Umoja wa Ulaya umewawekea vikwazo vipya maafisa wengine
tisa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, akiwemo msemaji wa
serikali Lambert Mende na Kalev Mutondo ambaye ni mkuu wa kitengo cha
taifa cha ujasusi.
Vikwazo hivyo vimewekwa huku kukiwa na msukosuko baada ya rais Joseph
Kabila kukataa kuachia ngazi. Kulingana na Umoja huo wa Ulaya hao
waliolengwa na vikwazo hivyo vinavyojumuisha kufungiwa kwa mali zao na
kufungiwa kusafiri wanashikilia nyadhfa za juu katika uongozi na vyombo
vya usalama.Watu hao tisa sasa wanajiunga na wengine saba waliolengwa na vikwazo vya EU mwezi Disemba baada ya makabiliano na waandamanaji waliokuwa wanampinga Kabila mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 50 walifariki dunia. Umoja wa Ulaya ulionya mwezi Machi utatoa vikwazo vipya iwapo wanasiasa na viongozi wa kijeshi watayawekea vigingi maafikiano ya mwaka jana na upinzani kuhusiana na kukataa kwa Kabila kuachia ngazi mwishoni mwa muhula wake mwaka jana.
Msemaji wa serikali Lambert Mende ambaye ni mmoja wa hao waliolengwa alisema, "vikwazo hivi vitakuwa na athari. Lazima kutakuwa na jawabu lake." Mende ambaye kwa sasa yuko China, amelengwa kutokana na ile sheria inayovikandamiza vyombo vya habari nchini humo.
EU inataka kuivuruga DRC kama Libya na Iraq
Duru ya serikali mjini Kinshasa ililiambia shirika la habari la AFP kwamba hali hiyo ni ya kutia wasiwasi na akaushutumu Umoja wa Ulaya kwa kujaribu kuivuruga Congo kama Libya na Iraq.
Wengine waliowekewa vikwazo hivyo ni waziri wa sasa wa usalama wa ndani Ramazani Shadari na mkuu wa zamani katika wizara hiyo Evariste Boshab ambaye ni rafiki mkubwa wa Kabila. Gavana wa mkoa wa Kasai Alex Kande Mupompa na gavana wa zamani wa Haut-Katanga, Jean-Claude Kazembe, pamoja na maafisa wengine wakuu na kiongozi mmoja wa jeshi pia wamewekewa vikwazo.
Umoja wa Ulaya unasema wamechangia katika matendo ya ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu nchini Congo kwa kupanga, kuelekeza au hata kuyafanya mambo hayo wenyewe.
Kabila alikataa kuondoka madarakani baada ya muhula wake kukamilika
Chini ya makubaliano yaliyoongozwa na Kanisa Katoliki nchini humo katika mkesha wa mwaka mpya, Kabila aliye na umri wa miaka 45, anastahili kusalia afisini hadi uchaguzi utakapoandaliwa mwishoni mwa mwaka 2017 ambapo pia Waziri Mkuu mpya atachaguliwa kutoka muungano wa upinzani Rassemblement.
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Congo baada ya mazungumzo kati ya serikali na upinzani January 1, 2017
Kabila
amekuwa mamlakani tangu mwaka 2001 na alikataa kuondoka madarakani
tangu muhula wake ufikie kikomo mwezi Desemba na amelaumu kucheleweshwa
kwa uchaguzi kwa ukosefu wa fedha na pia changamoto ya kuwasajili
mamilioni ya wapiga kura.Kumekuweko na hali ya wasiwasi nchini Congo tangu mwezi Desemba na mkoa wa Kasai umeshuhudia machafuko tangu Septemba, pale wanajeshi wa serikali walipomuua kiongozi wa wanamgambo Kamwina Nsapu aliyempiga rais Kabila. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa kikabila huko Kasai katika kipindi cha miezi minane iliyopita, yamesababisha zaidi ya watoto 400,000 kukabiliwa na kitisho cha kufariki kutokana na njaa.
SHARE
No comments:
Post a Comment