Utambuzi wa historia ya nchi una
mchango mkubwa kwa vijana kuweza kufahamu madhila yaliyotokea na jinsi
viongozi walivyopigana katika kuleta uhuru na maendeleo ya Taifa. Katika
makala haya Judith Mhina wa Idara ya Habari MAELEZO anaelezea.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya
Kwanza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt Salim Ahmed Salim
amesema kuwa vijana barani Afrika wana wajibu wa kujua historia ya nchi
na viongozi waliojitolea kuleta uhuru, umoja, amani na maendeleo ya
watu.
Amesema, athari za vijana kutojua
historia ya nchi na viongozi waliopigania uhuru ni pamoja na kukosa
uzalendo na uwajibikaji katika kutekeleza malengo ya Serikali katika
kuleta mapinduzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii jambo ambalo
linarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Ameeleza kuwa, nafasi waliyonayo
kama vijana ni kujifunza jinsi viongozi wetu walivyoweza kuweka misingi
ya umoja, amani, mshikamano na changamoto zilizowakabili na jinsi
walivyoweza kuzitafutia ufumbuzi badala ya kukata tamaa na kuilaumu
Serikali kuwa haiwasaidii.
Dkt Salim amefafanua kuwa nchi
yetu imeonyesha muelekeo mzuri katika kulikomboa kundi kubwa la vijana
kuelekea kwenye uchumi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. “Mimi
binafsi naipongeza Serikali yetu kwa kuonesha nia njema ya kupunguza au
kuondoa changamoto, zinazowakumba vijana wetu. Vijana ni wengi kuliko
kundi lolote nchini na hawana uhakika wa maisha yao ya kila siku hivyo
wanahitaji kubadilika.”
Mwana-diplomasia huyo mkongwe
nchini ameendelea kusema kwamba maamuzi ya Serikali ya Tanzania kuelekea
kuwa Taifa la viwanda yatahamasisha vijana kupenda kujishughulisha na
kazi mbalimbali za uzalishaji kama vile kilimo nk.
“Jambo la msingi kwa Serikali ni
kuhakikisha kwamba inaweka mazingira mazuri na rafiki kwa vijana
kuvutiwa katika sekta mbalimbali kwani nchi yetu inayo ardhi ya kutosha
tofauti na nchi nyingine barani Afrika. Lakini pia napenda kuchuku fursa
hii kuwaasa vijana kuchangamkia fursa hiyo kwani ni mtaji mkubwa kwao
katika kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.”
“Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba malighafi zote zinapata masoko
katika viwanda, miundombinu ya uhakika. Aidha, hii itachochea uzalishaji
na ajira kuongezeka maana bidhaa zote zitaongezwa dhamani hapa nchini
badala ya kuagiza nje bidhaa zilizoongezwa thamani na kudidimiza uchumi
wa nchi yetu.” Amesisistiza Dkt Salim.
Akitoa Mfano wa athari za vijana
kutojua historia yao Dkt Salim amesema Afrika ya Kusini ni moja kati ya
nchi za Afrika amabazo vijana wake wamekata tamaa na kutowathamini Wazee
walioshiriki katika harakati za kuleta ukombozi. Amesema, kitendo hiki
cha kuwadharau wazee kimepelekea mfarakano kati ya makundi haya mawili
ambayo yanawajibu mkubwa wa kushirikiana na kuijenga Afrika ya Kusini
yenye neema kwa wananchi wake wote bila kubagua.
Ameeleza kwamba vijana hao
wamejenga chuki na kuwachukia vijana wenzao waliotoka katika nchi
nyingine za Afrika na kuwaona maadui kwa kwenda nchini mwao na kufanya
kazi ambazo wao wanadhani ni za kwao. Athari hii inajitokeza kwa kuwa
hawajui historia ya nchi yao na nini viongozi wao walipigania katika
kuweka misingi ya umoja, amani na mshikamano Barani Afrika.
Hata hivyo siwalaumu vijana hata
kidogo kwa hakika vijana wana hali ngumu ya maisha kweli kweli,
wanahangaika kutafuta riziki, bila mafanikio. Ni vema kukaa nao na
kuongea kuhusu hali zao za maisha na changamoto zinazowakabili kwa
pamoja kutafuta ufumbuzi wa changamoto husika.
Bara la Afrika lina changamoto
nyingi, kama za uongozi, vita vya madaraka, makundi yanayohamisiana,
vita vya wenyewe kwa wenyewe , ukabila na mengineyo ambayo hayaleti
picha nzuri kwa Afrika na yanadhoofisha ustawi wa Bara letu na vijana
kukata tamaa.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere ina
jukumu la kutoa elimu kwa vijana wote Barani Afrika juu ya mustakabali
wao na kuweka misingi imara ya umoja, amani, mshikamano na Maendeleo
kwa watu wote katika nchi zao bila kubaguana.
Tunaendesha makongamano, midahalo
na semina katika majukwaa mbalimbali ili kuwaelimisha vijana kuhusu
historia za nchi zao , viongozi wao na misingi waliyoiweka na umuhimu wa
kutanzua kwa pamoja changamoto zilizopo na kuongea yale yote ambayo
wanadhani hayaendi vizuri.
Dkt. Salim amewomba vijana
kuzingatia elimu wanayopewa maana Taasisi ya Mwalimu Nyerere inahitaji
kupata viongozi miongoni mwa vijana wa Tanzania. Ni vema kujua
changamoto zilizopo ili vijana hao watakaochukua uongozi kuendelea
kuelezea, kufundisha, kuuisha katika misingi ya umoja, amani, mshikamano
na maendeleo kwa watu wote na pia ustawi wa Mataifa yote ya Afrika.
Akizungumzia suala la uongozi
na ushiriki wa vijana katika kujenga Taifa, Dkt Salim amesema ni vema
vijana kushirikishwa katika uongozi kwa kuwa bado wana nguvu ya kuleta
maendeleo katika nchi zao. Hata hivyo alitoa tahadhari na kusema “Kijana
sio kigezo cha uongozi hata kidogo”,
Akitoa mfano Dkt Salim amesema,
“Mimi niliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri nikiwa na miaka
22, nadhani ni umri mdogo kuliko vijana wa sasa wanaoteuliwa, lakini
niliaminiwa na kutimiza wajibu wangu kwa nchi na viongozi wangu
walioniteua, kwa kuwa nilijua tulikotoka, tulipo na tunakotaka kuelekea.
Hayo nilijifunza kutoka kwa viongozi wangu Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.”
Dkt Salim muda wote wa uongozi
kama Balozi na mwakilishi wa nchi kimataifa alielezea msimamo, matakwa
na mapendekezo tunayokubaliana nayo kimataifa. Aidha, alisisitiza suala
la umoja, amani, mshikamano na jinsi ya kuleta maendeleo katika nchi
zote za Afrika kwa kuwa nchi yetu inaona bila umoja hakuna suluhisho la
amani katika nchi zetu na alifanya hayo kwa kuwa nilijua historia ya
nchi yangu.
“Wito wangu kwa vijana ambao
watakuja kuiongoza Taasisi ya Mwalimu Nyererer ni vema wakajipanga kwa
kuwa kazi iliyopo mbele yao ni kuwaelimisha vijana wenzao ili kuthamini
na kuuisha umoja, amani na kuleta maendeleo kwa watu wote iwe ni sehemu
ya maisha yao.”
Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume ni mfano wa kuigwa katika kudumisha
umoja, amani na mshikamano katika Bara la Afrika. Umoja wao ulizaa
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Dkt. Salim alimalizia kwa kusema
Mwalimu Nyerere siku zote za maisha yake, alikuwa akitembea na kuwaasa
Watanzania juu ya umoja, aman, mshikamano na Maendeleo kwa watu wote
bila ubaguzi. Mwalimu alitambua wajibu wake.
Akitoa hitimisho Dkt Salim
amesema: “Hapa Tanzania asilimia 60 ya idadi ya watu milioni 50 ni
vijana, hawa wasipoelewa na kuuisha misingi ya Taifa lao yaani umoja,
amani, mshikamano na Maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi tutakuwa
tumefanya kosa kubwa sana na dunia itatulaumu kwa hilo, kwa sababu
Tanzania ndio mfano wa kuigwa.”
SHARE
No comments:
Post a Comment