Kijiko kikifanya kazi ya kuchimba makaa ya mawe katika mgodi
wa makaa ya mawe uliopo eneo la mgodi wa Ngaka Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10
Mei, 2017.
|
Malori maalum yakibeba vifusi yakielekea kupakia vifusi vya
udongo katika eneo linaloandaliwa kuanza kuchimbwa makaa ya mawe katika eneo la
mgodi wa Ngaka Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei, 2017.
|
Kijiko kikiweka kifusi cha makaa ya mawe katika lori la
kupakia kifusi mara baada ya kuchimbwa katika eneo la mgodi wa makaa ya mawe wa
Ngaka lililopo Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei, 2017.
|
Mashine ya kusaga makaa ya mawe katika eneo la mgodi wa makaa
ya mawe wa Ngaka Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma ikifanya kazi ya kusaga makaa ya
mawe yaliyochimbwa 10 Mei, 2017.
|
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya kuzalisha makaa ya mawe nchini, Tancoal Energy Limited imetekeleza
kwa zaidi ya asilimia 100 agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe maradufu.
Taarifa hiyo iliyotolewa
jana na Mtendaji
Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. James Shedd wakati alipokutana na Waandishi wa habari
waliotembelea mgodi huo uliopo eneo la Ngaka katika wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma.
Bw.
Shedd amesema kwamba, kampuni yake kwa sasa inazalisha kiasi kikubwa cha makaa
ya mawe kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya tani 60,000 kwa mwezi na ziada ya
tani nyingine 20,000 ambazo pia zinauzwa katika nchi za Uganda, Kenya na Rwanda.
“Kampuni
yetu imeongeza uzalishaji wa makaa ya mawe kwa zaidi ya asilimia 100 na tayari
magari yatumikayo katika ubebaji na uchimbaji wa makaa ya mawe yako njiani
kufika huku katika eneo la mgodi ili kuzidi kuongeza uzalishaji na hatimaye
tani za uzalishaji wa madini haya zitazidi kuongezeka”, alisema Bw. Shedd.
Kwa
upande wake Naibu Meneja wa Mgodi wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania
Bw. Edward Mwanga ameeleza kuwa, kampuni
ya Tancoal kwa sasa imeongeza magari yakiyofanya kazi toka 25 hadi 30 ambapo
kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia gari 67, na sambamba na ongezeko
hilo wameongeza mizani ya kupimia magari ili pindi itokeapo ongezeko la magari
ya kubeba makaa ya mawe mzani huo utumike kuyapima.
“Kazi
yetu huku ni kupakia kutokana na oda ya wateja wetu na idadi ya gari zilizokuja
na asubuhi huwa tunapewa taarifa ya gari zilizoko njiani na tunahakikisha kuwa
ndani ya saa moja gari hizo ziwe zimepakia makaa yam awe na kuondoka, hivyo tumeongezaidaid
ya magari na pia tumeboresha mizani na kupanua eneo”, alisema Mwanga.
Kuhusiana
na changamoto zikizoikabili kampuni hiyo amesema kuwa mwanzo wamekuwa
wakikabiliana na changamoto za ikiwemo uhaba wa vifaa, barabara, mvua pamoja
suala la uagizaji wa makaa ya mawe toka kwa wateja ambapo kwa sasa changamoto
hizo zimetatuliwa na hali ya ongezeko la uzalishaji wa madini hayo imeongezeka.
Kwa
upande wake Meneja Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa Kampuni ya Tancoal Energy
Tanzania Limited Bw. Bosco Mabena amesema kwamba, katika mgodi wao kuna sehemu
ya Maabara ya kisasa ambayo hutumika kuchukua sampuli za makaa ya mawe na
kuzipeleka katika hatua mbalimbali ikiwemo mkaa ulipochimbwa, katika hatua ya
processing na pia mkaa unapokwenda kwa wateja, hivyo maabara yetu hutumika
kuchukua sampuli kwa kila gari ili kutunza rekodi.
Ameongeza
kuwa mgodi wao una udhibiti mzuri wa makaa ya mawe kwasababu ili kuhakikisha
kuwa mkaa wa mawe uko safi magari yote yanayofika katika eneo hilo yanakaguliwa
ili kuhakikisha kuwa hayana uchafu wowote na shughuli ya ufungaji hufungwa na
wataalam wao maalum ambao ufungaji wao hauwezi kuchafua mkaa huo kwakuwa
taarifa za gari ikiwemo dreva wa gari na namba ya gari huchukuliwa ili pindi
itakeapo taarifa ya uchafuzi wa mkaa inakuwa rahisi kutambua chanzo.
Kwa
kipindi walipokuwa na mzani mmoja waliweza kupakia gari 50 kwa mzani mmoja kwa
wakati wa mchana na usiku gari 30 hadi 40 ambapo hiyo ni sawa na wastani wa
tani 2,500 kwa siku.
“Kwa
sasa pindi mizani ilipoongezeka ongezeko la upakiaji naamini utaongezeka hadi
kufikia gari 75 kwa mchana, na kuanzia 40 hadi 50 kwa usiku kwakuwa bado tuna
nafasi kubwa ya kufanya hivyo na pindi magari yatakapozidi kuongezeka basi
tutatumia mizani yote miwili”, alisema Mwangosi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilinith Mahenge ametaja baadhi ya
changamoto zilizoikabili Kampuni ya Tancoal na namna jinsi Kampuni hiyo
ilivyotekeleza agizo la Serikali ambapo amekiri kuwa kwa sasa kampuni hiyo
inafanya vizuri katika kuhakikisha kuwa madini hayo yanazalishwa kufikia
malengo yaliyoagizwa na Serikali.
“Tancoal
walikua na changamoto ikiwemo ubovu wa barabara, uhaba wa vifaa vya uchimbaji
makaa lakini kwa sasa wamejitahidi kuzitatua changamoto hizo na mimi mwenyewe nimekwenda
kukagua na kujionea baadhi ya vifaa walivyoongeza na ninaamini zile tani elfu
60 kwa mwezi watazifikia”, alisema Dkt. Mahenge.
Mhandisi
Migodi toka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, Godfrey
Wandibha anaeleza kuhusu suala la bei ya makaa yam awe na suala la agizo la
Mhe. Rais la kumpatia mmiliki wa kampuni ya Dangote eneo la kuchimba madini
hayo ambapo amesema kwamba, tayari alishapatiwa leseni kwa ajili ya kuanza
kuchimba.
“Dangote
yeye kwa sasa anatakiwa kukaa na mtu ambaye alikuwa mwenye lile eneo ili
kukubaliana baadhi ya mambo ambayo ni ya kawaida ili akishayakamilisha aanze
uchimbaji lakini suala la kupewa eneo tayari lilishakamilika kama Rais
alivyokuwa ameagiza”, alisema Wandibha.
Awali agizo la Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alilitoa mapema Januari 6, 2017 mara
baada ya kupokea taarifa na kutembelea katika mgodi wa Ngaka ili kuona shughuli
za uzalishaji katika eneo hilo.
Aidha,
Waziri Mkuu aliitaka kampuni hiyo ya TANCOAL Energy kutimiza masharti ya
mkataba iliouingia na Serikali mwaka 2008.
Kampuni
ya TANCOAL iliundwa Aprili 3, 2008 na kampuni tanzu ya Atomic Resources
Limited, ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Pacific Corporation East
Africa (PCEA) na kwa sasa inaitwa Intra Energy (T) Limited, ambayo hisa zake ni
asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye asilimia 30 ya hisa.
Mgodi
wa Ngaka uko wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na unamilikiwa na kampuni ya
TANCOAL kwa ubia baina ya NDC na kampuni ya Intra Energy Corporation ya
Australia.
SHARE
No comments:
Post a Comment