Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alimkaribisha mwenzake
wa Urusi, Vladimir Putin, mjini Paris katika mazungumzo yaliyomalizika
jana jioni, ambayo baadaye Macron alisema yalikuwa ya kuelezana ukweli
wote.
Ulikuwa mkutano wa kwanza baina ya marais Emmanuel Macron na Vladimir Putin tangu Macron aliposhinda uchaguzi wa tarehe 7 Mei, na ulidumu kwa zaidi ya saa mbili. Wote walielezea nia ya kujikita juu ya maslahi ya pamoja, badala ya tofauti kati ya nchi zao.
Putin alisema Macron amependekeza kuwepo kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa nchi mbili katika masuala ya kupambana na ugaidi, na wote wawili walikubaliana kuwa Syria haipaswi kuachwa kugeuka taifa lililoshindwa. Macron alisema mzozo wa Syria utasuluhishwa kupitia juhudi za pamoja, ambazo alisema zimejengewa msingi katika mazungumzo baina yake na Vladimir Putin.
Syria yapata kipaumbele
Rais Putin ambaye ni mshirika muhimu wa utawala wa Rais aBashar al-Assad wa Syria alipinga hatua zozote ambazo zinaweza kuhujumu uhuru wa Syria kama taifa.
Alisema ''Kuhusu Syria msimamo wetu unafahamika vyema, na nimeurudia pia kwa rais: Ni muhimu kwamba vita dhidi ya ugaidi visiharibu uhuru wa nchi ambazo tayari zinazongwa na matatizo ya ndani, lakini nina uhakika kwamba tunaweza kuungana katika kuwapiga magaidi na kupata matokeo mazuri''.
Putin aliongeza kuwa, ''tunaweza kushinda tu iwapo tutaunganisha nguvu zetu na kufanya kazi pamoja'' kupambana na janga hili la karne ya 20 na ya 21''
Rais Macron alikubaliana na Putin kuhusu kuepushga kusambaratika kwa mataifa, lakini akaeleza bayana kuwa kwa Ufaransa kuna msitari ambao kamwe haupaswi kuvukwa.
''Natilia maanani kuwa mataifa yaliyoshindwa ni kitisho kwa demokrasia yatu, na tumeshuhudia yakigeuka ngome za makundi ya kigaidi. Kwa hiyo tuna matumaini kuwa tutaweza kuhakikisha kipindi cha mpito kwa Syria kuelekea demokrasia, na hilo nimemhakikishia Rais Putin. Lakini pia nimesema wazi kuwa ikiwa upande wowote utavuka msitari mwekundu kwa kutumia silaha za sumu, bila kuchelewa Ufaransa itachukua hatua za kulipiza kisasi'', Alisema Macron.
Mizengwe ya wakati wa uchaguzi yaibuliwa
Juhudi za Urusi kumhujumu Emmanuel Macron wakati wa kampeni na kumpendelea mpinzani wake kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen pia lilizungumziwa, na ingawa Putin alitaka kulipuuza, Macron alivishutumu wazi wazi vyombo vya habari vinavyodhaminiwa na Ikulu ya Rais Putin, Kremlin, kuwa vilitangaza habari za uongo.
Mambo mengine yaliyopewa umuhimu katika mazungumzo baina ya viongozi hao ni mzozo wa Ukraine, ambao ulisababisha nchi za magharibi kuiwekea vikwazo Urusi. Putin alisema vikwazo hivyo ambavyo vimeuumiza uchumi wa nchi yake, havisaidii chochote katika kuusulihisha mzozo wa Ukraine.
Wachambuzi wamesifu jinsi Rais Macron mwenye umri wa miaka 39 alivyoonyesha ukomavu wa kisiasa, kwa kusimamia maadili na maslahi ya nchi yake katika hali ya utulivu lakini isiyotetereka.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment