Trump alidokeza kwamba ataipeleka Mahakama ya Juu.Baadae aliamua kusaini amri mpya ya rais,safari hii akipiga marufuku kuingia nchini kutoka tu nchi sita.Amri hiyo pia imesitishwa na hivi sasa iko mahakamani.
5.Marekani kwanza : Ahadi hii inaweza kutafsiriwa kwa mapana kwa njia mbali mbali -kuyaweka mbele kwanza maslahi ya kiuchumi ya Marekani au kuikwamuwa Marekani katika ahadi zake za sera ya kigeni.Watu wengi walifikiri kwamba ilikuwa imekusudia ahadi ya kulenga kwenye matatizo yalioko ndani ya nchi na kuipuza dunia.
Mmojawapo wa mfano mkubwa kabisa wa ahadi hiyo ni uamuzi wa Trump wa kujitowa katika makubaliano ya ushirikiano kati ya Ulaya,Pasiifiki na Marekani (TTP) ambayo ni makubaliano ya biashara ya kimataifa yenye utata yalioshinikizwa na Obama na Clinton na yaliyojadiliwa kwa miaka mingi na na mataifa 12 ya Asia. Ameyataja kuwa ni "makubaliano mabaya" ambayo yatazidhuru kampuni na wafanyakazi wa Marekani
Hata hivyo inaonekana Trump amejifunza kwamba kuwa kiongozi wa dunia ilio huru inamaanisha uwasiliane nayo kwa kawaida,.Siku 100 za Trump madarakani pia zimeshuhudia shambulio la kijeshi la kwanza la Marekani dhidi ya Syria,kuongezeka kwa mvutano na Korea Kaskazini na kutaka kurudi katika ahadi yake ya kuyatupilia mbali makubaliano ya nyuklia ya Iran aliyoyaita "mabaya".
Uchunguzi wa maoni unadokeza kwamba kambi ya" Marekani kwanza"  bado inamuunga mkono lakini hakuweza kupata wafuasi wapya

MAKAMU WA RAIS MAMA SAMIA SULUHU HASSAN KUZINDUA MRADI MKUBWA WA MAJI MKOANI TABORA

No comments:



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo mafupi leo kutoka kwa mmoja wa wataalamu wa mradi huo, kuhusiana na mradi wa maji unaojengwa katika kijiji cha Mabama wilayani Uyui mkoani Tabora,Makamu wa Rais Mama Samia atazindua mradi huo wa maji utakao wafikia watu zaidi ya elfu 40 katika vijiji 32 mradi huu umedhaminiwa na serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA.Picha kwa hisani ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akileza jambo mara baada ya kupata maelezo mafupi leo kutoka kwa mmoja wa wataalamu wa mradi huo, kuhusiana na mradi wa maji unaojengwa katika kijiji cha Mabama wilayani Uyui mkoani Tabora,Makamu wa Rais Mama Samia atazindua mradi huo wa maji utakao wafikia watu zaidi ya elfu 40 katika vijiji 32 mradi huu umedhaminiwa na serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akifuatilia yaliyokuwa yakijili kabla ya uzinduzi wa mradi wa maji utakao wafikia watu zaidi ya elfu 40 katika vijiji 32 mradi huu umedhaminiwa na serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA.Kulia ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji,Inj.Gerson Lwenge na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mh.Prof.Kitila Mkumbo pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Mh.Aggrey Mwanri.
Baadhi viongozi na wawakilishi wa wananchi na wadau mbalimbali wakiwa katika tukio hilo la uzinduaji mradi wa maji,ambapo Mgeni rasmi ni Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan.
Baadhi ya vijana wakishiriki kuhudhudia tukiao hilo
Baadhi ya Wanachama wa CCM na wananchi wa kwa ujumla wakifurahia kwa tukio hilo adhimu la kuzinduliwa mradi mkubwa wa maji unaozindulia katika kijiji cha Mabama wilayani Uyui mkoani Tabora,Makamu wa Rais Mama Samia atazindua mradi huo wa maji utakao wafikia watu zaidi ya elfu 40 katika vijiji 32 mradi huu umedhaminiwa na serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA.

MIKOPO YA TSH. BIL 1 YATOLEWA JIJINI ARUSHA, WAZEE WAPATIWA VITAMBULISHO

No comments:


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo(katikati) akiwakabidhi wawakilishi wa Vikundi vya Wanawake na Vijana mfano wa hundi ya Tsh Bil 1 wakati wa Ziara yake Jijini hapa .kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya Mhe. Gabriel Daqaro na Kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji Athumani Kihamia.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo (katikati kulia) akimkabidhi Mzee Zahran Mtweike (Mbele kulia) Kitambulisho cha Wazee.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Athumani Kihamia(kulia) akiteta Jambo na Naibu Meya wa Jiji Mhe. Viola Likindikoki wakati wa Ziara ya Mkuu wa Mkoa Jijini hapa.
Diwani pekee wa Cccm katika Jiji la Arusha Mhe. Abdulrasul Tojo (mbele) akifuatilia nkikao cha Mkuu wa Mkoa wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake Jijini hapa.

Nteghenjwa Hosseah, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amekabidhi hundi ya Tsh Bil 1 kwa vikundi vya wanawake na Vijana ikiwa ni mchango wa asilimi kumi (10%) ya mapato ya Halmashauri Jiji la Arusha.

Akikabidhi hundi hiyo kwa Vikundi 269 ambavyo kati ya hivyo 162 ni Vikundi vya wanawake na 107 ni vijana amewataka kutumia fedha hizo kwa shughuli zilizokusudiwa ili ziweze kuwatoa katika lindi la umasikini.

“Mikopo hii inatolewa ili kuendeleza shughuli za kijasiriamali ambazo ndizo zilizopelekea mkidhi vigezo vya kupata Fedha; Nimatumaini yangu fedha hizi  zitawawezesha kuongeza mitaji yenu na kuwapa ari ya kujituma zaidi huku mkizingatia nidhamu ya pesa ili muweze kuzirejesha kwa wakati na makundi  mengine waweze kupata fedha hizo”Alisema Rc Gambo.

Mikopo hiyo inayotolewa kwa mujibu wa Sheria na miongozo inayoelekeza asilimia kumi ya Mapato ya ndani ya Halmashauri kutolewe kama Mikopo ya riba nafuu kwa vikundi vya wananwake na vijana na kwa jiji la Arusha kiasi kinachotakiwa kutolewa ni Bil 1.2 kwa Mwaka huu wa Fedha hivyo kiasi kilichotolewa ni kwa kipindi cha robo tatu kuanzia Julai 2016 – March 2017.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa Mhe. Gambo amekabidhi vitambulisho 3850 kwa Wazee wa kuanzia miaka 60 ambao ni wakazi wa Jiji la Arusha vitakavyowasaidia kutambulika katika Vituo vvya Afya na kupatiwa huduma za Afya bure.

Kukabidhi kwa Vitambulisho hivyo kunafanya jumla ya Idadi ya vitambulishbo vilivyotolewa na Jiji kwa wazee kufikia 5966 na bado zoezi hili linaendelea kuwabaini wazee wote na kuwatengenezea vitambulisho.

MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI APRIL 29,2017

No comments:


 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger