Borussia Dortmund imefikisha mwisho vipigo
katika fainali tatu zilizopita za kombe la Ujerumani, DFB
Pokal na kunyakua mara hii kombe hilo kwa kuishinda Eintracht Frankfurt
2-1 siku ya Jumamosi(27.05.2017) mjini Berlin.
Bao la mkwaju wa penalti katika dakika ya 67 la
Pierre-Emerick Aubameyang lilitosha kuipa ubingwa Dortmund. Ilikuwa
taji la kwanza kubwa kwa mshambuliaji huyo kutoka Gabon akiwa
na Dortmund, lakini inawezekana kuwa ni mara ya mwisho kwa
mchezaji huyo kuonekana katika sare za BVB baada ya kusema
ataamua hatima yake baada ya mazungumzo na viongozi wa klabu
hiyo.Ushindi wake wa kombe la Ujerumani unakamilisha msimu wa mafanikio kwake binafsi wa mabao 40 katika mashindano yote aliyoshiriki, ikiwa ni pamoja na kumshinda mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski na kuwa mfungaji bora katika Bundesliga akiwa na mabao 31.
Ushindi huo umekamilisha hali ya mabadiliko kwa Dortmund ambayo msimu huu ulishanza kuonekana umeharibika kufuatia shambulio la bomu katika basi la timu hiyo mwezi Aprili ambapo mlinzi wa Dortmund Marc Bartra alijeruhiwa na wachezaji kupata fadhaa.
Mapambano yaliendelea
Lakini kocha Thomas Tuchel aliendelea kuwapa machezaji wake motisha na ari ya kucheza hadi mwisho.
"Nimepwelewa, sina nguvu tena sasa," amesema Tuchel , ambaye hatima yake katika klabu hiyo haifahamiki baada ya mzozano na wakubwa wake katika klabu. "Ilikuwa ni kazi ngumu lakini tumefanikisha."
"Baada ya kile kilichotokea katika shambulio na kuweza kuepuka vikwazo kila mara na kisha kuja hapa na kushinda ni kitu mahsusi kabisa kwetu sisi," alisema , na kuongeza angependa kubakia Dortmund. "ndio , bila shaka ningependa kubakia."
Lilikuwa ni taji la kwanza kwa Tuchel , ambae alijiunga na Borussia Dortmund mwaka 2015, na kwa mshambuliaji wa pembeni Marco Reus , anaonekana kuwa miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vya juu kabisa katika kizazi chake , lakini ambaye amepoteza fainali nne tangu kuwasili mwaka 2012 katika kikosi cha BVB, ikiwa ni pamoja na fainali ya Champions League ya mwaka 2013.
Ushindi wa Dortmund pia una maana kwamba Freiburg , iliyoshika nafasi ya 7 katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga , itashiriki katika ligi ya Ulaya katika awamu ya mchujo.
Mchezo ulikuwa wa vuta nikuvute
Dortmund ilianza kwa nguvu mwanzoni mwa mchezo huo wakati Dembele alipokea pasi kutoka kwa Lukasz Piszczek upande wa kulia na kumpiga chenga mlinzi kabla ya kuuzungusha mpira huo na kutumbukia wavuni na kuandika bao la kwanza kwa Borussia.
Frankfurt ilihitaji muda kuweza kurejea katika hali yao ya kawaida baada ya bao hilo na walifanya hivyo katika fursa yao ya kwanza wakati Rebic alipopewa pasi safi kutoka kwa Mijat Gacinovic na kuutumbukiza mpira wavuni akimwacha
mlinda mlango Roman Buerki akigaaga.
Karibu Frankfurt wapate bao la pili katika dakika ya 39 lakini shuti la chini la Haris Severovic liligonga mlingoti wa goli wakati Dortmund walisubiri kwa hamu mapumziko.
"Tulicheza mchezo mzuri katika muda wote wa dakika 90," alisema kocha wa Frankfurt Niko Kovac. "Walikuwa wazuri katika kipindi cha pili. Mambo fulani yanaamua fainali. Tulipiga mpira katika mlingoti wa goli, na kisha ikaja penalti dhidi yetu."
Dortmund ilipata mkwaju wa penalti katika dakika ya 67 na Aubameyang , aliukwamisha mpira huo wavuni na kuhitimisha msimu wenye kumbukumbu kadhaa .
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment